Mkanganyiko wizi wa kompyuta ofisi za DPP

Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam likikiri kutokea wizi wa kompyuta katika ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Waziri wa Sheria na Katiba Dk Augustine Mahiga amesema kompyuta hizo zinazodaiwa kuwa na taarifa za watuhumiwa wa uhujumu uchumi ziko salama.

Gazeti la Serikali la Habari Leo la Agosti 18 limedai kuzungumza na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyekiri kupata taarifa za wizi huo Oktoba 15 akisema wanafanya uchunguzi.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Mahiga alisema vilivyoibiwa ni vipande vya kompyuta mbili zilizokuwa katika ofisi ya DPP mkoa wa Dar es Salaam.

“Ukweli ni kwamba, ofisi ambayo ilivunjwa na baadhi ya kompyuta, si zote bali ni vipande tu. Ofisi ya Mkurugenzi mkuu wa mashitaka ya serikali haikuguswa, nyaraka zote zipo, taarifa zote zipo na kazi yake inaendelea,” alisema Dk Mahiga.

Aliendelea kusema, “Hivyo vipande vya kompyuta ni sehemu ya vizibiti ambavyo polisi wanachunguza.

“Kwanza ni ofisi ndogo ambayo haina nyaraka, bali ni ukusanyaji wa taarifa tu iko hapo Mkwepu street na siyo kompyuta zote ni vipande vya kompyuta mbili. Lakini taarifa zote zinazohusu uhujumu uchumi zipo kwa DPP na ofisi yake haikuguswa na shughuli zake ambazo ametumwa zitaendelea,” alisema.

Hadi sasa Jeshi la Polisi halijatangaza kukamata mtu yeyote anayehusishwa na wizi huo, zaidi ya kuelezwa kuwa wanaendelea na uchunguzi, huku DPP Biswalo Mganga akiwa kimya.

Utata zaidi umeibuka baada ya Kamanda Mambosasa aliyetoa taarifa ya kufanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuahirisha mkutano huo, bila kutoa sababu.

Hata mkutano wa Waziri Mahiga na waandishi wa habari haukulenga kuzungumzia suala hilo, bali mkutano wa mashauriano ya kisheria kati ya nchi za Asia na Afrika, jambo linaloendeleza utata huo.

Dk Mahiga alizungumzia suala hilo baada ya kuulizwa swali na mwandishi wa habari wa Mwananchi.

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa sheria ya Plea bargaining, Mahiga alisema ni mwendelezo wa mapambano ya uhujumu uchumi yaliyoanza miaka ya 1970.

“Kihistoria kumekuwa na changamoto za kiuchumi tangu miaka ya 1970. Tangu vita ya Kagera ilipotokea. Kuna changamoto zilizotoka na na vita vile. Marehemu (Edward) Moringe Sokoine alikabidhiwa jukumu hilo la kupambana wafanyabiashara wachache waliokuwa wakaficha bidhaa na kupandisha bei,” alisema.

“Tofauti ya wakati ule wafanyabiashara walikuwa wanaficha bidhaa, lakini kwa sasa wajhujumu uchumi wanaiibia Serikali na kwa hivyo kuwaibia raia wake kwa mbinu mbalimbali kama kutorosha bidhaa kama vile dhahabu na madini mengine na kukwepa kulipa kodi,” alisema.

Mashauriano ya kisheria Asia na Afrika

Awali akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mahiga alisema Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa mashauriano ya kisheria kwa nchi za Asia na Afrika (Asia, Afrika Legal Consultative Consultative Organization- AALCO) utakaofanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 21 hadi 25.

Alisema mkutano huo utakaofunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu kwa niaba ya Rais Magufuli utahudhuriwa na mawaziri wa sheria kutoka nchi 48 za Asia na Afrika.

Alitaja mambo yatakayojadiliwa kuwa ni pamoja na sheria ya kimataifa ya bahari, kuvunjwa kwa sheria ya kimataifa nchini Palestina na maeneo mengine yanayoshikiliwa na nchi ya Israel na masuala mengine yanayohusiana na Palestina.

Mengine ni sheria ya kimataifa katika masuala ya mitandao, utatuzi wa migogoro kwa amani, sheria ya kimataifa katika biashara na uwekezaji, matumizi ya sheria za nje ya nchi, vikwazo dhidi ya nchi nyingine na tume ya sheria ya kimataifa.

Akifafanua zaidi kuhusu AALCO alisema ilianzishwa mwaka 1956 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kufanyika mkutano wa Bandung Indonesia wa mwaka 1955 uliozaa nchi zisizofungamana na upande wowote.

“Ilikiwa ni kuendeleza ukombozi wa nchi ambazo bado zilikiwa hazijakombolewa. Chombo hiki kiliundwa ili kutumika kama jukwaa la ushauri wa wataalamu katika kubadilishana taarifa na maoni kwa nchi za Asia na Afrika,” alisema.

Alisema Tanzania ilianza kushiriki mikutano ya AALCO mwaka 1965 lakini ilikuja kujiunga rasmi mwaka 1973.

Akifafanua zaidi kuhusu shirika hilo, Katibu Mkuu Profesa Kennedy Gaston alisema lina lengo la kujadili

masuala ya sheria kabla ya kwenda Umoja wa Mataifa, kutoa ushauri kuhusu sheria za kimataifa, kujange uwezo kwa sheria na maeneo mapya ya sheria za kimataifa na kuendeleza sheria za kimataifa hasa biashara na uwekezaji.