Mkapa ataka tume huru ya uchaguzi

Dar es Salaam. Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ni njia mojawapo ya kuondoa manung’uniko ya vyama vya siasa na kuimarisha demokrasia barani Afrika.

Mkapa, rais wa kwanza wa Tanzania kuchaguliwa katika mfumo wa vyama vingi, ameandika hayo katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” ambacho kinazungumzia matukio na maamuzi aliyofanya katika utawala wake wa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, akijutia na kukubali kubeba lawama zote kwa baadhi ya matukio, huku akieleza somo alilopata.

Mkapa amesema ili kuwa na usawa katika mfumo wa vyama vingi nchini, ni muhimu kuwa na chombo huru kilichojumuisha vyama vyote.

“Kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi itakayokubalika na vyama vyote vya siasa ndio chachu ya kulea na kukuza demokrasia nchini,” anasema Mkapa, ambaye anasema alipata funzo kubwa la umuhimu wa kushirikiana na vyama vya siasa baada ya mauaji ya wafuasi 22 wa CUF yaliyofanywa na polisi kisiwani Pemba mwaka 2001.

Mkapa anatahadharisha kuwa muundo wa tume umekuwa miongoni mwa masuala yanayopigiwa kelele na kupata upinzani mkubwa kutokana na upatikanaji wa viongozi wake.

Anashauri kuwa mamlaka ya nchi inaweza kubaki na mamlaka ya kuteua mwenyekiti wa tume ingawa lazima vyama vya upinzani vishirikishwe kwa uwazi katika suala zima la kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

“Hatua hii itasaidia kupunguza malalamiko na pia vyama vya upinzani vitajenga imani na tume ya uchaguzi,” alieleza Mkapa, ambaye aliwahi kusuluhisha migogoro ya kisiasa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kenya, Sudan Kusini na Burundi.

Mkapa anasema kumekuwa na malalamiko mengi ya vyama vya siasa vikidai kutotendewa haki na tume na kilio hicho ni katika nchi nyingi za Afrika.

Ameonya kuwa malalamiko hayo ya kutotendewa haki kwenye uchaguzi ndio yamekuwa kichocheo cha kuzuka kwa machafuko katika nchi nyingi.

Maoni ya Mkapa ni mwendelezo wa kilio cha muda mrefu cha vyama vya upinzani nchini.

Vyama hivyo vinasema mwenyekiti wa tume huteuliwa na Rais, ambaye pia anaweza kubadilisha wakurugenzi wa chombo hicho.

Pia wasimamizi wa uchaguzi wilayani ni wakurugenzi wa wilaya, ambao pia ni wateule na katika kesi iliyofunguliwa na wanaharakati na vyama vya siasa, Mahakama Kuu ilibatilisha mamlaka ya wakurugenzi hao katika uchaguzi baada ya kuridhika kuwa zaidi ya sabini walikuwa ni makada wa CCM.

Hata hivyo, Serikali ilikata rufaa na kushinda.

Mapendekezo ya kuundwa kwa tume ya huru ya uchaguzi yamewahi kupendekezwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1991, Tume aliyoiunda Mkapa ya Jaji ya Robert Kisanga mwaka 1998 na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2012 ambazo zote zilikusanya maoni ya wananchi.

Kwa sasa kuna sintofahamu nchini juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 24, huku vyama saba vikitangaza kujitoa kupinga uendeshaji wa uchaguzi huo.

Mkapa, ambaye amezungumzia demokrasia kwa ujumla barani Afrika, anapendekeza pia vyama vya siasa kupewa nafasi ya kueneza sera zao na kuitisha mikutano ya hadhara kwa uhuru.

Kuhusu kipindi chake, anasema hakukuwa na malalamiko dhidi ya tume kwa kuwa iliundwa na majaji walioheshimika katika jamii, lakini akasema vyama havikuwa vinaridhishwa na suala la kuhesabu na kutangaza matokeo na ndio maana wakaruhusu wawakilishi wa vyama tofauti kwenye vituo vya kupigia kura.

Uhuru wa mikusanyiko

Mkapa pia anasema katika kitabu chake kuwa angependa kuona vyama vya siasa vikipewa nafasi ya kufanya shughuli zao kwa uhuru.

“Ninapenda kuona vyama vyote vya siasa vikipewa fursa sawa kuhamasisha wanachama, kufanya mikutano ya hadhara na kutangaza manifesto (ilani) zao,” anasema Mkapa.

Anasema tatizo ambalo analiona kwa sasa ni chama tawala kuendesha mambo kama vile kipo katika mfumo wa chama kimoja.

“Tatizo ninaloliona ni kuwa tulipoingia katika mfumo wa vyama vingi tuliiga demokrasia ya nchi za Magharibi ya mshindi kunyakua kila kitu na kuwatenga wengine katika masuala ya utawala,” anasema Mkapa.

“Nadhani si jambo zuri na hasa likija suala zima la kuimarisha umoja wa kitaifa.”

Pia Mkapa, ambaye hakuwa na urafiki mzuri na vyombo vya habari nchini, anashauri vyombo vya habari vya serikali kutoa nafasi kwa habari za vyama vya upinzani.

“Kumekuwa na malalamiko mengi ya chama tawala ya kubebwa kutokana na kutumia nyenzo za Serikali kufanya shughuli zao tofauti na vyama vya upinzani. Ninashauri uwepo kwa usawa sasa kwa vyama vyote katika nchi,” anasema Mkapa.

Mkapa anasema maridhiano ndio njia pekee itakayosaidia kumaliza mivutano ya kisiasa, kukuza demokrasia na kuimarisha umoja wa kitaifa.