Mkemia kuchunguza vifo vya wanajeshi 10

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo

Dar/Njombe. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amesema sampuli za wanajeshi 10 waliokufa katika mazoezi ya kijeshi zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.

Wakati Mabeyo akieleza hayo jana Ikulu, Dar es Salaam baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, mjini Njombe Polisi watatu wamekufa na wengine tisa kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongana na basi na kampuni ya Sharon linalofanya safari kati ya Njombe na Arusha.

Jana Ikulu, Rais Magufuli alitoa pole kwa vifo vya watu 20 katika kongamano wa Nabii na Mtume, Boniface Mwamposa vilivyotokea mjini Moshi, vifo vya watu 21 mkoani Lindi baada ya nyumba zao kusombwa na maji na vifo vya wanajeshi hao 10.

Mabeyo alisema wanajeshi hao walikuwa kwenye mazoezi ya kawaida ya kutembea lakini baada ya saa mbili, hali zao zilianza kubadilika wakiwa eneo la Msata, walipelekwa hospitali ya Jeshi ya Lugalo.

Alieleza baada ya kulazwa hospitalini hapo, baadhi yao walifariki na wengine hali zao ziliimarika.

“Tunahisi walikula chakula chenye sumu, labda wakati wanatembea walinunua vyakula barabarani vikawadhuru. Mazoezi yalikuwa ya kawaida tu,” alisema na kuongeza:

“Tumepeleka sampuli za waliofariki kwa Mkemia Mkuu ili kubaini chanzo hasa cha vifo,” alisema Mabeyo akizungumzia vifo hivyo vilivyotokea Januari 30.

Kuhusu ajali iliyosababisha vifo vya polisi watatu, mganga mfawidhi wa Hospitali ya Kibena-Njombe, Dk Anord Mtega Maganga alithibitisha kupokea miili ya askari polisi hao, kwamba wengine tisa ni majeruhi.

Ajali hiyo ilitokea jana alfajiri eneo la kituo cha Polisi cha Mkoa wa Njombe.