Mkopo uliokwama Benki ya Dunia watoka, sababu za kukwama zatajwa

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) hatimaye jana ilifikia muafaka na Serikali kutoa mkopo wa Dola500 milioni (Sh1.2 trilioni) kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari nchini Tanzania.

Benki ya Dunia ilichelewa kutoa fedha hizo kufuatia maombi ya baadhi ya wanasiasa wa upinzani na asasi za kiraia waliokuwa wanataka watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa mashuleni waruhusiwe kuendelea na masomo kwenye mfumo wa elimu wa kawaida.

Mkopo huo wa Benki ya Dunia utakaoanza kutolewa mwaka 2021, unatazamiwa kunufaisha wanafunzi milioni 6.5 wanaopata elimu ya sekondari huku nusu yao wakiwa wasichana.

Hao ni sehemu ya mpango wa mradi wa miaka mitano wa kuboresha elimu ya sekondari nchini Tanzania (SEQUIP).

Taarifa ya Benki ya Dunia ilisema, “mradi huu utawasaidia wasichana waliopata ujauzito, wasichana wadogo wenye watoto na wanafunzi wengine waliolazimika kuacha shule kwa matatizo mbalimbali.

“Sasa hii itakuwa fursa kwao kurudi shuleni na kuendelea na masomo kama kawaida kwenye mfumo rasmi. Mradi huu una lengo la kusaidia wasichana wanaopata ujauzito wakiwa mashuleni kwa kuzingatia ushauri wa vyama vya kiraia nchini Tanzania na duniani kote,” iliongeza.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Mara Warwick alisema mradi wa SEQUIP utawapa kipaumbele wasichana wadogo waliopata ujauzito.

“Hii ni hatua kubwa sana katika kukabiliana na changamto zinazowakabili watoto wa kike kupata elimu nchini Tanzania,” aliongeza.

Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alisema mkopo huo umetolewa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya elimu.

“Tunawashukuru watu wote wenye nia njema waliotuunga mkono katika suala hili,” aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter jana na hakupatikana kutoa ufafanuzi wa ziada.

Mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe na baadhi ya wanaharakati nchini Tanzania waliendesha kampeni ya kuiomba Benki ya Dunia kutotoa mkopo huo kwa Tanzania kwa madai ya kuwepo matatizo katika masuala ya haki za binadamu.

Sababu nyingine ya kuzuiwa kwa muda kwa fedha hizo ni madai ya mfumo wa elimu ya Tanzania kutoruhusu wanafunzi wa kike kuendelea na masomo pale wanapopata ujauzito.

Akizungumzia uamuzi wa Benki ya Dunia wa kutoa fedha hizo, Kabwe alisema mkopo huo umetolewa na sharti la wasichana kuruhusiwa kurudi shuleni pale wanapopata ujauzito.

“Nilipoandika barua Benki ya Dunia niliwaomba wasitoe fedha hizo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020 kwa kuhofia fedha hizo zinaweza kutumika kwenye masuala ya uchaguzi badala ya kusudio lake. Sasa fedha hizo zitaanza kutolewa 2021 na asilimia 4% tu ndiyo itakayotolewa.

“Asilimia 96 ya fedha hizo zitatolewa baada ya wakala huru kufanya ukaguzi na Benki ya Dunia kuridhia,” aliongeza Zitto.

Baada ya muafaka huo, sasa Benki ya Dunia na Serikali wanaweza kuanza utekelezaji wa makubaliano baina yao kuhusiana na utoaji wa mkopo huo.

Awamu ya kwanza ya mkopo huo itaanza kutolewa 2021, ambapo kiasi cha Dola72.47 milioni (Sh166 bilioni) zinatazamiwa kuanza kutolewa.

Fungu jingine la mkopo litatolewa mwaka 2022, ambapo zitatoka Dola 101.10 milioni (Sh233 bilioni), mwaka 2023 kiasi cha Dola114.73 milioni (Sh263 bilioni) na mwaka 2024 kiasi cha Dola98.52 milioni (Sh226 bilioni).

Fedha nyingine zitatolewa mwaka 2025 kikiwa ni kiasi cha Dola85.37 milioni (Sh196 bilioni) na fungu la mwisho litatolewa mwaka 2026, ambacho kitakuwa kiasi cha Dola27.81 milioni (Sh64 bilioni).

Kipaumbele cha fedha ni kuelekezwa katika maeneo manne kwa ajili ya kuboresha elimu ya sekondari.

Maeneo hayo ni pamoja na kuwajengea uwezo wasichana kupata elimu ya sekondari na kujifunza stadi za maisha.

Wasichana watapatiwa elimu hiyo bila ya matatizo katika shule au vituo maalum, ambapo inakadiriwa wasichana wapatao 900,000 watanufaika kutokana na mpango huu.

Eneo la pili linalowekewa mkazo kwenye mradi huo ni uendelezaji wa elimu ya sekondari na kuanzishwa kwa mfumo wa kufundisha masomo ya sayansi na hesabu kwa njia ya kidijitali ili kusaidia wanafunzi kuelewa masomo hayo na pia kuongeza ufanisi wa waalimu.

Pia mazingira ya shule za sekondari yataboreshwa.

Madhumuni mengine ya mradi huo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga shule mpya za sekondari ili ziwe karibu na makazi ya watu.

Mradi utaweka mkazo katika kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira ya kutoa elimu bora na kwa usalama.

Ili kufanikisha jambo hili, fedha za kutosha zitatolewa ili kuhakikisha ongezeko la wanafunzi haliathiri utoaji wa elimu ya sekondari.

Eneo la nne ambalo linatazamiwa kuwekewa mkazo na mradi wa SEQUIP ni kujengewa uwezo wa watu wanaohusika katika kupanga na kufanya maamuzi kwenye sekta ya elimu.

Vyama vya walimu na wazazi na bodi za shule zitapatiwa mafunzo maalumu ili kuwasaidia kulinda usalama wa wanafunzi na hasa wale wa kike.

Akitoa maoni yake kuhusu uamuzi wa Benki ya Dunia, mshauri wa masuala ya elimu na mhadhiri wa zamani, Dk Thomas Jabil alisema kuwa fedha hizo zinatolewa katika kipindi muafaka kwani kwa sasa sekta ya elimu nchini Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi.

“Kwa kweli si jambo jema kumnyima mtoto haki ya kupata elimu. Ninaona Serikali ishirikiane na Benki ya Dunia ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazowakabili wasichana kupata elimu,” alishauri.

Mradi huo wa kuboresha elimu ya sekondari nchini Tanzania unatazamiwa kutelekezwa chini ya programu mpya ya Benki ya Dunia inayoshughulikia masuala ya jamii na mazingira.

Katika makubaliano hayo ya kupata mkopo huo, serikali imepanga kujadiliana na wadau mbalimbali zikiwamo asasi za kiraia ili kupata maoni yao kuhusiana na utekelezaji wa mipango yake ya kujenga shule za sekondari katika maeneo yenye mazingira bora na salama.