Msafara wa Mengi wazuiwa saa moja kijijini

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi baada ya kuwasili nyumbani kwake, katika Kijiji cha Foo Nkweseko, Macheme, Mkoani Kilimanjaro. Picha na Dionis Nyato

Hai. Nyumbani ni nyumbani. Ndivyo unavyoweza kuelezea mapokezi waliyoyatoa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa mwili wa aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Mengi aliyezaliwa Mei 29, 1942 Kijiji cha Nkuu, Machame mkoani hapa jana, mwili wake ulirejeshwa nyumbani kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika leo.

Umati wa watu ulijitokeza kwa wingi kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kuupokea mwili wa mfanyabiashara huyo aliyefariki usiku wa kuamkia Mei 2, akiwa Dubai, Falme za Kiarabu.

Katika maeneo mbalimbali ulipopita mwili wake wananchi waliingia barabarani na kuligusa gari la kifahari lililobeba jeneza lililokuwa limebandikwa mbele na nyuma maandishi yaliyosomeka Rest in Peace Dr R.A. Mengi.

Wasimamishwa saa nzima

Baada ya msafara huo uliokuwa na magari zaidi ya 20 kufika Kijiji cha Nkwarungo, kilomita chache kutoka nyumbani kwake, wananchi walisimamisha msafara huo kwa zaidi ya saa moja.

Lengo la wananchi hao kusimamisha msafara huo walitaka jeneza hilo lishushwe ili walibebe hadi Kijiji cha Nkweseko ambako ndiko mwili wake ulikuwa unapelekwa.

Licha ya polisi kuwataka wananchi hao wakiwemo wanafunzi na madaktari waondoke, hawakufanya hivyo, hali iliyosababisha baadhi ya viongozi waliokuwa kwenye magari kushuka na kwenda kuwasihi wananchi hao waliokuwa wakiimba ‘tunataka tumbebe tunataka tumbebe’ kuruhusu msafara uendelee.

Wananchi hao walikuwa wamezingira gari hilo huku wengine wakiwa wamebeba majani ya sale na majani mengine ya miti.

Majani ya sale hutumiwa na wananchi wa kabila la Wachaga kuonyesha heshima, upendo na amani.

Hata hivyo, baada ya kuona gari lililobeba mwili limesimama muda mrefu na haliondoki, baadaye king’ora cha gari la polisi kililia ili kuwatawanya wananchi, jambo lililoruhusu safari kuendelea.

Baada ya mwili wa Mengi kuwasili nyumbani kwake, vilio na simanzi vilitawala pale mkewe, Jacqueline alipoangua kilio kilichosababisha waombolezaji waliojitokeza kuanza kulia.

Mwili ulivyowasili Kia

Awali, mwili wa mfanyabiashara huyo ulipowasili Kia, baadhi ya wanafamilia waliokuwepo waliangua vilio baada ya kuona ukishushwa kwenye ndege ya Shirika la Precision Air. Mwili huo ulipowasili ulipokewa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa, Anna Mghwira (Kilimanjaro), Christopher Ole Sendeka (Njombe) na Paul Makonda (Dar es Salaam) pamoja na wakuu wa wilaya za mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Mwili ulipotolewa uwanjani hapo kwenda Machame, maelfu ya wananchi walijipanga barabarani kuulaki huku wakipiga ukunga (yowe), huku wengine wakiwa wameshikilia majani mikononi.

Vilevile baadhi ya watu walitandika majani ya sale barabarani huku wengine wakiyapiga chini wakipiga mayowe.

Ujenzi wa kaburi

Hadi jana mchana ujenzi wa kaburi atakalozikwa Mengi ulikuwa unaelekea katika hatua za mwisho.

Kunda Sawe, fundi mkuu wa ujenzi wa kaburi hilo akizungumza na Mwananchi mchana nyumbani hapo alisema walikuwa wanakamilisha upakaji rangi na walitarajia kukamilisha kazi hiyo jana jioni.

“Kwa sasa tunamalizia ujenzi wa kaburi hili na mpaka ifike jioni (ya jana) tutakuwa tumekamilisha,” alisema Sawe.

Kaburi la mfanyabiashara huyo liko jirani na lile la mwanaye, Rodney Mutie aliyefariki dunia 2005.

Kuagwa na kuzikwa

Leo mwili wa Mengi utapelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Moshi mjini kwa ajili ya ibada na kuagwa, kisha utasafirishwa hadi kijiji cha Nkuu Sinde, Machame ambako ndiko atazikwa.

Katika mazishi hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Serikali.

Hadi mauti yanamfika, Mengi alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (Moat) na pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Nyadhifa nyingine ambazo aliwahi kushika ni pamoja na kamishna wa Kamati Inayoshughulikia Mishahara (SRC), mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA), mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mwenyekiti wa Baraza la Wafanyabiashara Afrika Mashariki na kamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids).