Msimamo wa Bashiru katika mambo haya matano

Mei 29 mwaka 2018, Chama cha Mapinduzi (CCM) kilifanya mabadiliko ya mtendaji wake mkuu kwa kumteua Dk Bashiru Ally kuvaa viatu vilivyoachwa na Abdulrahman Kinana.

Baada ya safari ya mwaka mmoja na ushehe ya utendaji wake ndani ya chama hicho tawala, Dk Bashiru anakutana na wahariri wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wachapishaji wa Magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na kutoa msimamo wa mambo matano ambayo bado yalikuwa yakiacha maswali kwenye vichwa vya wananchi.

Mazungumzo hayo yaliyorushwa mubashara kupitia mitandao ya kijamii ya MCL, yalisikilizwa na wananchi wengi ambao pia waliuliza maswali na naye aliyajibu.

Miongoni mwa maswali lililoulizwa na mfuatiliaji wa mahojiano hayo ni lile lilihusu mkwamo wa upatikanaji wa kadi za kielektroniki za chama hicho, licha ya watu kujiandikisha ili wazipate.

Akijibu hilo, Dk Bashiru alikiri kuwa kwa sasa kadi hizo hazitoki kutokana na sababu kuu nne.

Anasema awali walikubaliana mkandarasi wa kutengeneza kadi hizo atoke nje ya nchi, lakini Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli akashauri awe mzawa.

Alitaja mambo hayo manne yanayosababisha kadi hizo kutokutoka kuwa ni suala la usalama, gharama, ubora na ukubwa wa chama hicho.

Anasema kadi hizo zikitengenezwa nchini zitakuwa salama, lakini kutokana na ukubwa wa chama hicho, kinahitaji kuwa na kadi bora zaidi lakini zenye gharama nafuu ili wanachama wao waweze kumudu kuzinunua.

Katika mahojiano hayo, Dk Bashiru aliulizwa swali linalohusu ukimya wa utekelezaji wa mapendekezo ya tume aliyoiunda kufanya uhakiki wa mali za chama hicho nchi nzima, alisema inatekelezwa.

Dk Bashiru alisema tume aliyoiongoza ilitakiwa ipendekeze namna ya kuzuia wizi wa mali za chama na si kufukua makaburi.

“Siku tunamkabidhi mwenyekiti (Rais John Magufuli) alisema humu kwenye ripoti tukianza kufukua makaburi tutakosa mahali pa kuyaweka, akasema lakini tunataka ripoti hii izuie ufujaji wa mali za chama,” alisema Dk Bashiru.

Alisema waliokuwa wezi wa mali hizo sasa hivi wamempachika jina la ‘mzee wa swaumu kali au control number’ akisema, “kuna matawi Dar es Salaam walikuwa wanalipana posho ya kikao kimoja Sh500,000, lakini sasa hivi ni Sh40,000, kwa nchi nzima. Kwa hiyo, katika mazingira haya hawawezi kukupenda.”

Anasema wamefanya uhakiki wa mali na kufikia nusu, lakini hadi sasa thamani ya mali za CCM ni Sh1 trilioni.

“Nilipoingia walikuwa wanasema Sh50 bilioni, tumefanya tathimini inafikia Sh1 trilioni, kwa hiyo msingi wa tume yangu si kufufua makaburi bali kufunga makufuli ya wizi na tusiwe ombaomba.”

“Nimeingia kwenye chama nimekuta akaunti ina Sh3 bilioni lakini sasa kuna Sh31 bilioni na mikutano nafanya, ziara zote tunafanya kutoka kwenye Sh3 bilioni,” alisema Dk Bashiru.

Anasema Ilala jijini Dar es Salaam waliwakuta wana Sh1 milioni kwenye akaunti lakini hadi juzi walikuwa

na Sh1.4 bilioni na hawajaongeza banda wala mradi, Arusha walikuwa na Sh500,000 lakini sasa wana zaidi ya Sh100 milioni.

“Mwizi yeyote ndani ya chama hana nafasi, mali bado ni nyingi mno na hizi zingine bado hazijaanza kutumiwa vizuri,” alisema Dk Bashiru.

Zuio la mikutano ya kisiasa

Kuhusu zuio la mikutano ya kisiasa hasa kwa wanasiasa wa upinzani, Mtendaji Mkuu huyo wa CCM anasema anachokifahamu yeye hakuna zuio la mikutano ya kisiasa na kwa wabunge na madiwani.

Anasema wananchi waliichagua CCM ili iweze kuwaongoza kwa nafasi ya urais, kwa hiyo kuna wakati inapokuwa inatekeleza shughuli mbalimbali upande wa pili wanatoa lugha chafu dhidi ya viongozi na serikali jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

Dk Bashiru anasema hata yeye tangu aingie kwenye nafasi hajawahi kufanya mkutano wa hadhara ukiondoa ile ya uchaguzi mdogo wa udiwani na ubunge pindi inapofanyika.

Anasema mikutano mingine ni ile ya ndani na anapoonekana maeneo mbalimbali yeye au viongozi wengine wa CCM wanakwenda kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo waliinadi kwa wananchi na kuwachagua.

Hata hivyo, kumekuwapo na mazuio ya mikutano ya wabunge na madiwani wa upinzani kwenye maeneo yao kutokana na kile kinachoelezwa na Jeshi la Polisi kwamba uwapo wa taarifa za kiinterejensia kunasababisha ipingwe marufuku.

Tume huru ya uchaguzi

Kuhusu mjadala wa uwapo wa tume huru ya uchaguzi, Dk Bashiru anasema kuna mazingira mengi yanayopima uwapo kwa uhuru na amani wakati wa uchaguzi, ikiwamo kwa wanasiasa wenyewe na tume ya taifa ya uchaguzi kila mmoja kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Alisema kamati kuu ya chama hicho iliyokutana hivi karibuni imeagiza Serikali ya Muungano na ya Zanzibar kuhakikisha zinasimamia uchaguzi huo ili uwe wa amani, huru na haki huku akiwataka wanasiasa kuendelea kubainisha kasoro zilizopo ili ziweze kufanyiwa kazi.

“Kinachoweza kusababisha uchaguzi usiwe huru ni pamoja na watu wenyewe kutokusimamia haki,” anasema Dk Bashiru.

Anasema katika uchaguzi kuna jukumu la jamii, wanasiasa na tume kama chombo na, “mimi kwangu, mazingira bora na ya kisiasa yanaifanya tume kuwa huru na kwa wanasiasa wafuate sheria na tume ifuate sheria ili haki iweze kutendeka.”

Mtendaji mkuu huyo wa CCM anawataka wanasiasa kuwekeza nguvu katika kuandaa kura badala ya kupiga kelele na kuweka visingizio.

Kuhusu CCM kubebwa na polisi alisema, “Polisi hawawezi kuibeba CCM, CCM ni kubwa mno kuliko polisi, tuna wanachama zaidi ya milioni kumi, labda vyama hivi vidogovidogo, sisi tuna ahidi na kutekeleza.”

Onyo kwa Ma RC, DC

Dk Bashiru alitumia fursa hiyo kutoa onyo kwa wakuu wa mikoa na wilaya wanaotamka hadharani kuwa hawaezi kushirikiana na wabunge na madiwani wa upinzani.

Anasema viongozi wenye msimamo wa aina hiyo hawajui wanachokifanya na kwamba, wasipobadilika watapoteza nafasi zao.

Msingi wa onyo hilo ulitokana na swali lililoulizwa na moja ya wafuatiliaji wa mahojiano hayo aliyetaka kupata msimamo wa CCM juu ya kauli ya wakuu wa mikoa kutangaza kutoshirikiana na madiwani na wabunge wa upinzani.

“Ni marufuku kwa wakuu wa wilaya na mikoa kutoshirikiana na wenzao waliopewa dhamana na wananchi, wajiandae kabisa akiwamo mkuu wa mkoa wa aina hiyo kupoteza kazi,” anasema Dk Bashiru.

Ingawa muulizaji wa swali hilo hakutaja jina la aliyekuwa akimlenga, lakini Februari 11 mwaka juzi, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Haydom wilayani Mbulu, aliwataka madiwani wa upinzani kujiunga na CCM ili waweze kushirikiana naye.

Alisema yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.

Katika mahojiano yake, Dk Bashiru anasema wakuu wote wa mikoa na wilaya wako chini ya Rais aliyechaguliwa nchi nzima na wanamwakilisha kwenye maeneo yao.

Anasema Rais aliapa kuilinda Katiba na kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi na ndiye Rais anayesema maendeleo hayana chama na wao wanapaswa kusema hivyo kwenye maeneo yao.

Mnyeti alitangaza marufuku hiyo baada ya mkazi wa kata ya Hayderer, John Tluway kuuliza swali akitaka kujua sababu za mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga kutofika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema.

hilo, Mnyeti alimpongeza Mofuga kwa kutokufika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema kwa maelezo kuwa diwani wa kata hiyo anapaswa kujiunga na CCM ili kufanikisha maendeleo.

Sakata la Membe

Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza ni uamuzi uliochukuliwa na chama hicho wa kumfukuza katika chama hicho, Bernard Membe huku akiwataka wana CCM kutofurahia kwa hatua hiyo bali wahuzunike kwani ni msiba.

Februari 28, kamati kuu ya chama hicho yenye wajumbe 24 chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli iliridhia kwa kauli moja kumfukuza uanachama Membe baada ya kukutwa na hatia ya uvunjifu wa maadili.

Kauli ya Dk Bashiru imekuja siku chache baada ya kada huyo kudai kuwa alifukuzwa CCM kutokana na nia yake ya kutaka kupambana na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Hata hivyo, Dk Bashiru amemtaka Membe kama ana ndoto ya kugombea urais, asake tiketi ya chama chochote cha siasa ili wakutane uwanjani Oktoba mwaka huu.

Membe na makatibu wakuu wawili wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba walifikishwa mbele ya kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kujibu mashtaka ya kinidhamu.

Makada hao waliingia matatani baada ya sauti zao pamoja na za wanachama wengine watatu, kusambaa katika mitandao ya kijamii ikizungumzia kuporomoka kwa umaarufu wa chama hicho na uenyekiti wa Magufuli.

Makamba alisamehewa makosa yake wakati Kinana atakuwa chini ya matazamio kwa miezi 18, kipindi ambacho hataruhusiwa kugombea uongozi, wakati Membe amevuliwa uanachama na hivyo hataweza kutimiza ndoto yake ndani ya chama hicho.

Dk Bashiru alisema Katiba haimnyimi nafasi ya kugombea kupitia vyama vingine 19 vilivyobaki huku akidokeza kwamba kinachosubiriwa sasa ni maazimio ya kamati kuu kumtimua Membe kupelekwa katika Mkutano wa Halmashauri Kuu kwa ajili ya uamuzi wa mwisho ambao unaweza kubariki uamuzi huo au kuupinga.