Mtoto wa miaka 10 aozeshwa Tanzania

Wednesday March 25 2020

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Kiteto. Matukio ya ukatili kwa jamii ya wafugaji dhidi ya watoto wilayani hapa mkoani Manyara yamezidi kukithiri, baada ya mtoto wa miaka 10 mkazi wa kijiji cha Seki kata ya Partimbo kuozeshwa na wazazi wake kwa mahari ya Sh10,000.

Mtoto huyo aliolewa mwaka jana baada ya kulipiwa mahari hayo na kuishi kinyumba kwa mwaka mmoja na Baraka Melau (48).

Akizungumza juzi mtoto huyo alisema alitoroka alikokuwa ameolewa baada ya kuona mateso yanazidi.

Alisema aliolewa mwaka jana baada ya wazazi wake kulipwa mahari ya Sh10,000 na kutoa idhini ya kuondoka nyumbani kwao na kuishi na mwanaume huyo.

Mtoto huyo alisema baada ya kuolewa alifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwamo kukeketwa huku akifanyiwa mateso makali kwa kuingiliwa kinyumba kabla kidonda hakijapona.

“Nilipoona mateso yanazidi nilimsimulia mama mmoja jirani yetu aliyeniambia nikatoe taarifa polisi kisha wakanisaidia kunipeleka ofisi za maofisa wa maendeleo ya jamii Kiteto,” alisema.

Advertisement

Mmoja kati ya wasaidizi wa kisheria wilayani Kiteto, Mwadawa Ally alisema kupitia shirika lao la Kiwocodia walipata taarifa ya mtoto huyo na kumchukua hadi sasa wanaishi naye.

Mwadawa alisema wanalifuatilia suala hilo tangu kituo cha polisi hadi ofisi za maendeleo ya jamii wilayani Kiteto, huku wakiwafuatilia pia wazazi wake.

“Wazazi wake walikimbia makazi baada ya kupata taarifa kuwa suala hilo limefika polisi linafuatiliwa kwa ukaribu na wasaidizi wa kisheria,” alisema.

Hata hivyo, mwanaume anayedaiwa kumuona mtoto huyo, Melau alisema ni jambo la kawaida kwa jamii ya wafugaji wa Kimasai kuoa wake wengi wakiwamo wasichana ilimradi alipe mahari kwa wazazi.

“Nililipa mahari ya Sh10,000 kwa wazazi wa huyu binti ila akatoroka baada ya kuishi naye kwa mwaka mmoja na hadi sasa sijui amekimbilia wapi naendelea kumtafuta,” alisema Melau.

Hata hivyo, licha ya sheria zilizopo kupingwa na wanaharakati kuhusu umri wa mtoto wa kike kuolewa, hakuna hata moja inayoruhusu mtoto kuolewa akiwa na miaka 10 bali miaka 14 kwa kibali cha mahakama au 15 kwa ridhaa ya wazazi.

Advertisement