Mwalimu Nyerere angesifu, kukemea mengi-wananchi

Wananchi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye maandamano ya amani ya kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere yaliyofanyika katika Barabara ya Nyerere jijini Mwanza juzi. Picha na Johari Shani

Dar/mikoani. “Kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere angekuwepo leo angekemea mambo gani?”, ni swali ambalo Mwananchi iliuliza kwa watu tofauti kutaka kujua jinsi anavyokumbukwa, na limezaa mambo kadhaa ambayo wanaona hayaendi sawa.

Na “kama angekuwepo angesifia mambo gani?” Ni swali jingine la utafiti wa Mwananchi kwa wananchi ikiwa ni kuenzi miaka 20 ya kumbukumbu ya kifo cha kiongozi huyo wa harakati za uhuru wa Tanganyika na muasisi wa Taifa la Tanzania.

Mambo ambayo watu hao wanaona angekemea ni rushwa, unafiki, viongozi kutowajibika wanapokosea, kutofuatwa kwa Katiba, ukandamizaji wa demokrasia, uhuru wa kujieleza na mmomonyoko wa maadili.

Pia walisema Nyerere angekemea mauaji yanayohusisha watu wasiojulikana, uonevu, uzembe, ufisadi, ubaguzi katika maendeleo na kukosekana uzalendo.

Lakini katika swali la pili walisema Nyerere angefurahishwa na namna Serikali ya Awamu ya Tano na hivyo kumpongeza Rais John Magufuli kwa namna alivyoboresha miundombinu ya usafiri na huduma za kijamii kama afya na elimu.

Maoni hayo yalitolewa juzi, Oktoba 14 siku ambayo Nyerere alifariki dunia akiwa jijini London ambako alipelekwa kutibiwa. Nyerere aliyeongoza Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka mwaka 1961 hadi mwaka 1985 alipong’atuka, anasifika kwa siasa za Ujamaa na Kujitegemea, Azimio la Arusha, usawa na utu na harakati za ukombozi barani Afrika.

Anasifika pia kwa kusimamia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utengemano wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti yaliyojikita katika masuala hayo.

“Angeshangaa sana kuona watawala hawafuati Katiba katika kuongoza, viongozi kupenda kusifiwa na viongozi kudidimiza demokrasia,” alisema mtu aliyejitambulisha kwa jina la Gregory Mwafube.

“Mfano mtoto wa Mwalimu alienda upinzani ambako kwa leo kiongozi wa Serikali asingethubutu kumruhusu mtoto au ndugu kuingia upinzani.

“Angeukemea kwa nguvu zake zote utawala wa kimabavu. Oneni watu wamegoma kujiandikisha, kwa sababu wanadhulumiwa haki yao!”

Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, alijiunga na NCCR-Mageuzi wakati nchi iliporudi katika siasa za vyama vingi na mwaka 1995 aligombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini na kushinda. Nyerere hakuonekana kukerwa na kitendo cha mwanawe na badala yake alizunguka nchini kumpigia kampeni mgombea urais wa CCM, Benjamin Mkapa.

Makongoro Nyerere amesharudi CCM na mwaka 2015 aliomba bila mafanikio ridhaa ya chama hicho agombee urais.

Ingawa Serikali ya sasa imefanya kazi ya kupambana na rushwa na ufisadi, bado baadhi ya waliohojiwa wanaona Mwalimu Nyerere angekemea uovu huo.

“Angekemea viongozi kuendekeza rushwa. Rushwa imekithiri kwa baadhi ya viongozi,” alisema mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, John Mboko.

Watu kadhaa, wakiwemo watumishi wa umma, mashirika ya umma, wafanyabiashara na viongozi wa kampuni binafsi wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma tofauti kama uhujumu uchumi, rushwa na utakatishaji fedha tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingine madarakani.

Suala jingine lililotajwa na baadhi ya waliohojiwa ni watu kupotea, mashambulizi dhidi ya raia na watu wasiojulikana.

“Hivi Baba wa Taifa angevumiliaje watu kupigwa risasi hadharani?” alihoji Mecky Sanchez Filbert.

“Watu kuvunja katiba, watu kujiita miungu watu? Nawaza tu angewaita majina gani mabaya wanasiasa wa leo?”

Mkoani Arusha, William Laizer (75) mkazi wa Sanawari, alisema Nyerere angekemea watu kupotea bila sababu na kuwajaza hofu wananchi.

Kilio cha wanasiasa wa upinzani kuhusu demokrasia. pia kilitolewa na watoaji maoni ambao walisema Nyerere alipenda demokrasia.

“Asingekubali kuua demokrasia kwa kuwa madhara ni makubwa. Mojawapo ni jinsi wananchi walivyosusia (kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya) uchaguzi, alisema mkazi wa Msufini, Kenneth Tesha.

Naye Hamis Mkindi, ambaye alijitambulisha kuwa ni wakili, alisema Baba wa Taifa “aliamini katika kujenga demokrasia, hivyo kwa hali ya sasa ambayo inaonekana kuminywa siasa za ushindani Baba wa Taifa asingefurahi”.

Mwingine anayejiita Steven Modestus alisema Nyerere “angekemea siasa za matusi na angeshauri siasa za kujenga hoja zaidi. Angekemea jinsi vyama vya siasa vinavyotugawa kutoka kwenye umoja wetu”.

Suala la kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa lilitajwa na Godfrey Kweka aliyesema Mwalimu Nyerere asingependa kuzuia mikutano ya kisiasa, kitu ambacho alisema athari yake zinaonekana sasa kutokana na wananchi kutoona umuhimu wa uchaguzi.

Wachangiaji hao wa maoni pia walizungumzia mambo ambaye muasisi huyo wa Taifa angesifia kama angekuwepo leo.

Na suala la ujenzi wa miundombini ya usafiri kama reli ya kisasa (SGR), barabara, viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege yalikuwa ni baadhi ya mambo yaliyotajwa.

“Kwa kiasi chake sasa miundombinu ya nchi inatengenezwa,” alisema Gustaph Cassian.

“Hakupenda kabisa ufisadi, rushwa, unafiki, na kutokuwajibika kwa viongozi pale wanapokuwa wamekosea.”

Naye Judith Ferdinand alisema kama Mwalimu angekuwapo angeweza kufurahia kuona mambo mengi ambayo aliyaamini yameweza kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Kila mara akizungumzia ujenzi wa bwawa la kuzaalishia umeme Mto Rufiji katika bonde la Stigler, Rais Magufuli anasema ni moja ya hatua zake za kutimiza ndoto aliyokuwa nayo Baba wa Taifa ambayo haikuweza kutimia kutokana na njama za mabeberu.

Pia, Rais anasema kitendo cha kutekeleza uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma uliofanywa mwaka 1973 ni kutekeleza ndoto za muasisi huyo wa Tanzania.

“Mwalimu Nyerere angefurahishwa na jinsi Rais Magufuli anavyofanya baadhi ya mambo ambayo aliyasimamia katika uhai wake,” alisema mkazi wa Shinyanga, Monica Mhoja.