Nacte yatangaza dirisha la udahili kwa wanafunzi

Mkuu wa kitengo cha Udahili wa NACTE, Twaha Twaha,

Muktasari:

Dirisha la pili kwa ajili ya maombi kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na masomo ngazi ya Astashahada na Stashahada limefunguliwa Septemba 7 na linatarajiwa kufungwa Septemba 25,2019.

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) nchini Tanzania limetangaza kufungua dirisha la pili la udahili kwa waombaji wa ngazi ya astashahada na shahada ili kuwapa nafasi wale ambao hawakupata na kujaza nafasi wazi katika vyuo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Septemba 17,2019 na Mkuu wa Idara ya Usahili Nacte, Twaha Twaha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa dirisha hilo lilifunguliwa kuanzia Septemba 7 na litafungwa Septemba 25, 2019.

Amesema wahitimu wa kidato cha nne na sita walio na sifa za kujiunga na programu mbalimbali wanapaswa kutumia fursa hiyo kutuma maombi ya udahili kwenye taasisi na vyuo vyenye nafasi na ambavyo bado vinapokea maombi ya udahili.

“Mpaka sasa baraza linaendelea kuhakiki majina 58,193 ya waliochaguliwa na taasisi na vyuo mbalimbali vinavyotoa elimu ya ufundi na mafunzo ikiwa ni idadi pungufu ya wanafunzi 160,000 ambao wanapaswa kudahiliwa kupitia vyuo na Taasisi.”

“Japokuwa wanafunzi wengine 40,000 wamedahiliwa kupitia Tamisemi na tutaletewa majina yao ili tuyafanyie uhakiki kabla ya kuyatangaza Oktoba 4, 2019 ili waweze kuanza masomo Oktoba 15,2019 kama ilivyo kwenye kalenda ya baraza,” amesema

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (Tahliso) Peter Niboye amevitaka vyuo kudahili kwa kufuata kanuni na vigezo walivyoelekezwa na Nacte ikiwa ni pamoja na kufuata mitalaa ili kuzalishwa wataalamu walio bora.

“Tumekuwa tukishuhudia changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi hususan kuhamishwa vyuo baada ya Nacte kuvichukulia hatua, jambo hili si zuri na tunaomba wazingatie kanuni,” amesema Niboye na kuongeza

“Aidha kutokana na malalamiko kuwa mengi juu ya kuchelewa kwa upatikanaji wa Award verification Number (AVN) tunazielekeza serikali za wanafunzi kote nchini kuhakikisha taarifa za wanafunzi ikiwemo matokeo ili kuondoa malalamiko kwa wanafunzi wanapohitaji huduma.”