Nyuma ya ahadi ya Sh50 milioni kwa kila kijiji

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza na wahariri na waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) alipotembelea makao makuu ya kampuni hiyo, jijini Dar es Salaam juzi. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dar na Mikoani. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ameanika tatizo lililosababisha ahadi ya Sh50 milioni kwa kila kijiji kutotekelezeka, akisema lilianzia wakati wa kuandika ilani.

CCM ilijinadi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kuwa itatoa fedha hizo kwa kila kijiji ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi. Ahadi hiyo imo katika Ilani ya CCM ya 2015 - 2020.

“Kutenga kiasi cha Sh50 milioni kwa kila kijiji kama mfuko wa mzunguko (revolving fund) kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa (Saccos) katika vijiji,” kinasema kifungu cha 57 (d) cha ilani hiyo.

Kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli, makamu wake, Samia Suluhu Hassan, na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole walizungumzia ahadi hiyo wakisema wameamua kuelekeza fedha hizo katika miradi mingine ya kijamii ambayo kukamilika kwake kutakuwa kichocheo cha maendeleo.

Hata hivyo, bado kumekuwa na watu mbalimbali wanaokumbushia ahadi hiyo na hata wabunge mara kadhaa wamehoji utekelezaji wa ahadi hiyo huku wakihofu kwamba suala hilo linaweza kuwa kizingiti kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Lakini maswali yamekuwa yakiibuka huku wabunge wakihoji na wa upande wa upinzani wakitumia suala hilo kama silaha kuonyesha chama hicho kinashindwa kutekeleza ahadi zake.

Lakini Dk Bashiru juzi alieleza bayana chimbuko la matatizo ya utekelezaji wake na jinsi linavyosumbua kwa kuwa kila wanapotoa maelezo, halieleweki na maswali hayaishi.

Dk Bashiru alisema suala hilo lilianza kuibua mvutano miongoni mwa wajumbe wa kamati ya Ilani ya CCM ambayo yeye alikuwa katibu wake na kwamba hoja ilikuwa ni kuhusu utekelezaji wake na kwamba kwa kumbukumbu zake “halikuwa na mwafaka”.

“Kuna ahadi zinakaa katika ilani kwa sababu ya kimuktadha,” alisema msomi huyo aliyebobea katika sayansi ya siasa.

“Na zinaweza kutekelezwa wakati ule wa miaka mitano au zisitekelezwe. Na nitatoa mifano. Kuhamia Dodoma ilikuwa ni ahadi ya Tanu mwaka 1973. Na ilani zote za CCM zimetaja kazisome.

“Ilani (labda alitaka kusema ahadi) iliyoko 2015 ndiyo imetuwezesha kuhamia Dodoma.”

Alisema enzi hizo ilionekana kama ingetekelezeka kwa muda mfupi, haikuwezekana lakini ikaendelea kuwemo katika ilani ya CCM hadi ilipotekelezwa na Rais wa Tano.

Alisema ahadi ambayo haikuwa inatekelezeka na waliitoa katika ilani ni ya kubadili Kigamboni kuwa mji wa kisasa kama Dubai, akisema waliofikiri na watekelezaji walitofautiana.

“Hili la milioni 50, sitaki kusema mjadala ulivyokuwa kwa kuwa nilikuwa katika kamati ya ilani. Sitaki kutoa siri za vikao,” alisema Dk Bashiru.

“Lakini nachoweza kusema ni kwamba tulikuwa hatuna muafaka kuhusu utekelezaji wake; kama linatekelezeka au lina tija. Sasa hiyo itabaki katika rekodi. Lakini hatimaye likapita.

“Baada ya kupita katika utekelezaji ikaja hoja. Hivi hizi pesa zikipelekwa huku milioni hamsini hamsini, kwa vijiji vyote itakuwa shilingi ngapi? Na huku tumeshaahidi kuanza mara moja utekelezaji wa kupeleka watoto wote bila malipo tangu darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Je, kupanga ni kuchagua. Tucheleweshe hili kuanza ili tulipe hii.”

Katika bajeti ya 2016/17, Serikali ilitenga Sh59 bilioni na mwaka 2017/18 ikatenga Sh60 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo kwa kila kijiji, lakini fedha hizo hazikutolewa hali iliyoibua mvutano wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango 2018/19.

Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu alikuwa miongoni mwa wabunge waliotaka majibu ya Serikali kuhusu ahadi hiyo akisema itakuwa kazi kubwa katika uchaguzi mkuu.

Pia Juni 5, 2018, Bunge likiwa limekaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti ya wizara ya fedha ya 2018/19, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philp Mpango alisema ahadi hiyo ingeanza kutekelezwa mara baada ya mfumo wa kuanza kuzitoa kukamilika.

Waziri Mpango alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Karagwe (CCM), Innocent Bashungwa aliyehoji sababu za kutotolewa kwa fedha hizo zilizoahidiwa katika Ilani ya CCM.

“Haya mambo yanajadiliwa kwa ukali kuliko ninavyozungumza,” alisema Dk Bashiru juzi.

“Kupanga ni kuchagua, tukaanza na shule na ni jukumu la kwanza kutekelezwa na CCM na mpaka sasa linatekelezwa na hatuna mpango wa kuliacha katika ilani ijayo.”

Ili kufanikisha mpango wa elimu bure, Serikali imekuwa ikitoa takriban Sh28 bilioni kila mwezi.

Wasemacho wananchi

Wachambuzi walioongea na Mwananchi walisema kutotekelezwa kwa ilani kunatokana na ahadi kutokuwa halisia.

“Mara nyingi sera za CCM zinakwama kwa sababu ya kuahidi kitu, lakini havifikii mwisho kama vile kilimo kwanza, sera ya viwanda na hawana mtiririko rasmi,” alisema mchambuzi na mtaalamu wa masuala ya kijamii jijini Mwanza, Holela Mabula.

“Ndio maana ilipiganiwa Katiba mpya ili yale masuala ya kitaifa yawe na utaratibu wake. Lakini mpaka sasa nchi inaendeshwa kwa ilani, kila unayemuuliza anakwambia natekeleza ilani.”

Mkazi wa Mtaa wa Bunda Stoo wilayani Bunda, Sadiki Maregesi alisema uamuzi uliofanywa na Serikali kutotoa fedha hizo, hauna madhara kwa vile miradi iliyotekelezwa inaonekana.

Alisema endapo fedha hizo zingegawanywa kwa wananchi kusingekuwa na tofauti ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete zilizojulikana kama “Mabilioni ya JK”.

Mjini Geita, Ester Nduguru alisema wananchi walihamasika 2015 wakiamini kila kijiji kingepata mamilioni hayo, lakini kubadili uamuzi huo ni kuonyesha kushindwa.

Naye mkazi wa jijini Dodoma, Calvin Nassib alisema kama imeshindikana kuzifikisha fedha hizo katika kila kijiji, basi wapatiwe wajasiriamali kwa lengo la kuwasaidia kuongeza mitaji yao.