Nyuma ya pazia kurejea kwa Lissu

Monday September 9 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. “Subira imefika mwisho” ndio tafsiri sahihi ya “the wait is over” kwa wale ambao wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kurejea kwa Tundu Lissu, mwanasiasa ambaye amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017.

Kauli yake wiki hii kuwa hangerejea Septemba 7 kama alivyoahidi awali na kutengeneza shauku kwa mashabiki, wafuasi wake, wanasiasa, wadau na wachambuzi, imefanya subira kugeuka kuwa ubashiri wa nini kinachomzuia kurudi mapema nchini.

“Nilisema mwanzoni nitarudi Septemba 7 lakini mpaka sasa hivi sijapata ruhusa ya madaktari wangu. (Daktari) Ameniambia ataniona Oktoba Mosi, na mara ya mwisho Oktoba 8,” alisema Lissu , ambaye alikuwa mbunge wa Singida Mashariki.

“Ratiba ya tarehe 7 Septemba haitawezekana kwa sababu daktari wangu bado anahitaji kuniona hizo tarehe mbili. Baada ya hapo nitafanya taratibu za kurudi nyumbani.”

Siku hiyo ni muhimu katika maisha ya Lissu.

“Septemba 7 niliondoka Tanzania nikiwa nusu mfu. Kuna watu walitaka nife, hivyo nimeamua Septemba 7 iwe safari yangu ya kurudi Tanzania nikiwa mzima ili kudhihirishia hao waliotaka kuniua kuwa niko hai,” alisema Lissu katika moja ya mahojiano na Mwananchi siku za nyuma.

Advertisement

Na awali, mwenyekiti wake, Freeman Mbowe aliunga mkono kuhusu kurejea siku hiyo.

“Ni siku muhimu na maalumu kwa wapigania demokrasia na haki za binadamu,” alisema akiunga mkono Septemba 7 (jana) kuwa siku ya Lissu kurejea nchini.

Lakini kuahirisha kwa siku ya Lissu kurejea kunazidisha tashwishi ya suala hilo la mwanasiasa ambaye ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa masuala ya kisiasa na kiuchumi nchini.

Hali hiyo inatokana na video ambazo amekuwa akituma kila wakati au ambazo zinachukuliwa na watu wanaomtembelea, ikiwemo ya hivi karibuni iliyotumwa mtandaoni na kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe .

Video hizo zinamuonyesha akikata mitaa ya Brussels, Ubelgiji akichechemea, na hivyo kusababisha baadhi ya watu kuamini kuwa ameshapona na hivyo kuchelewa kwake ni kwa mkakati.

Suala hilo lilikuwa moja ya sababu zilizotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai siku ya mwisho ya Bunge la Bajeti, akisema kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kiko wazi kwa kuwa Lissu hajulikani alipo.

Lissu alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa kwenye gari, nje ya makazi yake mjini Dodoma baada ya kuwasili akitoka kuhudhuria shughuli za Bunge za asubuhi Septemba 7, 2017.

Alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Dodoma siku hiyo na usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, ambako alitibiwa kwa miezi kadhaa kabla ya kuhamishiwa Ubelgiji ambako anaendelea na matibabu.

Hata chama chake bado hakijawa na taarifa ya tarehe kamili ya kurejea kwake.

“Ni kweli Agosti 27 (Lissu) alisema angekutana na madaktari wake, na baada ya kumcheki wamemwongezea kwamba watakutana naye. Labda kuna vitu havijakaa sawa. Hatuna jinsi ya kulazimisha aje kesho (Septemba 7) wakati madaktari wanasema bado,” alisema mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema .

Lakini alipoulizwa kama kuna kitu chochote kinachosababisha asirudi sasa mbali na sababu za kitabibu, alisema: “Sisi kama chama tunasubiri ripoti ya madaktari. Maandalizi yalikuwa yanafanyika na sasa tunasubiri. Tunasikiliza sana madaktari kuliko matamanio yetu na ya wengine. Kwa hiyo muda ukifika atakuja.”

Kumekuwepo na ubashiri kuwa Chadema inamuandaa mwanasheria huyo kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 na hivyo inataka kurejea kwake kuwe kwa kishindo na ndio maana ikaahirisha tarehe ya awali ya Septemba 7 ambayo imekuwa ni siku ya kuadhimisha miaka miwili kamili tangu ashambuliwe.

Inabashiriwa kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kinataka kutengeneza shauku kwa wananchi kwa kuchelewesha ujio wake hadi wakati harakati za urais zitakapokaribia ili kuongeza ushawishi.

Chadema haijawahi kutoa nafasi kwa mwanachama mmoja kujaribu mara mbili kugombea urais. Mwaka 2015 ilimpa nafasi hiyo waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa lakini mwanasiasa huyo amesharejea CCM, hali inayotoa nafasi zaidi kwa Lissu kupewa fursa hiyo.

Mwaka 2010, chama hicho kiliwakilishwa na Dk Wilbrod Slaa, ambaye alijiondoa katika nafasi ya ukatibu mkuu baada ya chama hicho kumpokea Lowassa na kumpa fursa ya kugombea urais. Dk Slaa sasa ni balozi nchini Sweden.

Mwaka 2005, Chadema ilimsimamisha Mbowe kugombea urais na hajagombea tena tangu wakati huo na hatajwi.

Lissu amekuwa akiweka bayana msimamo wake kuhusu suala la kugombea urais kuwa hatakuwa na pingamizi iwapo Chadema itapitisha jina lake.

Alirudia tena kauli hiyo hivi karibuni alipohojiwa na BBC.

“Suala la kugombea urais mwakani halina uhusiano wowote na kesi iliyopo mahakamani. Hakuna chochote cha kunizuia kugombea ubunge wala urais mwaka ujao kama chama changu na vyama rafiki vitasema nafaa kuviwakilisha katika urais,” alisema.

Lissu pia amekuwa na kesi kadhaa mahakamani, baadhi zikiwa za uchochezi na ambazo zimekuwa haziwezi kuendelea kutokana na kuwa nje kwa matibabu.

Lissu amekuwa mmoja wa wanachama wanaoiweka hai Chadema kutokana na kuwa mstari wa mbele kuzungumzia matatizo kadhaa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanapotokea, akitumia nafasi yake ya mwanasheria mkuu wa Chadema, ubunge na mnadhimu mkuu wa upinzani.

“Tangu ashambuliwe, pengo la Lissu limekuwa linaonekana ndani ya chama. Lissu ni mwanasheria mkuu wetu, mnadhimu mkuu wa wabunge, pamoja na wanasheria waliobaki wakiongozwa na mkurugenzi wa sheria Peter Kibatala. Lakini Lissu ni Lissu na Kibatala ni Kibatala,” alisema Mrema.

“Tunatarajia akirejea pengo lake litazibika lakini kwa sasa tumuache kwanza amalizie matibabu yake kwani amekutana na mambo mengi.”

Advertisement