Polisi hawajui vurugu mkutano wa Mbowe

Moshi. Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni amesema hajapokea taarifa kuhusiana na mkutano wa hadhara wa mbunge wa Jimbo la Hai (Chadema), Freeman Mbowe kufanyiwa vurugu.

Akizungumza jana na Mwananchi, Kamanda Hamduni alisema hakuna malalamiko yoyote yaliyowasilishwa kituo cha polisi na watu wa Chadema kuhusiana na mkutano wao kufanyiwa vurugu.

“Sijapata taarifa zozote za vurugu, zaidi ya kelele zilizokuwepo wakipinga kile kinachozungumzwa, lakini hapakuwa na vurugu yoyote,”alisema Kamanda Hamduni na kuongeza kuwa;

“Hakuna malalamiko yaliyowasilishwa kituo cha polisi na watu wa Chadema, labda pengine ilikuwa ni shamra kwenye mkutano ambazo hazikuangukia kwenye jinai kwa sababu kungekuwa na mtu amekerwa angeripoti kituo cha polisi.”

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila alipoulizwa kama wametoa taarifa polisi, alisema baada ya mkutano kuvunjika kila mmoja alikuwa na hasira, hivyo hawakutoa taarifa kwa usiku ule na kwamba wanajipanga kuiwasilisha leo kituo cha polisi.

“Tunaandaa maelezo kwa ajili kuwasilisha malalamiko polisi kwa kuwa jana (juzi) tulipomaliza mkutano kila mtu alikuwa na hasira na hatukuwa na namna ya kufanya, hivyo hatukwenda polisi kupeleka malalamiko yetu,”alisema Kilawila.

Juzi, Mbowe akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kikafu, kata ya Weruweru, muda mfupi kabla ya kumalizika kiliibuka kikundi cha watu kilichoanza kupiga kelele na kuzomea.

Baada ya kelele kutulia na watu hao kuondoka, Mbowe alishuka jukwaani na kuzungumza na waandishi wa habari akisema walipata taarifa mapema kuwa kuna mpango ulioratibiwa na baadhi ya viongozi wa CCM na mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya kuhusu kuvuruga mkutano wake na waliliripoti hilo polisi.

“Tuliripoti tukio hili polisi, tulitegemea wangechukua hatua, lakini tulishangaa genge la vijana lilivyojitokeza mbele ya kamanda wa Polisi wa Wilaya alionekana kuwalinda na hawakummata hata mmoja, wakavuruga mkutano kwa zaidi ya dakika 15, ” alisema Mbowe.