Profesa Kabudi azitaja Uingereza na Marekani vikwazo dhidi ya Zimbabwe

Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema nchi hiyo itatumia uenyekiti wake wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) kushinikiza Uingereza na Marekani zinaiondolea vikwazo Zimbabwe.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema nchi hiyo itatumia uenyekiti wake wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) kushinikiza Uingereza na Marekani zinaiondolea vikwazo Zimbabwe.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 25, 2019  katika kongamano maalum  la vikwazo na hatima ya Afrika, Profesa Kabudi ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa SADC amesema vikwazo hivyo vinakwenda kinyume na mkataba wa Umoja wa Afrika.

“Tanzania ndiyo mwenyekiti wa SADC katika uenyekiti wetu tumejiwekea maazimio na moja ni hili la Zimbabwe. Sisi ndio tuliowahakikishia. Tumeifanya kuwa ajenda baada ya kupata uenyekiti.”

“Wenzetu walianza miaka iliyopita na sisi tunaendelea mpaka vikwazo viondolewe. Tukimaliza muda wetu atakayekuja naye ataendelea,” amesema.

Amesema Zimbabwe kuwekewa vikwazo ni kwenda kinyume na mkataba wa umoja wa mataifa unaotaka nchi kupeleka hoja zake kwenye baraza la umoja wa mataifa.

“Kama kweli Uingereza na Marekani wangekuwa na hoja za msingi kuhusu Zimbabwe basi wangepeleka kwenye baraza la umoja wa mataifa, wapime waone kama wanaweza kuchukua hatua hiyo,” amesema.

Amesema kiini cha vikwazo hivyo ni Wazimbabwe kuchukua ardhi yao ambayo  katika mkutano wa Lancaster (Uingereza) mwaka 1979 hoja hiyo ndiyo ilichelewesha kutolewa kwa uhuru.

“Mwalimu (Julius Nyerere) aliyewatuma Warioba (Jaji Joseph) na Dk Salim (Ahmed Salim) kwenye mikutano ya Lancaster, akiwaambia kuwa kubalini kwanza hiyo mpite,” amesema Profesa Kabudi.