Profesa Ndalichato atoa maagizo kwa katibu mkuu wizara ya elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya elimu katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Muktasari:

Waziri Ndalichako amekagua miradi ya elimu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma katika shule ya msingi Bwega, shule ya sekondari Janda,  shule ya sekondari Muyama, shule ya msingi Kasumo na shule ya sekondari Mwibuye wilayani Kasulu na kubaini kasoro mbalimbali .

Buhigwe. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa  Joyce Ndalichako  amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo kwenda wilayani Buhigwe mkoani Kigoma kufanya ukaguzi maalumu wa miradi ya elimu kama utekelezaji wake ulifuata utaratibu.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya waziri huyo kufanya ziara katika wilaya hiyo katika miradi mbalimbali ya elimu inayotekelezwa na fedha za mpango wa lipa kwa matokeo (EP4R), miradi yenye thamani ya fedha zaidi ya Sh1 bilioni.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 15, 2019, Waziri Ndalichako amesema katika baada ya kukagua miradi hiyo aliweza kubaini kasoro mbalimbali za ujenzi wa majengo ya elimu yanayoendelea kujengwa katika wilaya hiyo.

"Nimeweza kubaini kasoro mbalimbali katika miradi ya elimu ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya kiwango pamoja na kutumia ramani ya michoro yao binafsi na kuacha ya wizara katika majengo ya utawala," amesema Waziri Ndalichako.

Amesema pia ameweza kubaini usimamizi wa miradi kwa ujumla katika wilaya hiyo sio mzuri na kwamba maofisa elimu wameshindwa kuwajibika katika kuangalia kazi zao kutokana na makosa mengi yaliyojitokeza ni ya kukosa uangalizi na si swala la fedha kukosekana. 

 

 

 

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina amesema kabla ya kuja waziri aliweza kubaini baadhi ya upungufu wa kuyatolea maelekezo kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Anosta Nyamoga na kuzichukulia hatua.

"Kamati ya usalama ya wilaya iliweza  kubaini upungufu katika miradi mbalimbali na tulitoa maelekezo kupitia kwa  mkurugenzi na vyombo vyetu vilishaagizwa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki," amesema mkuu wa wilaya

Mhandisi wa halmashauri ya Buhigwe ambaye anashughulikia miradi hiyo Aidan Iddi amesema ramani ambayo anaitumia ndio waliyokubaliana katika vikao vyao na kwamba hakuna ramani iliwahi kuletwa kwake.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo amekiri kuwepo kwa upungufu katika ujenzi wa majengo hayo ya elimu na kusema kuwa tayari ameshaanza kuchukua hatua kwa waliohusika katika ujenzi huo .