Rais Magufuli atoa salamu za mwaka mpya, amuonya DED Chato

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli jana Jumanne alitembelea maofisa na askari wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita ambako akiwa huko alitoa salamu za mwaka mpya 2020.


Chato. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya mwaka mpya wa 2020 na kuwaomba waendelee kudumisha amani na upendo ili uwe mwaka wa maendeleo na ustawi kwa Taifa.

Rais Magufuli ametoa salamu hizo jana Jumanne Desemba 31, 2019 wakati akiagana na maofisa na askari wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita.

Akiwa kisiwani huko pamoja na mkewe, Janeth Rais Magufuli alitembelea na kujionea vivutio vya utalii pamoja na wananchi wa Nyabugera na Muganza aliowasalimu wakati akiwa njiani kurejea nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amepokea salamu za heri ya mwaka mpya wa 2020 kutoka kwa wananchi, viongozi mbalimbali wakiwamo marais wastaafu, maaskofu na masheikh ambao wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuongoza nchi kwa mafanikio makubwa na wamemuelezea matarajio yao ya kufanikiwa zaidi katika mwaka ujao.

“Mhe. Rais wangu, Magufuli, Bwana Yesu Asifiwe. Ninakupa hongera sana kwa wajibu mzito ulionao. Kwa neema ya Mungu tumejaaliwa kufikia siku ya mwisho kwa mwaka huu wa 2019.”

“Mimi nakupongeza kwa jitihada zako nyingi za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Ninakuombea na kukutakia mwaka mpya 2020 wa heri na mafanikio makubwa. Uso wa Bwana uende nawe popote utakapokuwa,” amesema Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo.

Akiwa kisiwani huko, Rais Magufuli alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, kufuatilia ukusanyaji wa mapato katika soko hili na kuchukua hatua za kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato itakayobainika ili Halmashauri ya Wilaya ya Chato iweze kupata fedha zitakazosaidia kutatua kero za wananchi ikiwamo kuboresha mazingira ya soko hilo na ujenzi wa shule ya sekondari ya Nyabugera ambayo amechangia Sh5 milioni.

Pia, Rais Magufuli alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato (DED), Eliud Mwaiteleke kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Kasenda - Muganza yenye urefu wa kilometa 2.2 ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi na kwamba Serikali itatoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo.

Rais Magufuli pia amewasalimu wananchi wa Muganza, ambapo amewapongeza kwa maendeleo yaliyopatikana katika eneo hilo na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma ili iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.

“Nchi hii ilikuwa inaliwa sana na majizi na mpaka sasa bado wapo, namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kunipa uhai ili katika mwaka 2020 niendelee kuwatumbua majizi wote na fedha tutakazopata tuzipeleke kwenye miradi ya maendeleo kama ambavyo tumenunua ndege 11, tunajenga reli (standard gauge), tunatoa elimu bure na mengine mengi,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia alimuonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Eliud Mwaiteleke kwa matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na halmashauri hiyo na ametaka dosari hizo zirekebishwe mara moja.

“Nataka ujirekebishe, wananchi hawa wanateseka sana,” alisisitiza Rais Magufuli.