Ras Jeshi asema wajasiriamali wanataka faida kubwa

Sunday September 22 2019

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam. Malighafi kuwa juu na wajasiriamali kutaka faida kubwa ni miongoni mwa sababu za bidhaa za asili kukosa soko.

Hayo yameelezwa na mjasirimali Ras Jeshi Beku wakati wa maonyesho ya bidhaa za utamaduni zinazoonyeshwa katika Tamasha la utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest) Dar es Salaam nchini Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Septemba 22,2019 Ras Beku amesema soko la bidhaa zao linaonekana kuwa gumu kutokana na wafanyabiashara wengi kutaka kupata faida kubwa.

“Wengi wanalalamika wanatengeneza vitu vizuri lakini havipati soko, tatizo wanataka faida kubwa ila wakiuza kawaida soko lipo,” amesema

Amesema changamoto iliyopo ni malighafi kupatikana kwa gharama kubwa kwa kuwa nyingi zinatoka nje ya nchi.

Ras Beku ameeleza ili kukabiliana na hilo ni muhimu kukawa na viwanda vya kuzalisha malighafi Tanzania kuepusha gharama ya kutoa nje ya nchi.

Advertisement

Kuhusu maonyesho hayo yaliyoanza jana Jumamosi na kuhitimishwa Septemba 28, 2019 amesema yanawapa fursa wajasiriamali kuuza bidhaa zao kwa watu wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Rahabu Mbukwa ambaye ni mjasiriamali kutoka Kenya amesema tamasha hilo ni chachu ya kutangaza biashara zao na kujifunza tamaduni za nchi nyingine.

Advertisement