Saa 20 za patashika uchaguzi wa Chadema

Muktasari:

Freeman Mbowe alifanikiwa kutetea kiti cha uenyekiti wa Chadema ambacho amekuwa anashikilia tangu 2004.

Dar es Salaam. Saa 20 za uchaguzi wa Chadema wa kuchagua mwenyekiti na makamu wenyeviti wa bara na visiwani hazikuwa rahisi kutokana na mchakato huo kuchukua muda mrefu kuanzia juzi asubuhi hadi jana alfajiri.

Shughuli za uchaguzi zilianza juzi saa tatu asubuhi kwa wajumbe wa mkutano huo kuanza kukaguliwa ili kuingia katika ukumbi wa Mlimani City.

Baada ya wajumbe hao kuingia ndani ya ukumbi huo waliketi kwenye viti kwa mfumo wa kikanda kwa mujibu wa taratibu za Chadema, kisha wakaingia viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa.

Katika mkutano wa uchaguzi pia walialikwa mabalozi wa nchi za nje, wabunge kutoka nje ya nchi na viongozi wa dini kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo ambalo hutokea mara moja baada ya miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya Chadema.

Wakati hayo yakiendelea nje ya ukumbi huo, bendera zenye nembo ya Chadema zilikuwa zikipepea huku ulinzi ukiimarishwa kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa amani na utulivu.

Mabango yenye picha ya Mbowe ambaye ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti yaliwekwa ndani na nje ya ukumbi huo yakibeba ujumbe wa `mwamba tuvushe’, huku wajumbe wengine wakidiriki kupiga picha kisha kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Mbali na hilo, ndani ya jengo na nje ya ukumbi zilitapakaa kadi maalum ndogo zilizokuwa na picha ya mwenyekiti huyo zikiwa zimeandikwa ujumbe wa `mwamba tuvushe’.

Wakati wakisubiri viongozi wakuu wa Chadema kuingia burudani za nyimbo za hapa na pale zikisindikiwa na vikundi vya ngoma na hamasa vya chama hicho vilikuwa vikitumbuiza kwa ustadi wa aina yake na kuwainua wajumbe na waalikwa wa mkutano huo.

Ukiachana na vikundi, msanii wa miondoko ya Hip Pop na mbunge wa Mikumi, Joseph Haule aliwainua kwa mara nyingine watu waliokuwemo katika ukumbi kwa vibao vyake vya `ndio mzee’ na `hapo vipi’.

Vibao hivyo vilionekana kukonga nyoyo za washiriki wa mkutano waliosimama na kumpigia makofi msanii huyo mkongwe ambaye alianza kuimba wimbo wa `ndio mzee’.

Baada ya hapo burudani hizo, ulianza utambulisho wa wageni mbalimbali waalikwa, kisha kupewa nafasi ya kutoa neno kwa wajumbe wa mkutano akiwamo Mwenyekiti wa UPDP, Fahmy Dovutwa na Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya.

Lakini hali ilikuwa tofauti kwa mwenyekiti wa Ada Tadea, John Shibuda na Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza ambao walipata wakati mgumu wakati wakitoa salamu zao.

Minong’ono ya wajumbe na kelele vilimlazimu Mbowe kuwatuliza wajumbe hao akiwataka kuwa na nidhamu kwa wageni waalikwa.

Naye Mbowe aliwaeleza wajumbe na wageni waalikwa siri ya chama sera ya `Chadema msingi’ na namna chama hicho kitakavyopata mapato yake kupitia mkakati wa kidijitali utakaowezesha kukusanya ada ya wanachama wake itakayofikia Sh15 bilioni kwa mwaka.

Hotuba ya Lissu aliyoitoa kwa njia ya mtandao akitokea Ubelgiji nayo ilisisimua na kuwatoa machozi baadhi ya wajumbe.

Shughuli za ufunguzi wa mikutano, salamu kwa wageni na uzinduzi wa sera mbadala zilimalizika saa 12 jioni juzi ndipo wageni na wajumbe hao wakapewa muda wa mapumziko kabla ya kurejea tena katika ukumbi huo saa 2:30 usiku.

Baada ya upigaji kura kumalizika, wajumbe walipumzika tena saa nane usiku jana wakati mchakato wa kuhesabu kura ulipoanza na kuhitimishwa saa 11 alfajiri.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Sylvester Masinde alimtangaza Mbowe kama mwenyekiti baada ya kupata kura 886 sawa na asilimia 93.5 dhidi ya kura 59 sawa na asilimia 6.2 za Cecil Mwambe.

Masinde, alisema nafasi ya umakamu uenyekiti wa bara ilinyakuliwa na Lissu aliyemshinda mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda.

Lissu alizoa kura 930 sawa na asilimia 98.8 dhidi ya 11 sawa asilimia 1.2 za Mwakagenda.

Said Issa Mohamed alitetea nafasi yake kama makamu mwenyekiti kutoka Zanzibar.