VIDEO: Saa 24 za Mbowe, Mwambe

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Chadema linakutana jijini hapa ajenda kuu ikiwa ni kuwajadili na kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Katika nafasi ya mwenyekiti, Freeman Mbowe na Cecil Mwambe watajadiliwa na ama kupitishwa au kukatwa kuwania nafasi hiyo kubwa ya chama katika uchaguzi utakaofanyika kesho.

Baraza Kuu ambalo linaundwa na wajumbe 600, pia litawajadili aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu na mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti.

Upande wa Zanzibar aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo ni Said Issa Mohammed ambaye anaitetea.

Akizungumza na wanahabari jana, mkurugenzi wa Chadema wa masuala ya itifaki, uenezi na mambo ya nje, John Mrema alisema kamati kuu imeyapitisha majina hayo na kazi iliyobaki ni kwa baraza kuu kuyapitia na kuyapeleka kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyika kesho.

Mkutano mkuu unatarajiwa kuwa na wajumbe takribani 1,300.

Mrema alisema mtu mwingine aliyekuwa anawania uenyekiti, Frederick Sumaye aliandika barua ya kujitoa uanachama waliyoipata jana hivyo kupoteza sifa ya kugombea huku Said Kubenea aliyekuwa anawania umakamu mwenyekiti akiandika barua ya kujitoa kuwania nafasi hiyo.

Mrema alisema barua ya Kubenea ya kujitoa iliyosomwa katika kikao cha kamati kuu ikieleza kuwa anajitoa katika mchakato huo na kumuachia Lissu ambaye anaona anaweza kufanya kazi ambazo angefanya yeye.

“Nafasi ya umakamu uenyekiti wa Zanzibar aliyejitokeza ni Said Issa Mohammed anayetetea nafasi hiyo kwa mara nyingine na yeye atajadiliwa katika katika kikao cha baraza kuu kitakachofanyika kesho (leo),” alisema Mrema.

Mrema alifafanua kuwa katika mchakato wa kufanya usaili wagombea kadhaa baadhi yao akiwamo Lissu, Mohammed na Mwakagenda hawakuwepo, lakini walitumia wasifu wao waliojaza kwenye fomu kupitisha majina yao kwenda baraza kuu.

Mbali na hilo, Mrema alisema kamati hiyo ilipitisha majina ya Gibson Meiseyeki (mbunge wa Arumeru Magharibi), Patrick Ole Sosopi, Samson Mwambene, Mechard Tiba na Ahobokile Mwaitenda walioomba nafasi ya ujumbe wa kamati kuu upande wa wanaume.

Kwa wanawake waliopitishwa ni Suzan Kiwanga (mbunge wa Mlimba), Catherine Vermand, Grace Kihwelu (mbunge viti maalumu), Pamela Massay (mbunge Afrika Mashariki), Ester Daffi, Sara Katanga na Betty Massanja.

“Upande wa kundi la wanawake watakaochaguliwa ni watatu hivyo hivyo kwa wanaume. Idadi ya wajumbe wanaotakiwa kwa mujibu wa katiba ni wanane, sita kutoka Bara na wawili kutoka Zanzibar,” alisema Mrema.

“Wajumbe wa kamati kuu wanaume kwa upande wa Zanzibar waliopitishwa ni Hemed Ali Hemed na Yahya Alawi Omary. Upande wa wanawake ni Sharifa Suleiman Suleiman, Zeud Mvano Abdillah na Zainab Mussa Bakary.

Majina hayo yatapelekwa kwenye baraza kuu la chama hicho litakaloketi keshokutwa kuteua wajumbe wanane wa kamati kuu ya chama hicho.