Sababu tano zilizomfanya Mkapa kuwania urais

Rais mstaafu Benjamin Mkapa

Dar es Salaam. Rais mstaafu Benjamin Mkapa amezungumzia mengi kuhusu utawala wake wa miaka 10 katika kitabu chake alichozindua hivi karibuni, lakini pia ameanika sababu tano zilizomsukuma kuwania urais.

Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)”, Mkapa ameweka bayana kuwa wazo la kuwania urais lilimjia baada ya baadhi ya rafiki zake kumshawishi.

Hata hivyo, anaeleza kabla ya hapo alikuwa anatafakari kuachana kabisa na siasa mwishoni mwa mwaka 1994.

Anaeleza alifikia uamuzi huo wa kutaka kuachana na siasa kutokana na kuchoka baada ya kuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu. Anasema pia alikuwa hafurahishwi na mwenendo wa hali ya mambo nchini.

Mkapa anasema alikuwa anasononeshwa na jinsi Serikali na CCM zilivyoshindwa kushughulikia matatizo ya nchi.

“Kulikuwa na malalamiko mengi, watumishi wakilalamika kuchelewa kulipwa mishahara, makusanyo madogo ya Serikali na nchi wafadhili zilisusa kutoa misaada na mikopo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uendeshaji wa nchi,” anasema Mkapa.

“Nilichukua uamuzi wa kuwania urais baada ya kulitafakari suala hilo kutokana na matatizo yaliyokuwepo nchini na pia katika kipindi hicho kuna rafiki zangu mara kwa mara walinitaka niwanie nafasi hiyo wakiamini nina uwezo wa kurekebisha mambo.”

Mkapa anasimulia alipozungumza na mkewe alimjibu: “Kweli una uhakika, hivi kweli utakuwa unanitendea haki kweli?”

Anasema baadaye mkewe alikubaliana naye na kumuunga mkono na hatua ya pili ilikuwa kumtaarifu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Sababu tano za kuwania urais

Mkapa anasema alianza kutafuta njia ya kumueleza Mwalimu Nyerere kuhusu uamuzi wake kwa kuwa kipindi hicho alikuwa kijijini kwake Butiama mkoani Mara.

Kutokana na hali hiyo, aliamua kuandika barua ya kumtaarifu ambayo alimkabidhi Jaji Joseph Warioba, ambaye anatokea Bunda akiamini ni karibu na Butiama na alimfikishia Mwalimu Nyerere bila ya kujua kilichoandikwa ndani.

Mkapa anaeleza sababu yake ya kwanza ilitokana na kuyumba kwa vyama vya ushirika. Anasema wakulima walitoa mchango mkubwa wa kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika kupitia vyama vya ushirika. Lakini anasema katika kipindi hicho vyama vilitekwa na viongozi, ambao aliwatuhumu kujinufaisha na jasho la wakulima.

“Nilisikitishwa kuona wakulima wakikosa sauti katika uendeshaji vyama vya ushirika,” anasema huku akitoa mfano wa viongozi walioendeleza vyama hivyo miaka ya nyuma kama Paul Bomani (Nyanza), George Kahama (Bukoba) na Nsilo Swai (Kilimanjaro).

Jambo jingine lililomsukuma kugombea urais ni malalamiko ya wafanyakazi.

Anasema hali ilikuwa mbaya katika kipindi hicho kwa kuwa hakukuwepo maelewano mazuri kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi.

Malalamiko hasa yalikuwa kwenye sekta ya umma, ambako wafanyakazi walikuwa wanalalamikia mishahara midogo na kibaya zaidi ilikuwa inachelewa.

Mkapa anadai alihuzunishwa na matatizo ya wafanyakazi ambao wana mchango mkubwa katika ustawi wa nchi.

“Pia nilikuwa na kumbukumbu nzuri wakati wafanyakazi wakiwa chini ya Rashid Kawawa walivyoshiriki katika harakati za kupigania uhuru,” anasema Mkapa.

Anafichua sababu nyingine iliyomfanya kuwania urais kuwa ni kuvurugika kwa uhusiano kati ya Tanzania na nchi wahisani.

Ufisadi na rushwa vinaelezwa kuwa ndio sababu zilizosababisha wafadhili kupunguza misaada.

“Wafadhili walikuwa tayari kugharamia miradi iliyokuwapo huku wakigomea kutoa pesa kwa miradi mipya,” anasema.

Hoja ya nne ya Mkapa nitofauti kati ya Tanzania na taasisi za fedha za kimataifa, yaani Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

Uhusiano wa Tanzania na taasisi hizo nao ulikuwa umedorora na kusababisha nchi kukosa mikopo ya riba nafuu.

“Kurudisha uhusiano na taasisi hizi za fedha ni jambo ambalo lilikuwa muhimu ukizingatia taifa letu bado ni changa,” anasema.

Mkapa anasema kuwa aliamua kugombea.

“Kwenye kinyang’anyiro hicho sikutaka kuja kujuta baadaye kwa nini sikuwania nafasi hiyo ya urais,” anaongeza Mkapa, ambaye alipitishwa na CCM na kushinda uchaguzi uliomfanya kuwa rais wa tatu wa Tanzania.