Sakata la Meya Dar laacha maswali lukuki

Diwani wa Kata ya Tabata (chadema), Patrick Asenga akiondolewa na askari wa jiji na Polisi wakati wa kikao maalumu cha kujadili tuhuma za  Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita kilichofanyika jana. Picha na Said Khamis

Kukalia kiti cha Umeya wa Jiji la Dar es Salaam kwa diwani kutoka chama cha upinzani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 haikuwa kazi rahisi. Vikwazo vingi viliibuka kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo Machi 2016.

Uchaguzi uliahirishwa mara kadhaa kutokana na mvutano uliokuwa unaibuka kati ya wajumbe wa CCM na wa wapinzani na wakati mwingine kuzua vurugu.

Mvutano huo ulitokana na vyama vya upinzani kuwa na wajumbe 87 na CCM 76, hivyo kuwapo uwezekano wa kutwaa halmashauri ya jiji.

Ulipofanyika uchaguzi baada ya vitimbwi vya takriban miezi mitatu, Isaya Mwita, Diwani wa Vijibweni kwa tiketi ya Chadema alishinda nafasi hiyo.

Uchaguzi huo uliweka historia, kwani ilikuwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, chama cha upinzani kushinda nafasi ya kuongoza jiji hilo.

Sasa Meya huyo anakamiwa kuondolewa katika wadhifa huo kwa mbinde. Ingawa utaratibu uliotumika kumwondoa unaelezwa hakuwa sahihi, Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana ameshamwandikia barua akimtaka kukabidhi ofisi hiyo ndani ya siku 10 kuanzia Januari 10.

Pamoja na kwamba siku hizo bado hazijakwisha, Mwita ameshanyang’anywa gari na jana alipokwenda ofisini alikuta zimefungwa. Je nini kipo nyuma ya pazia la sakata la kumng’oa katika wadhifa wake?

Sakata hilo linaacha maswali lukuki na yasiyo na majibu miongoni mwa wafuatiliaji wa suala hilo lililoanza wiki iliyopita.

Swali tata

Utaratibu uliotumika kumng’oa ulikuwa sahihi? Je, bado ni Meya halali wa Jiji la Dar es Salaam?

Nani aliandika jina na kusaini kwa diwani asiyekuwapo kwenye kikao? Kwa nini aliyesaini hajachukuliwa hatua yoyote?

Tuhuma zinazomkabili meya zina mantiki? Wakati gari linapata ajali meya ndiye alikuwa dereva? Kwa nini meya alinyang’anywa gari kabla ya kupewa barua ya kung’olewa?

Nani anafunga ofisi ya meya kabla ya muda wa kukabidhi ofisi kuisha?

Sakata lilivyoanza

Zilianza kusikika tetesi katika mitandao ya kijamii hususan Twitter kwamba kuna mpango wa kumng’oa Meya Mwita.

Baada ya kusikika kwa tetesi hizo, kukawepo mchakato wa mkutano maalumu uliokuwa na ajenda ya kutoa azimio la kutokuwa na imani na meya huyo, hatimaye uliandaliwa, ukija na tuhuma nne.

Miongoni mwa tuhuma hizo ni kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

Tuhuma nyingine ni kutumia vibaya gari la ofisi ambalo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubungo Boniface Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.

Mchakato huo ulianzishwa mwaka jana na wajumbe wa baraza wa CCM waliopitisha fomu iliyosainiwa na madiwani 17 mmoja akiwa mpinzani na kutimiza takwa la kanuni za halmashauri ya kuwa theluthi 2/3 ya wajumbe ili kuunga mkono mchakato huo.

Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, walipeleka kwa mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana aliyewasilisha kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa iliyounda kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma hizo dhidi ya Mwita.

Alipoitwa baada ya baadhi ya wajumbe wa baraza hilo kuhojiwa, Mwita alidai hahusiki na tuhuma hizo akidai ni njama za kutaka kumwondoa katika nafasi hiyo.

Kabla ya kuitishwa mkutano mkuu Januari 9 uliokuwa na ajenda ya kupokea taarifa na kutoa uamuzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Mwita, alikimbilia mahakamani kuweka zuio la kutojadiliwa katika kikao chochote kitakachoitishwa na halmashauri ya jiji la Dar es Salaam.

Kabla ya mahakama kutoa uamuzi, mkutano huo ulifanyika na wajumbe 16 waliafiki taarifa hiyo na hawana imani na Mwita huku wajumbe wawili Chadema wakigoma kupiga kura. Hata hivyo, kura hizo hazikutimia theluthi mbili ya wapiga kura ambazo zingeweza kumg’oa Mwita baada ya kukosekana kura moja.

Baraza la madiwani wa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, lina wajumbe 26, kati yao CCM 16, Chadema saba na CUF watatu.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halmashauri ya jiji kifungu cha 84 (1) kinaeleza ili uamuzi uweze kufanyika wa kumwondoa meya madarakani kutokana na tuhuma kadhaa, itapaswa kuwapo kwa theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri. Theluthi mbili ya wajumbe 26 ni 17.

Hata hivyo, Liana alisisitiza wajumbe 16 waliopiga kura hiyo walifikisha theluthi mbili, akibainisha kuwa kanuni ya kumuondoa meya ilikuwa inaelekeza theluthi mbili ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho.

Baada ya mkutano huo, Meya Mwita alinyang’anywa gari alilokuwa akitumia na ameandikiwa barua ikimtaka akabidhi ofisi hiyo

Mkutano ulivyokuwa

Meya wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob aliomba kupewa daftari la mahudhurio na kubaini kuwepo na mjumbe aliyesainiwa katika kitabu cha mahudhurio anaitwa Kassim Mshamu (CUF).

Hatua hiyo ilimfanya diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Assenga kumtaka Mwita aliyekuwa meza kuu kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa yeye ndiye anayeendesha kikao hicho.

Hatua hiyo iiibua majibizano kati ya Mwita na mkurugenzi huyo, hatua iliyomlazimu Liana kuagiza polisi waliokuwa nje kuingia ndani haraka kutuliza vurugu. Baadaye Liana aliagiza jina la Mshamu kuondolewa katika daftari hilo. Baadaye Mshamu alipozungumza na Mwananchi alieleza hakuwapo kwenye kikao na hajasaini na alikuwa nje ya Dar es Salaam.

Wachambuzi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Idara ya Sayansi ya Jamii Dk Richard Mbunda anasema ni vema kuwepo na utaratibu wa kutumia fursa ya kisheria kwenda mahakamani ili kuondoa sintofahamu kama hiyo. “Tuwe na utaratibu wa kwenda mahakamani, kama ameondolewa kinyume cha utaratibu mahakama ina nafasi kubwa ya kutoa order (amri) ya kurudishwa katika nafasi yake. Aende mahakamani tu,” anasema Dk Mbunda.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke anasema kutokana na sakata hilo Meya Mwita ana nafasi ya kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana, Selemani Jafo kuonyesha hakuridhika na mwenendo mzima wa azimio la kutokuwa na imani naye.

Mhadhiri mwingine wa Udsm, Faraja Kristomus anasema wanaoweza kuondoa sintofahamu iliyopo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo.

“Makonda anatakiwa aeleze mwenendo kwa mchakato mzima wa azimio la kumuonda Mwita na Jafo anatakiwa amwelekeze mkurugenzi au mkuu wa mkoa kuanzisha upya mchakato huo,” anasema.

Pamoja na hayo, anasema kinachoendelea anaona siasa za kujiandaa na uchaguzi wa mwaka huu zimeanza kwa kutaka kuonyesha wananchi kuwa Chadema haina uhalali wa kuongoza Dar es Salaam.