VIDEO: Serikali yanunua mtambo mpya kuchapisha vitambulisho vya Taifa

Dodoma. Serikali imewaahidi Watanzania kuanza kuzalisha vitambulisho vya Taifa mwishoni mwa mwezi huu kwa kutumia mtambo mpya ambao una kasi ya kuzalisha vitambulisho 9,000 kwa saa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alisema kuwa uzalishaji wa vitambulisho hivyo utaanza mara baada ya mtambo huo kumalizika kufungwa mwishoni mwa mwezi huu.

Simbachawene alisema mtambo huo mpya umenunuliwa kwa zaidi ya Sh8 bilioni, fedha zilizotolewa na Rais John Magufuli ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa vitambulisho ili ndani ya miaka miwili Watanzania wote wanaostahili kuvipata wawe navyo.

Matarajio ya awali ilikuwa hadi kufikia mwaka 2021 Watanzania zaidi ya milioni 27.7 wanaostahili kupata vitambulisho wawe wamepata, lakini kutokana na uzalishaji wake kusuasua, lengo hilo halikufikiwa.

“Kuna mtambo mpya ambao mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi huu utakuwa umekamilika kufungwa na hapo tutaanza kuzalisha vitambulisho 9,000 kwa saa,” alisema.

Waziri Simbachawene alisema “kuna changamoto katika mtambo ambao unatumika sasa na baadhi ya mashine hazifanyi kazi, hii imesababisha uzalishaji wa vitambulisho kutokuwa wa kuridhisha, kwa saa unazalisha vitambulisho chini ya 500,” alisema Simbachawene.

Alisema kuharibika kwa mtambo huo kumesababishwa na uzembe wa baadhi ya watu kutousimamia vizuri hadi kufikia hatua hiyo.

Hadi kufikia Machi 27, 2020 watu zaidi ya milioni 21.8 wamejitokeza na kujisajili ili kupatiwa vitambulisho ambapo kati ya hao zaidi ya milioni 17.8 wamepatiwa namba za vitambulisho huku waliopatiwa vitambulisho wakiwa milioni 6 tu.

Waziri aliwaomba radhi Watanzania kwa kucheleweshewa kupata kwa wakati vitambulisho hivyo vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

“Kumekuwa na changamoto nyingi katika maeneo ya serikali za mitaa juu ya ucheleweshwaji wa vitambulisho vya Nida, wananchi kutopata huduma nzuri katika ofisi za Nida, idadi ndogo ya watumishi, kuharibika mashine ya kuzalishia vitambulisho, changamoto ni nyingi na nyingine zimechangiwa na usimamizi mbovu,” alisema.

Alisema ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma iliyo bora wakurugenzi wa halmashauri pamoja na wakuu wa wilaya wawasimamie watendaji wa Nida katika ufanyaji kazi wao.

Aliwataka baadhi wa watendaji wa Nida hususani maeneo ya mipaka kuwatumia viongozi wa Serikali za mitaa kuwatambua raia halali na wale ambao si Watanzania ili kuepuka kutoa vitambulisho kwa watu ambao si wahusika.

Aliwakemea baadhi ya watendaji wa mamlaka hiyo wanaowaambia wananchi kuwa wao si raia wa Tanzania bila kuwashirikisha viongozi wa Serikali za mitaa husika.

Ili kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inafanya kazi kwa weledi, Simbachwene aliahidi kufanya mabadiliko makubwa katika mamlaka hiyo ndani ya siku chache zijazo.