Sh340 bilioni zatumika kukarabati miundombinu ya shule Tanzania

Baadhi ya wadau wa vitabu akiwamo Jack line Mengi wakionyesha vitabu vya mchepuo wa kingereza na vilivyo andikwa kwa mfumo wa nukta nundu kwa ajili ya watoto wasioona

Muktasari:

Zaidi ya Sh340 bilioni imetumika kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari nchini Tanzania katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh340 bilioni imetumika kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari nchini Tanzania katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  William Olenasha  leo Alhamisi Februari 27, 2020 wakati akizindua usambazaji wa vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza kwa ajili ya shule za mchepuo huo.

Vitabu vingine vilivyoanza kusambazwa ni vilivyoandikwa kwa mfumo wa nukta nundu na vilivyokuzwa maandishi kwa ajili ya wanafunzi wasioona na walio na uoni hafifu.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Olenasha amesema usambazaji wa vitabu shuleni ni kati ya mkakati ya kuboresha elimu inayoenda sambamba na kazi za ukarabati na ujenzi wa shule.

"Maudhui ya elimu yapo ndani ya vitabu hivyo hatuishii kujenga na kukarabati shule tu isipokuwa pamoja na kuhakikisha maudhui yanakuwepo shuleni," amesema.

Amewataka wamiliki wa shule binafsi kutumia vitabu hivyo katika kufundishia ili waende sambamba na mtalaa wa elimu.

Awali, mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET),  Aneth Komba amesema zaidi ya vitabu 1.3 milioni vyenye thamani ya zaidi ya  Sh2  milioni vimechapishwa na kuanza kusambazwa shuleni.

Amesema vitabu vilivyosambazwa ni vya wanafunzi wa darasa kwanza mpaka la sita kwa mchepuo wa Kiingereza na shule ya msingi mpaka sekondari kwa wanafunzi wasioona.

Amezitaka shule zote nchini kutumia vitabu vyenye ithibati kwa ajili ya kufundishia na si vinginevyo.