Shahidi kesi ya kina Mbowe aieleza mahakama alivyowatawanya

Dar es Salam. Mrakibu mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi jana aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliamuru askari kupiga mabomu na risasi hewani kwa ajili ya kusambaratisha maandamano ya viongozi na wafuasi wa Chadema.

Ngiichi, shahidi wa kwanza katika kesi ya kufanya mikusanyiko isiyo halali inayowakabili viongozi tisa wa chama hicho akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Shahidi huyo alisema maandamano hayo yalifanyika Februari 16, 2018 wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni.

Ngiichi ambaye ni ofisa operesheni wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, alitoa ushahidi wake kwa saa sita kuanzia saa 4:25 asubuhi hadi saa 10:15 jioni.

Akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi, Ngiichi alidai siku hiyo kulikuwa na mikutano mikubwa mitatu ya vyama vya CCM, Chadema na CUF.

“Mkutano wa CUF ulifanyika viwanja vya Vegas Makumbusho, wa Chadema ulifanyika viwanja vya Buibui Mwananyamala na CCM ulifanyika viwanja vya Biafra Kinondoni,” alidai Ngiichi ambaye aliajiriwa na polisi mwaka 2000.

Alidai katika mikutano hiyo alipanga maofisa watatu wa ngazi ya juu kutoka jeshi hilo ili kusimamia.

“Mkutano wa Chadema ulisimamiwa na SSP Dotto, mkutano wa CCM ulisimamiwa na SP Magai na mkutano wa CUF ulisimamiwa na SP Batiseba. Wakati mikutano hiyo ikielekea ukingoni, nilipigiwa siku na SSP Dotto na kupewa taarifa kuwa kwenye mkutano wa Chadema kuna dalili za kuwapo kwa uvunjifu wa amani,” alidai.

“Nilimwelekeza ofisa huyo kusimamia kwa weledi mkutano huo na awaelekeze askari wachukue kumbukumbu za matukio ya uvunjifu wa amani.”

Alidai kuwa licha ya SSP Dotto kuwaonya viongozi wa Chadema kuendelea na mkutano badala ya maandamano, lakini Mbowe na wenzake walikaidi amri hiyo na kuhamasisha wananchi kuanza maandamano.

“Niliamuru askari waliokuwa na mabomu ya moshi kuyapiga, lakini hakukuwa na mwitikio wa kutawanyika kwa waandamanaji kwa sababu mabomu yaliathiriwa na upepo, hivyo moshi ulikuwa ukirudi upande wa askari, na hivyo waandamanaji hao walianza kurusha mawe, miti na chupa na kusababisha askari wawili kujeruhiwa na kudondoka chini,” alidai Ngiichi.

Shahidi huyo alidai baadaye aliagiza askari wenye silaha kuwatawanya waandamaji hao.

Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 13, 14 na 15 itakapoendelea.