Sherehe, harusi zawekwa njia panda

Dar es Salaam. Wakati maharusi waliopanga kufunga ndoa siku za karibuni, wakibaki njia panda kutokana na kuzuiwa kwa mikusanyiko baada ya kutokea mlipuko wa virusi vya corona, baadhi ya watoa huduma wanatafakari kutafuta kazi nyingine za kuingiza kipato.

Tangu Machi 16 baada ya Tanzania kujulikana kuwa ina mgonjwa wa kwanza wa virusi vya corona, Covid-19, Serikali ilifunga kwa siku 30 shule na vyuo na kuzuia shughuli zinazokusanya watu kama mikutano, semina, warsha na shughuli za michezo.

Moja kwa moja amri hiyo imeathiri sherehe, hasa harusi ambazo hata hivyo mwezi huu hupungua kwa Wakristo kutokana na Kwaresma, lakini hali ya kuendelea kusambaa haitoi mwanga wa amri hiyo kuondolewa karibuni.

Nyuma ya sherehe hizo kuna washereheshaji, wapigapicha, wapambaji, watoa huduma za chakula na Ma-DJ.

“Baada ya mipango na maandalizi yote tusogeze mbele?” alisema Joyce Komba, 31, bibi harusi mtarajiwa wa jijini Dar es Salaam.

“Tulitamani tukio hilo lifanikiwe, lakini inaonyesha Covid-19 imeufanya mwaka 2020 kuwa mbaya kwetu.”

Joyce na mchumba wake, Thomas Mushi (36) walishaalika wageni 150 katika harusi yao iliyokuwa ifanyike Aprili 4 jijini Dar es Salaam, lakini hawataweza kufanya hivyo kutokana na amri hiyo.

Wawili hao wamelazimika kuahirisha tukio hilo la kihistoria maishani mwao kwa sababu hata ukumbi walioukodi umezuiwa kukusanya watu na hata ndugu wa karibu wameshajiondoa katika mipango hiyo.

“Nilifikiria kufuta sherehe yote, lakini kwa kuwa asilimia 95 ya ndugu na marafiki walikuwa wamechangia, ikawa vigumu kufuta,” anasema mchumba wake, Mushi.

“Bajeti nzima inafikia Sh15 milioni na kamati ilikuwa imeshapokea Sh10 milioni. Kiasi cha fedha kilishatumika kulipia ukumbi na chakula. Ni vigumu kuzirudisha.”

Bibi harusi mwingine mtarajiwa, Loveness Thompson (26) alikuwa afunge ndoa Machi 29 katika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza, lakini imeshindikana.

“Kwa kweli nimechanganyikiwa,” alisema Loveness.

“Inabidi nifanye mipango mingine, labda baadaye mwaka huu. Inakatisha tamaa lakini naamini Mungu ataiponya nchi yetu.”

Mbali na maharusi, kamati za maandalizi zimeanza kujadiliana na watoa huduma kuhusu fedha zilizowalipa kwa sababu waalikwa wameshaanza kujitoa katika harusi zilizopangwa.

“Tunapitia kipindi kigumu kwa sasa. Tunajaribu kuwashawishi wenye kumbi na watu wa vyakula kwa sababu tulishawalipa fedha na hatujui janga hili litaisha lini,” alisema mmoja wa wanakamati aliyejitambulisha kwa jina la Japhet Munira.

Mwanakamati huyo alisema baadhi ya wageni walishapanga kutohudhuria sherehe hizo kutokana na ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mussa Iddi ambaye ni wakala wa usafiri na fungate wa Zanzibar anayeishi Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam alisema biashara yake imeyumba kipindi hiki kwa kuwa wateja wake wengi wamesogeza mbele sherehe na wengine wakihamishia shughuli zao sehemu nyingine.

“Kila mtu ametishwa na taarifa za ugonjwa wa corona. Hakuna anayetaka huduma hii ya fungate na walioomba wamesogeza mbele,” alisema Idd akiwa katika ofisi yake ya Msimbazi Centre.

Wauza nguo za harusi

Mlipuko wa virusi vya corona pia umewakumba wauza nguo za harusi.

Duka la Modern Bride Shop la Kariakoo jijini Dar es Salaam lilikuwa likipokea maombi ya hadi nguo 50 za harusi kutoka China kati ya Februari na Mei kila mwaka, lakini hadi sasa limepokea nguo nne tu kutokana na taarifa za ugonjwa huo.

“Wateja wetu wengi walipendelea mavazi kutoka China kwa sababu ni ya bei nafuu kuliko yanayoshonwa hapa nchini.

“Kwa kuwa mimi ni mfanyabiashara, nimelazimika kurejesha fedha za watu waliokuwa wametanguliza malipo kwa sababu hakuna biashara na mwezi ujao ninafunga ili niende likizo Mtwara,” alisema Hamisi Mtebe, mmiliki wa duka hilo.

“Wafanyabiashara wote wa mavazi wameathirika na hali hii. Kama harusi ilipangwa kuwa Juni, vazi lilitakiwa liwe limefika Februari, lakini halitaweza kufika hadi Mei, utamwambia nini mteja?” Alihoji Mperi Johnson ambaye ni mfanyakazi katika duka la mavazi ya harusi la Golden Weds la Kariakoo.

Washereheshaji walia

Waathirika wengine ni washereheshaji. Thomas Michael, maarufu kwa jina la MC Chipolopolo, amesema kuzuiwa kwa mikusanyiko kumevurugga biashara yao.

“Tunaiunga mkono Serikali kwa kuzuia mikusanyiko, lakini tumeathirika sana. Utakuta mteja ameshatoa advance (malipo ya awali), lakini kwa kuwa harusi imeahirishwa, mnapanga tarehe nyingine, lakini tarehe hiyo inagongana na harusi nyingine. Ni mvurugano tu,” alisema MC Chipolopolo.

Chipolopolo ambaye ni mwanachama wa Chama cha Washereheshaji (SAA) alisema hupata wastani wa kazi nne kwa mwezi, lakini kwa Machi amelazimika kupumzika, bila kujua atapataje fedha.