Shinikizo la uchaguzi huru linavyoongezeka nchini

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Joto la uchaguzi mkuu limeonekana kuanza kupanda, huku kukiwa na shinikizo la kufanyika uchaguzi katika mazingira huru na ya haki.

Hali hiyo imechangiwa na kauli iliyotolewa hivi karibuni na Rais John Magufuli alipozungumza na mabalozi wa nchi tofauti katika sherehe ya kukaribisha mwaka mpya kwa kuahidi kufanyika uchaguzi huru na wa haki mwaka huu.

Kauli hiyo iliibua mjadala miongoni mwa mwanasiasa na wanaharakati ambao walihoji uwezekano wa jambo hilo kufanyika bila kufanyiwa kazi kasoro zinazolalamikiwa kwa muda mrefu.

Katika taarifa iliyoonyesha suala hilo limeigusa dunia, ubalozi wa Marekani nchini, ulipongeza kauli ya Rais Magufuli na kutoa wito wa kutaka kuharakishwa kwa uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi.

Taarifa ya ubalozi ilitaka kuharakishwa kwa kazi ya uandikishaji wapigakura ukitaka ufanyike kwa uwazi, kuanzishwa kwa tume huru ya uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na wa kimataifa wa kuaminika.

Ubalozi huo umesema unatarajia kuwepo kwa uchaguzi wa amani ambao wagombea watakutana kwa amani wakieleza mawazo yao na kampeni zitakazofanyika katika misingi ya usawa.

Taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani ilikuwa kamaimefungua mlango wa watu na taasisi tofauti kuanza kuweka shinikizo la kutekelezwa kwa ahadi hiyo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliingilia mlango huo alipowaeleza waandishi kuwa amemuandikia barua Rais akimuomba kufanyia kazi mambo matatu ili uchaguzi mwa mwaka huu uwe huru na wa haki.

Mbowe alisema amemuomba kufanyike marekebisho ya katiba yatakayozaa tume huru ya uchaguzi, kufutwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana na kurudiwa na kuanza mchakato wa maridhiano ya kitaifa.

“Kufutwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa kutahalalisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu (uchaguzi mkuu) utakuwa huru na wa haki. Uchaguzi huo ufanyike sambamba na uchaguzi mkuu,” alisema Mbowe.

“Mambo hayo matatu yasiposhughulikiwa, Chadema isilaumiwe kwa yatakayotokea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020. Kwa hali ilivyo kuna kila aina ya kiashiria cha kutokea machafuko ya kisiasa kama hatutazika viburi vyetu vya kiitikadi na kusimama pamoja.”.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Mbowe kushauri kuhusu maridhiano ya kitaifa, baada ya kufanya hivyo Desemba 9 mwaka jana wakati alipopewa nafasi na Rais ya kuzungumza katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika jijini Mwanza.

Kwa upande mwingine, mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe naye ametaka kuitishwa mkutano wa kitaifa wa maridhiano ya kisiasa, ili changamoto zote za uendeshaji wa siasa nchini zijadiliwe na kukubaliana kanuni za demokrasia ya vyama vingi.

Alisema kama watawala wanaona vyama vya upinzani ni kero, wawaeleze katika mkutano huo na wao watasema yao.

“Pawe na maridhiano, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wakulima na wafugaji, vyama vya wafanyabiashara na vinginevyo vishiriki katika mkutano huo kwa lengo la kuhakikisha tunapata uwiano, tunapata maridhiano ya namna gani ya kufanya siasa,” alisema Zitto.

“Kuendelea kufanya siasa kwa namna hii, na mambo mabaya yanaweza kutokea katika nchi yetu, na sisi wanasiasa tutawajibika.”

Maoni

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anasema ni hatari kuingia katika uchaguzi mkuu wakati kuna walakini katika umoja wa kitaifa na kusema suala la nchi linapaswa kupewa kipaumbele na vyama vikafuata baadaye.

“Amani ni tunda la haki, ili amani itawale katika uchaguzi mkuu ni lazima kuwepo na haki sawa ya kufanya siasa,” anasema.

Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof Mwesiga Baregu, anasema nchi inahitaji maridhiano kwa lengo la kujenga demokrasia makini.

“Kuna wakati nilikutana na Mwalimu Nyerere, nadhani nilikuwa NCCR-Mageuzi na akasema nikae hukohuko kwa sababu tunataka kujenga demokrasia imara,” alisema.

“Sasa inawezekana hakulizungumza jambo hili kwa wengine ndani ya CCM. Mimi nawakumbusha ndio misingi ya Mwalimu Nyerere kukubali mfumo wa vyama vingi, ili tuwe na demokrasia imara katika nchi yetu na kwa maana hiyo tuwe na nchi inayotenda haki inayoonekana kwa wananchi wake,” anasema.

Mbunge wa viti maalum (Chadema), Upendo Peneza pia amemuomba Rais Magufuli akubali maridhiano na viongozi wa upinzani kabla ya uchaguzi mkuu.

“Nitoe shukrani zangu za pekee kwa Rais wa Tanzania kwa kauli yake kuwa uchaguzi mkuu 2020 utakuwa huru na haki. Niombe Serikali ifanye mabadiliko katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa kuwaondoa wakurugenzi waliopo, ili kuwe na uchaguzi wa haki na huru,” anasema.

Pia anasema anaunga mkono kauli ya Mbowe ya kuwapo kwa maridhiano ya kitaifa, ili kundoa changamoto zilizopo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Innocent Moya anasema: “Sehemu pekee ambayo tunaweza tukajenga umoja wa kitaifa ni wakati huu tunapoelekea uchaguzi mkuu, tunachotakiwa kujua siasa zitakuwepo lakini Tanzania yetu itaendelea kuwepo siku zote.”

Anatoa mfano wa maridhiano yaliyofanyika Zanzibar na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambayo yalichangia kufanyika uchaguzi wa amani na hata malalamiko yaliyokuwapo miaka ya nyuma hayakuwapo.

Anasema hata Kenya baada ya kutokea machafuko ya mwaka 2007 na kuundwa Serikali ya umoja wa kitaifa, waliweza kutibu makovu yaliyotokana na machafuko ya kisiasa.

“Pia tunaweza kujifunza kwa kilichotokea Kenya kwa kuanzisha mchakato wa BBI mwaka jana. Ni mwelekeo wa wao kuamini kuwa maelewano, mazungumzo ya umoja wa kitaifa labda yanaweza kutibu ile hali ya kisiasa iliyotokea katika uchaguzi wa mwisho nchini humo.

“Hata Zimbabwe waliiunda serikali ya umoja wa kitaifa chini ya marehemu Robert Mugabe na marehemu Tshangirai. Hii inaweza kutupa picha kuwa Mbowe na vyama vya upinzani kwa ujumla wameona mafanikio chanya kwa baadhi ya wenzetu walioitikia wito wa kufanya mazungumzo na kukubaliana jinsi ya kufanya siasa,” anasema mchambuzi huyo.

“Ni wakati muafaka kwa mamlaka zinazohusika kusikiliza hoja hizo na kuzifanyia kazi kwa kukaa na kujadiliana kwa pamoja, kwa kuwa mambo hayo yanalenga kuona Tanzania inaendelea kuwa na amani.”