Siku tatu ngumu kwa Mbowe, wenzake

Dar es Salaam. Kuanzia Septemba 17 hadi 19, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wanane wa chama hicho watakuwa na kazi ya kujitetea katika kesi inayowakabili ya uchochezi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kuamua kuwa wanasiasa hao wana kesi ya kujibu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema katika uamuzi wake jana kuwa mahakama imepitia ushahidi wa mashahidi wanane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo saba na kujiridha kuwa washtakiwa hao wana kesi ya kujibu.

Hakimu Simba alisema washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 112/2018 na watatakiwa kujitetea Septemba 17, 18 na 19.

Kesi ya viongozi hao inatokana na matukio ya Februari 18 ambayo pia yalihusisha kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwilini aliyepigwa risasi akiwa ndani ya basi dogo la daladala.

Mbowe na wenzake, ambao ni pamoja na wabunge sita na watendaji wa Chadema wanakabiliwa na kesi ya kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya February Mosi na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba alisema ameridhika na vielelezo vilivyotolewa mahakamani.

“Mahakama baada ya kupitia ushahidi mmoja mmoja wa mashahidi nane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo saba vilivyotolewa mahakamani hapa na kama ushahidi, imejiridhisha kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanak esi ya kujibu,” alisema Hakimu Simba

Hakimu Simba alisema washtakiwa wote wamekutwa na kesi ya kujibu katika kila kosa waliloshtakiwa, hivyo kila mmoja atatakiwa kujitetea.

“Baada washtakiwa kukutwa na kesi ya kujibu, mahakama hii imepanga Septemba 17, 18 na 19 mwaka huu, washtakiwa hawa kuanza kujitetea,” alisema Hakimu Simba na kuahirisha kesi hiyo.

Baada ya kutoa uamuzi huo, wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari aliomba kueleza jambo, lakini Hakimu Simba alisema ameshapanga tarehe kwa ajili ya washtakiwa hao kujitetea, hivyo hawezi kuongea chochote.

Kabla ya uamuzi huo, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai kuwa upande wao ulikuwa umuulize maswali shahidi wao kuhusu kile alichohojiwa juzi na upande wa utetezi.

Nchimbi alidai kuwa baada ya kufanya tathimini ya maswali aliyoulizwa Bernard Nyambari (42) ambaye ni mkuu wa upelelezi wa Mbagala, wameona hawana haja ya kumuuliza chochote shahidi huyo.

“Tumefanya tathimini ya maswali yaliyoulizwa na upande wa utetezi na hivyo tumeona hatuna haja ya kumuuliza shahidi wetu swali lolote kuhusu kile alichojibu wakati anahojiwa na upande wa utetezi,” alidai Nchimbi.

“Kwa mukhtadha huo, upande wa mashtaka tunafunga rasmi ushahidi wetu wa mashahidi wanane waliotoa dhidi ya washtakiwa hawa.”

Mbali na Mbowe, wengine walioshtakiwa katika kesi hiyo ni Esther Matiko, ambaye ni mbunge wa Tarime Mjini, Peter Msigwa (mbunge, Iringa Mjini), John Mnyika (Kibamba), Ester Bulaya (Bunda), Halima Mdee (Kawe), na John Heche (Tarime Vijijini).

Wengine ni Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar) na Dk Vicent Mashinji ambaye ni katibu mkuu wa chama hicho.

Upande wa mashtaka ulianza kusikiliza ushahidi wao Aprili 17, 2019 hadi jana na kufunga, hivyo wametumia miezi miwili na siku 27.

Ushahidi wa Nyambari

Juzi, Nyambari ambaye ni mrakibu msaidizi wa Jeshi la Polisi, alitoa ushahidi wake wa masaa matano kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao, Shahidi huyo alihojiwa na mawakili watatu wa upande wa utetezi- Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Hekima Mwasipu- kuhusu ushahidi wake

Idadi ya mashahidi waliotoa ushahidi:

Mbali na Nyambari, wengine waliotoa ushahidi dhidi ya vigogo hao wa Chadema ni Victoria Wihenge (34) ambaye ni ofisa uchaguzi kutoka Manispaa ya Kinondoni na Koplo Charles, kutoka kituo cha polisi cha Oysterbay.

Wengine ni Dk Juma Khalfani (54), ambaye ni daktari msaidizi kutoka Hospitali Kuu ya Jeshi la Polisi, Kilwa Road, Fikiri Mgeta kutoka kituo cha polisi cha Osterbay na ofisa operesheni kutoka mkoa wa Kinondoni, SSP Gerald Ngi’chi.

Ngi’chi ambaye ni mrakibu msaidizi wa jeshi hilo, ndio shahidi wa kwanza katika kesi hiyo na alitoa ushahidi wake Aprili 17, 2019.