Simiyu haitaki mchezo ufaulu darasa la saba

Mikoani. Mkoa wa Dodoma upo katika hali mbaya kwa kuwa katika orodha ya mikoa mitano inayoshika mkia tangu mwaka 2016, lakini Mkoa wa Simiyu ambao mwaka jana ulishika nafasi ya 22, safari hii umetinga kumi bora.

Katika matokeo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Simiyu imeshika nafasi ya nane ikiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 86.46.

Nafasi ya mkoa huo kitaifa inaonyesha mwaka 2016 na 2017, Simiyu ilishika nafasi ya 14 na 16 mtawalia kabla ya kuporomoka hadi nafasi ya 22 katika matokeo ya mwaka 2018. Katibu tawala mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini anasema matokeo hayo ni mafanikio ya pamoja ya uongozi wa Serikali chini ya maelekezo na usimamizi wa mkuu wa mkoa, Anthony Mtaka.

Dodoma hali mbaya

Kutoka katika kashfa ya moja ya wilaya zake kufutiwa matokeo katika mtihani wa mwaka jana, Mkoa wa Dodoma bado haujatengemaa. Tangu mwaka 2016, umekuwa haukosekani katika orodha ya mikoa mitano ya mwisho.

Matokeo ya mkoa huo yanaonyesha mwaka 2016 ulikuwa wa 24 kati ya mikoa 26, mwaka 2017 ukashika nafasi hiyo, kabla ya kupata ahueni kidogo kwa kupanda nafasi moja kwa kushika nafasi ya 23, ambayo hata hivyo haikuuzuia mkoa huo kuwa katika orodha ya mikoa iliyofanya vibaya zaidi.

Uchambuzi wa Mwananchi unaonyesha mikoa ifuatayo imekuwa ikishika katika nafasi tano za mwisho.

Mwaka 2016 kulikuwa na mikoa ya Mbeya (22), Morogoro (23), Dodoma (24), Mtwara (25) na Songwe (26). Mwaka 2017 kulikuwa na mikoa ya Mtwara (22), Songwe (23), Dodoma (24), Manyara (25) na Singida (26).

Mwaka 2018 mikoa iliyokuwamo ni Simiyu (22), Dodoma (23), Lindi (24), Kigoma (25) na Mara (26).