Swali kuhusu uchaguzi Serikali za mitaa lazua jambo bungeni

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Devota Minja  akiwa amesimama bungeni leo baada ya kukataliwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kuendelea na kuuliza swali baada ya kukiuka kanuni. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amempiga ‘stop’ mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Devotha Minja kuuliza swali la hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa madai kuwa kanuni za chombo hicho cha Dola haziruhusu mbunge kuandikiwa swali.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amempiga ‘stop’ mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Devotha Minja kuuliza swali la hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa madai kuwa kanuni za chombo hicho cha Dola haziruhusu mbunge kuandikiwa swali.

Ndugai ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 14, 2019 baada ya Devotha kuanza kuuliza swali kuhusu mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Devotha alianza kuzungumzia kauli zilizotolewa na waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo  na naibu wake, Mwita Waitara kuhusu uchaguzi huo uliokumbwa na hali ya sintofahamu baada ya vyama saba vya upinzani kujitoa.

Kabla ya Devotha kuanza kujikita katika swali, Ndugai  alimkatisha na kusema kanuni za Bunge zinakataza mbunge kuandikiwa swali, kulisoma bungeni.

“Swali hilo linaonekana si lako umeandikiwa na waliokutuma,” amesema Ndugai na kumuita mbunge mwingine kuuliza swali huku Devotha akisema hakuandikiwa swali hilo.

Awali, mbunge wa Mkalama (CCM),  Allan Kiula amesema kumekuwa na hofu kwa baadhi ya Watanzania kuhusu  haki ya kupiga na kupigiwa kura katika uchaguzi huo na kutaka kujua kauli ya Serikali.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema kwa utaratibu ambao unaoongozwa kwa kanuni na sheria anaamini kuwa kila Mtanzania atapata haki yake.

“Muhimu ni kuzingatia hizo kanuni, sheria na taratibu ili uweze kutimiza azma ya kumchagua kiongozi unayemtaka kwenye eneo ambalo ulipo,” amesema.

Majaliwa ametaka wananchi kwenda kusikiliza sera za wagombea ili kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Vyama vilivyojitoa katika uchaguzi huo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP, CUF, ACT-Wazalendo na Chauma.