TLS yatia mguu kesi ukomo wa urais

Dar es Salaam. Kesi ya kikatiba inayohusu ukomo wa urais iliyofunguliwa na mkulima Patrick Dezydelius Mgoya inazidi kuvutia wadau baada ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kujitosa katika kesi hiyo.

TLS imefungua maombi Mahakama Kuu ya kuunganishwa katika kesi hiyo huku katika hati ya faragha ya maombi hayo ikieleza kuwa inaomba kuunganishwa katika shauri hilo kama mdaiwa mwenye maslahi.

Maombi ya TLS yaliyowasilishwa mahakamani hapo Oktoba 30 na kusajiliwa Novemba 5, mwaka huu yamepangwa kusikilizwa na Jaji Benhajj Masoud Jumatatu asubuhi.

Taasisi hiyo ya kisheria inakuwa taasisi ya pili kuomba kuunganishwa katika kesi hiyo ikitanguliwa na chama cha ACT Wazalendo.

Wakati TLS wakisubiri kujua hatima yao ya kujiunga katika kesi hiyo baada ya maombi yao kusikilizwa na mahakama kuyatolea uamuzi wa kukiruhusu au la, ACT waliowasilisha maombi yao Septemba 30 walikubaliwa na mahakama kujiunga katika kesi hiyo Oktoba 24.

TLS katika kiapo cha makamu wake wa rais, Wakili Mpale Mpoki kinaeleza kuwa miongoni mwa majukumu ya taasisi hiyo ni kulinda na kuisaidia jamii katika masuala yote ya kisheria na kuisaidia Serikali na mahakama masuala yote yanayoathiri utungwaji na usimamizi wa sheria nchini.

“Shauri lililoletwa na mjibu maombi wa kwanza, lina maslahi kwa umma hivyo matokeo yake yanaweza kuwa na athari kwa umma. Mwombaji (TLS) ataathirika na matokeo ya shauri lililotajwa,” anaeleza Wakili Mpoki katika kiapo chake hicho.

Wakili Mpoki anasisitiza kuwa TLS isipounganishwa katika shauri hilo itakuwa imenyimwa haki ya kusikilizwa ambayo ni haki ya msingi na ikiunganishwa basi itaweza kutekeleza jukumu lake hilo la kisheria, lililo chini ya sheria iliyoanzisha taasisi hiyo.

Mgoya, maarufu kama mkulima amefungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiiomba mahakama itoe tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya Ibara ya 40(2) ya Katiba ya nchi inayoweka ukomo wa mtu kuchaguliwa kuwa rais.

Anadai masharti ya ibara hiyo ya 40(2) ya mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais yaani miaka 10 (vipindi viwili vya miaka mitano mitano) yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) hasa haki za kuchagua na kuchaguliwa.

Serikali kupitia kwa AG imeshamwekea pingamizi la awali ikiiomba mahakama itupilie mbali pamoja na mambo mengine ikidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, na kwamba kesi ina kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

Pia Serikali inadai kuwa mwombaji hana haki kisheria kufungua na kwamba nafuu anazoziomba mwombaji haziwezi kutolewa kwa kuwa zinakiuka kifungu cha 44 cha Sheria ya Mawakili, Sura ya 341, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Shauri la msingi linalosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Kiongozi Eliezer Feleshi, akishirikiana na Dk Benhajj Masoud na Seif Kulita limepangwa kutajwa Novemba 22 mwaka huu.