TMA: Upepo ukiongezeka nzige wanaweza kuingia Tanzania

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza utabiri wa mwenendo wa hali ya hewa kwa mikoa ya Kaskazini inayopakana na Kenya na kubainisha kuwa endapo upepo utaongezeka kuna uwezekano wa kuongeza kasi ya nzige kuingia Tanzania.

Juzi TMA ilisema upepo unaovuma sasa ni wa kasi ya kilomita 20 hadi 25, hivyo ni kiwango hafifu ambacho hakiwezi kuhamisha nzige kutoka nchi hiyo kuja Tanzania kwa kuwa “Ili nzige wahame unatakiwa kufika kilomita 28 kwa saa.”

Akizungumza na Mwananchi jana ofisa uhusiano wa TMA, Monica Mutoni alisema upepo ndio unaowasukuma nzige kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Yaani upepo imekuwa kama unawaendesha, ukiwa mkali unawasukuma, hivyo kama utaongezeka utaongeza kasi ya wadudu hao kufika nchini,” alisema Monica.

Kundi la nzige lilionekana Februari 9 , mwaka huu katika Wilaya ya Moshi na kisha kutokomea kusikojulikana na hadi jana Februari 12 hawakuthibitishwa kuingia nchini.

Taarifa ya kuonekana kwa nzige hao ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu nzige hao kuingia Tanzania wakitokea Kenya.

Mbali na nzige, TMA ilitangaza mvua kubwa katika mikoa mbalimbali nchini.