TMA yafafanua mvua kubwa inayonyesha Dar

Muktasari:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema tangu kuanza kwa mvua zisizo za msimu ukanda wa Dar es Salaam umepata kiasi kikubwa cha mvua cha zaidi ya mililita 145 ambacho ni kiwango kikubwa kwa mvua hizo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema tangu kuanza kwa mvua zisizo za msimu ukanda wa Dar es Salaam umepata kiasi kikubwa cha mvua cha zaidi ya mililita 145 ambacho ni kiwango kikubwa kwa mvua hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema maeneo ya Pwani ya Kusini mvua hizo zimeanza nje ya msimu kutokana na mgandamizo uliojitokeza uliosababisha  kuongezeka kwa mvua katika ukanda wa Pwani.

Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha baadhi ya maeneo kujaa maji, kutopitika jambo ambalo limekuwa usumbufu kwa wananchi, wanaotumia magari.

“Mpaka sasa ukanda wa Dar es Salaam tumesharekodi mvua za mililita zaidi ya 145 ni mvua kubwa  pamoja na Pwani ya Kaskazini.”

“Na hizi mvua za nje ya msimu mifumo inaonyesha zitaendelea kwa muda hivyo tunawashauri wakulima ukanda wa Kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, Arusha na Manyara wanaweza kuzitumia kuanza  kilimo,” amesema Dk Kijazi.

Akizungumzia mvua za msimu, Dk Kijazi ametoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo mbalimbali na kwamba TMA inatarajia kuwepo kwa mvua zitakazoambatana na mawimbi makubwa baharini na upepo mkali.