TMDA yabaini aina saba ya dawa bandia zikiuzwa

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba, Akida Khea akionyesha baadhi ya dawa zilizokamtwa hivi karibuni kwenye ukaguzi maalumu uliofanyika nchini, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Ukaguzi huo ulikuwa na lengo la kubaini, kukamata na kuondoa dawa duni na bandia za binadamu na mifugo. Picha na Salim Shao

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) imesema kuna dawa bandia aina saba katika mzunguko, zikiwemo za sulphadoxine pyrimethamine (SP) zinazotibu malaria.

TMDA ilibaini dawa hizo bandia katika oparesheni iliyohusisha maeneo 558 ambayo yana maduka 209 ya dawa, maduka 263 ya dawa muhimu, vituo 27 vya huduma za afya, maduka 21 ya vifaatiba na vituo 38 vya dawa asili na tiba mbadala katika maeneo ya pembezoni ya mikoa, hasa Kigoma, Arusha na Kilimanjaro.

Mpaka sasa, TMDA imeshakamata dawa bandia zenye thamani ya Sh12 milioni katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na Tamisemi, Baraza la Famasia, Baraza la Dawa Asili na Tiba Mbadala.

Kaimu mkurugenzi wa TMDA, Akida Khea alisema hayo jana wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi uliofanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 18 katika wilaya 33 na mikoa 20. “Dawa hizo ni pamoja na inayotibu malaria sulphadoxine pyrimethamine (SP), dawa za kupaka za Sonadem Cream 10gm, Gentrisone Cream 10gm, Alprim, Homidium Chloride, Cold Cap na Temevac NDV (chanjo ya kuku ya ugonjwa wa mdondo),” alisema Khea.

Alisema kopo la dawa ya SP lina namba ya kughushi ya usajili ya TAN na kwamba dawa za Sonaderm toleo namba A1912 na A1758 na Gentrisone toleo namba GNTRO X030 zilizotengenezwa 21/04/2019 ni bandia na hazina viambato hai.

Naye Dk Chanasa Ngeleja kutoka Wakala wa Maabara ya Dawa za Mifugo alisema chanjo za kuku zilizobainika kuwa bandia ni Temevac NDV ambazo alisema zina tofauti kubwa na dawa halisi.

Alisema dawa hiyo bandia imeandikwa kwa Kiingereza na ina makosa ya kisarufi katika lebo na inaonyesha imetengenezwa na kiwanda cha Vaccine Institution of Holland.

“Katika kiwanda hiki cha Serikali kinachotengeneza dawa halisi cha TVI Kibaha, kwa taarifa, ni kwamba dawa hii ni bandia na haina viambato hai vyovyote,” alisema Dk Ngeleja.

Kwa upande mwingine, Khea alisema pia wamebaini kuwepo kwa dawa za Serikali zenye nembo ya GOT zinazouzwa katika maduka binafsi na kwamba wamefanikiwa kukamata dawa zenye thamani ya Sh481,600 na vifaatiba vya thamani ya Sh224,300 vikiwemo aina ya SD Bioline kwa ajili ya kupima virusi vya Ukimwi, kaswende na malaria, na vifaa tiba aina ya cannula na pamba.

Pia alisema wamekamata dawa na vifaatiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya Sh48 milioni, ikiwa ni matokeo ya ukaguzi maalumu wa dawa, vifaatiba na vitendanishi, dawa asili na mbadala uliofanyika kati ya Oktoba 8 hadi 11.

Alisema walikamata dawa zenye thamani ya Sh31,934,360 baadhi yake zikiwa kapsuli za dawa inayotambulika kwa jina la Indowin, vidonge vya dawa yenye mchanganyiko wa artesunate na amodiaquine, kapsuli za dawa inayojulikana kwa jina la Coldwin na sindano ya magnesium sulphate.

Pia, alisema oparesheni hiyo ilikamata vifaatiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya Sh16,384,750.

“Baadhi yake ni pamoja na Magnetic Quantum Analyser (3), Quantum Therapy Analyzer pamoja na aina mbalimbali ya kondomu kama vile Ultimate Condoms, Classic Maximum Protection na Prudence Condoms,” alisema.

Alisema pia kulibainika vifaatiba duni vyenye thamani ya Sh640,000 kama bandeji na H.Pylori Rapid Test.

Mrakibu wa jeshi la polisi kutoka makao makuu ya upelelezi, Alekunda Urio alisema maeneo yote yaliyopatikana na dawa bandia, dawa, vifaatiba au vitendanishi vya Serikali watafikishwa katika vyombo vya sheria na jumla ya majalada 19 ya kesi yalifunguliwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.

“Baada ya uchunguzi wa makosa kukamilishwa na jeshi la polisi na ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali, hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani kulingana na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura 219 na sheria nyingine za nchi,” alisema Urio.

Wafamasia wanena

Mwananchi haikuweza kuona dawa hizo katika maduka iliyotembelea jijini Dar es Salaam, lakini baadhi ya wauzaji wa maduka ya dawa walisema ni vigumu kubaini dawa bandia kutokana na kufanana kwa bidhaa.

Joseph Mushi, anayemiliki duka la dawa, alisema mamlaka zinapaswa kutoa elimu mara kwa mara kwa wamiliki ili kujiepusha kubambikiwa bidhaa bandia