TRA yatuhumiwa kukata mitaji

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imesema kitendo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kulimbikiza madeni ya madai ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kimesababisha wafanyabiashara kupunguza mitaji yao.

Akisoma taarifa ya kamati hiyo juzi makamu mwenyekiti wake, Masoud Ally Khamis alisema mwenendo wa urejeshaji fedha hizo si wa kuridhisha na unalalamikiwa kusababisha kupungua kwa mitaji ya wafanyabiashara wanaolipa kodi hiyo.

Masoud alisema jambo hilo linawazimisha kukopa ili kuendelea na uzalishaji.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2014 ambayo ilianza kutumika 2015, wafanyabiashara wanakusanya kodi hiyo kwa niaba ya Serikali na TRA inapaswa kuwarejeshea haraka.

“Madeni hayo yamekuwa makubwa na mzigo kwa Serikali. Kwa viwanda vinne tu Tanga Pharmaceutical Ltd, Allience One Tobacco, Alaf Ltd na Mufundi Paper Mills Ltd vinadai Sh55.5 bilioni,” alisema Masoud.

Alisema Serikali kwa taarifa ambazo zimehakikiwa iangalie namna ya kurejesha fedha hizo kwa wahusika kwa wakati.

Kuhusu TBS, Masoud alisema kamati haijaridhishwa na gharama za ujenzi wa maabara ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ya Sh19.3 bilioni.

Alisema licha ya kuitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya ukaguzi maalumu na kujua iwapo ukaguzi umeshafanyika, imekuwa ikizungushwa kupewa matokeo ya ukaguzi huo.

“Kamati iliendelea na ufuatiliaji mradi wa ujenzi wa jengo la maabara la TBS katika vikao vya Januari ilihoji juu ya hatua iliyofikiwa katika ukaguzi maalumu uliombwa kufanyika na kuarifiwa kuwa umekamilika,” alisema.

Alisema kamati ilijaribu kuomba taarifa iliyotokana na ukaguzi huo kuhusu gharama za mradi , lakini haikufanikiwa jambo linalosababisha sintofahamu kwa kamati.

Pia, kamati hiyo imeishauri Serikali kuwaongezea uwezo watumishi wa TBS kwa kuwawezesha kupata mafunzo yatakayowasaidia kuandaa viwango/vipimo vipya.

ambavyo kwa sasa TBS haina uwezo wa kuvikagua na imekuwa ikiwaelekeza wadau kwenda kupima bidhaa zao nje ya nchi.

Alitaja mfano ni bidhaa za elektroniki hususani simu na televisheni.

Aidha, Makamu Mwenyekiti huyo alisema mifuko mbadala iliyopo sokoni na inayotumika kwa kiasi kikubwa haina ubora jambo linaloleta hasara kwa watumiaji ambapo imekuwa ikichanika na kumwaga bidhaa ziliyobebwa ndani.

“Kamati inaishauri Serikali kwa kushirikiana na TBS kuwasimamia wazalishaji wa mifuko hiyo kuhakikisha wanatumia viwango vilivyopangwa,”alisema.

Alisema pia kwa inayoingia kutoka nje ukaguzi ufanyike na isiyokidhi viwango isiruhusiwe kuingia.

Alitaka Serikali iwasimamie watengenezaji wa mifuko mbadala wapunguze bei iwe yenye uhalisia na ukubwa na uimara wake.