Tahadhari yatolewa matumizi ya dawa za antibiotiki

Muktasari:

  • Matumizi holela ya dawa za antibiotiki (vijiuasumu) kwa binadamu na wanyama umetajwa kusababisha vimelea vya magonjwa ya kuambukiza kujenga usugu.

Dar es Salaam. Matumizi holela ya dawa za antibiotic (vijiuasumu) kwa binadamu na wanyama yametajwa kusababisha vimelea vya magonjwa ya kuambukiza na kujenga usugu.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 15, 2019 katika ufunguzi wa kongamano la siku moja kwa wataalamu ikiwa ni maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya wiki ya kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa za antibiotiki yanayotarajiwa kufanyika kati ya Novemba 18 hai 24, 2019.

Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa wa Wizara ya Afya, Dk Elias kwesi aliyemuwakilisha Waziri, Ummy Mwalimu amesema ili kuepusha usugu wa matumizi ya dawa hizo ni lazima kuhakikisha zinatumika pale zinapohitajika tu.

“Ni vyema tujifunze juu ya usugu wa vimelea dhidi ya vijiuasumu, pia niwakumbushe wananchi umuhimu wa kinga ya maambukizi kwa njia ya kuosha mikono na chanjo,” amesema Dk Kwesi

“Niwaagize watoa dawa kote nchini kuandika dawa kwa kufuata mwongozo wa matibabu wa mwaka 2017 na kutumia majina halisi ya dawa, pia vituo vyote vya huduma ya afya kutekeleza miongozo ya kukinga na kuzuia maambukizi ambayo ni kuhimu sana kwa kuzuia usugu,” amesema

Mtaalamu kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani, Dk Raphael Salla amesema miongoni mwa vitu vinavyochangia usugu wa vimelea ni watu kutomaliza dawa walizoandikiwa na daktari, kutumia dawa zisizo kuwa na ubora au bandia.

“Ni vyema kuzingatia na kumaliza dozi kama ulivyoshauriwa na mtaalamu ili kuweza kupona kabisa, wasitumie dawa bila maelekezo ya daktari na wajitahidi sana kutotumia dawa isivyofaa kwa mfano kumeza dawa zilizotakiwa kutumika kwa kudungwa sindano,” amesema Dk Falla