Tajiri Moshi aunganishwa sakata la shamba la bangi lililokamatwa

Moshi. Wakati raia wa Poland anayetuhumiwa kumiliki shamba la bangi, Damian Sanikowsik akitarajiwa kufikishwa kortini wakati wowote kuanzia leo, mfanyabiashara tajiri wa Moshi ameunganishwa katika tukio hilo.

Naibu Kamishina Jenerali kikosi kazi cha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), James Kaji jana alilithibitishia gazeti hili kuhusu kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, ambaye hakutaka kumtaja jina lake.

Hata hivyo, Mwananchi lilifanikiwa kupata jina la mfanyabiashara huyo ambalo linahifadhiwa kwa sababu za kisheria.

Mfanyabiashara huyo ni mkazi wa mji wa Moshi anayemiliki malori yanayosafirisha mizigo nchini na nchi jirani ya Kenya.

Mfanyabiashara huyo ni wa tano kukamatwa kutokana na sakata hilo la shamba la bangi linalodaiwa kumilikiwa na raia huyo wa Poland.

Raia huyo wa Poland, mkewe pamoja na watu wengine wawili, walikamatwa Februari 8, 2020 na maofisa wa DCEA.

Naibu Kamishina Jenerali wa DCEA, Kaji jana alilithibitishia gazeti hili kuwa mfanyabiashara huyo ni miongoni mwa waliowakamata pamoja na raia huyo wa Poland.

Kaji alieleza kuwa watuhumiwa hao watafikishwa wiki hii mahakamani na inaweza kuwa leo au kesho. “Subirini wiki hii watafikishwa mahakamani na sasa hivi taratibu za kuandaa mashitaka zinaendelea. Mfanyabiashara huyo ni kweli amekamatwa,”alisema.

Wiki iliyopita, Kaji alielezea namna walivyopata taarifa za siri kutoka kwa raia wema na kufanya maofisa wa DCEA kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda kitongoji cha Njiapanda mkoani Kilimanjaro na kumkamata mtuhumiwa.

Kaji alisema ingawa shamba liko Njiapanda ya Himo, lakini nyumbani kwake eneo la Bonite walikuta pia bangi iliyokuwa katika hatua za kusindikwa na nyingine ikiwa tayari imesindikwa.

Naibu Kamishna Jenerali alieleza kuwa huko nyumbani walikuta asali, jam na keki zilizotengenezwa kwa mchanganyiko wa bangi zikiwa tayari kwa ajili ya kuuziwa wateja wa ndani na nje ya nchi.

Majirani wasimulia

Katika hatua nyingine, wananchi wanaoishi jirani na eneo ambalo raia huyo wa Poand anadaiwa kukamatwa, wameeleza namna usiri ulivyotawala.

Wallisema mara zote walimuona mtuhumiwa akiendesha pikipiki au gari aina ya Toyota Rav4 kila alipoingia eneo hilo.

Baadhi ya wananchi wanaoishi kitongoji cha Njiapanda Mashariki jirani na eneo hilo, walisema, hawamfahamu mzungu huyo bali walizoea kumuona akiingia na kutoka tu.

Anna Mrutu alisema raia huyo alinunua eneo hilo mwaka jana na baadaye alijenga ukuta mrefu, na kuweka geti, hali ambayo haikuruhusu kuona kilichoendelea ndani.

“...Sisi hatumfahamu, tumekuwa tukimuona tu akiingia na pikipiki na kutoka na hatukuwahi kufahamu kama kuna chochote kunachofanyika katika shamba hilo,” alisema Anna.

Anna ambaye kama walivyo majirani wengine waliokuwa wakisita kuongelea suala hilo, alisema hawakubaini kilimo hicho kutokana na ukuta mrefu uliozunguka nyumba hiyo hadi siku anakamatwa.

Jirani mwingine, Ismail Mustapha alisema hakuwahi kufahamu shughuli zilizokuwa zikifanyika ndani kutokana na kuzibwa na ukuta mrefu na geti kufungwa muda wote.

“Nimekuwa nikimuona akiingia na kutoka, na si rahisi mtu aliyeko nje kujua kinachofanyika ndani ya ukuta huo, ila juzi ndiyo tulishtuka kuwa alikuwa akiendesha kilimo cha bangi,” alisema Ismail.

Balozi wa eneo hilo, Maro Mmbaga alisema mke wa raia huyo wa Poland, alifika katika eneo hilo mwaka jana, akitafuta eneo la kununua, na baada ya kuliona siku iliyofuata alikwenda na mumewe.

“Baadaye alinipigia mwenye shamba na kunieleza kuwa watu hao wamenunua eneo hilo hivyo ni mali yao, na wenyewe pia wakaja wakajitambulisha kuwa wamemalizana na mwenye shamba,” alisema.

Maro alisema baadaye walianza kujenga ukuta na kuweka geti na kwamba baada ya kumaliza ujenzi hawakuwahi tena kuwa karibu na mwananchi yeyote.

“Baada ya kuweka geti, kilichopo ndani si rahisi mtu afahamu, yeye anakuja asubuhi anaingia na kutoka, wakati mwingine alikuwa haonekani, na hakuna mtu anayefahamu kinachoendelea huko ndani,” alisema.