Takukuru wabaini ubadhilifu wa Sh82 milioni vitambulisho vya wafanyabiashara

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Mtwara imebaini ubadhilifu wa Sh82.7  milioni za mauzo ya vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo kutokana na fedha hizo kutopelekwa benki.

Mtwara. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Mtwara imebaini ubadhilifu wa Sh82.7  milioni za mauzo ya vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo kutokana na fedha hizo kutopelekwa benki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Februari 14, 2020 Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Enock Ngailo amesema waliendesha zoezi la ufuatiliaji wa fedha katika wilaya tatu za Masasi, Tandahimba na Mtwara na kubaini ubadhilifu kwa baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu. Amesema wanaendelea na uchunguzi katika wilaya za Newala na Nanyumbu.

Novemba, 2018 Rais wa Tanzania John Magufuli aliagiza wafanyabiashara wadogo nchini wapewe vitambulisho kwa gharama ya Sh20,000 kila kimoja na wasitozwe kodi au ushuru mwingine wowote kwa mwaka mzima.

Alitoa jumla ya vitambulisho 670,000 kwa kila Mkoa kupewa mgao wa vitambulisho 25,000 ambavyo vingeiwezesha kukusanya Sh500 milioni.

Amesema tangu waanze ufuatiliaji Novemba 25, 2019 hadi Februari  13, 2020 wamefanikiwa kuokoa Sh34.1 milioni  kati ya Sh82.7 milioni  baada ya kuwabana watendaji ambao walizipeleka fedha hizo benki.

“Tumebaini ubadhilifu kwa watendaji wasio waaminifu na katika ufuatiliaji tumebaini ubadhilifu wa Sh82.7 milioni kutoka na mauzo ya vitambulisho vya wajasiriamali pasipo fedha kuwasilishwa benki.”

“Katika ufuatiliaji  tayari zimeokolewa Sh34.1 milioni fedha ambazo hapo awali hazikuwasilishwa benki na zilikuwa mikononi mwa baadhi ya watendaji,” amesema Ngailo.

Ngailo amesema jumla ya vitambulisho 2,430 vya thamani ya Sh48.6 milioni,  fedha zake hazijawasilishwa benki.

“Jumla ya vitambulisho vilivyopokelewa katika wilaya tatu tulizofanya uchunguzi ni 43,000, wilaya ya Mtwara vitambulisho (15,300) Masasi (14,700) na Tandahimba (13,000) kwa maana hiyo wilaya nyingine bado ufuatiliaji unaendelea ili kupata jumla ya vitambulisho  vilivyotolewa,” amesema Ngailo

Kuhusu idadi ya vitambulisho vilivyogaiwa kwa wafanyabiashara  amesema Mtwara (15,175), Masasi (11,662) Tandahimba (11,047)

“Fedha zilizowasilishwa  benki baada ya mauzo ya vitambulisho vya wajasiriamali Mtwara ni  Sh303.5 milioni, Masasi Sh201 milioni na Tandahimba ni Sh 204.5 na jumla ya fedha hizo ni Sh709 milioni ambazo zimewasilishwa benki na vitambulisho zaidi ya  2,430 ambavyo ni  Sh48.6 milioni hizo fedha  hazijulikani zilipo.”

“Jumla ya fedha zote ambazo zinadaiwa hadi sasa ni Sh48.6 milioni  za wilaya tatu. Kimsingi kukosa uaminifu na uadilifu kwa sababu wanathibitisha vitambulisho viliuzwa lakini fedha hawakuwasilisha benki,  inaonekana walitumia kwa matumizi yao wenyewe lakini baada ya uchunguzi tulivyowabana ndio wakazitafuta na kuzipeleka benki lakini bado hawajakamilisha,” amesema Ngailo