Toka-ingia ya Simbachawene katika uwaziri

George Simbachawene.

Dar es Salaam. Kwa George Simbachawene, mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais John Magufuli juzi katika baraza lake la mawaziri, yanaweweza kutafsiriwa kama maji kupwa na kujaa.

Mbunge huyo wa Kibakwe juzi aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, moja ya wizara nyeti na kubwa, akihamishwa kutoka Wizara ya Mazingira na Muungano iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mabadiliko hayo yalitokana na uamuzi wa Rais kutengua uteuzi wa Kangi Lugola, aliyekuwa Mambo ya Ndani na Thonis Andengenye, aliyekuwa kamishna jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutokana na kashfa ya mkataba wa manunuzi ya vifaa vya uokoaji uliokiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma na taratibu za kupitishwa na vyombo stahiki.

Simbachawene amechukua nafasi hiyo ikiwa ni miezi sita tangu arejeshwe ndani ya Baraza la Mawaziri baada ya kuwa nje tangu mwaka 2017 alipolazimika kujiuzulu pia kutokana na kashfa ya mikataba mibovu na uendeshaji wa biashara ya madini.

Shinikizo la kujiuzulu lilitokana na ripoti zilizotolewa Septemba 7, 2017 za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi iliyoonyesha namna Serikali ilivyopoteza trilioni za fedha kutokana na mikataba mibovu, baadhi ikiwa imesainiwa wakati akiwa Waziri wa Madini katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne.

Baada ya kusomwa kwa ripoti hiyo, Rais Magufuli alitaka wote walioguswa kujiweka pembeni ili kupisha uchunguzi na Simbachawene, wakati huo akiwa Waziri wa Tamisemi, aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo.

Kwa hiyo kuanzia Septemba 7, 2017 akawa nje ya Serikali akifanya shughuli zake kama mbunge wa Kibakwe hadi Agosti 28, 2018 alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti kuchukua nafasi ya Hawa Ghasia aliyejizulu.

Akizungumzia kuteuliwa kwake kwenye nafasi hiyo alisema misingi ya uendeshaji wake ipo kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria hivyo atasimamia sheria zote.

“Nilipofika kamati ya bajeti nikaambiwa mwenyekiti na makamu wake wamejiuzulu basi nikapata interest. Ngoja nigombee na wajumbe wamenipitisha kwa kauli moja nataka niseme tu kwamba kamati ile nafahamu ni kamati muhimu katika Bunge na Serikali. Tutafanya majukumu yetu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo lakini pia kwa maslahi ya Taifa,” alisema Simbachawene wakati huo.

Nafasi ya uenyekiti wa kamati hiyo aliendelea nayo hadi Julai 21, 2019 aliporejeshwa barazani kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kuchukua nafasi ya January Makamba, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Tangu aliporudi serikalini, Simbachawene amekuwa tofauti, Si waziri anayeonekana mara kwa mara kwenye vyombo vya habari.

Miezi sita baada ya kuingia wizara hiyo, Simbachawene amejikuta akiaminiwa zaidi na kuhamishiwa wizara nyeti ya Mambo ya Ndani ya Nchi, akiwa waziri wa tatu tangu Rais Magufuli ateue baraza lake la kwanza mwaka 2015.

Simbachawene anaingia kukiwa na mambo mengi ya kuyafanyia kazi katioka wizara hiyo ambayo Rais Magufuli amesema ndiyo ambayo imekuwa ikimtesa.

Mikataba ni moja ya mambo ambayo yamekuwa machungu katika wizara hiyo na yamewasumbua mawaziri wengine kadhaa waliopitia wizara hiyo na kuwafanya kudumu kwa miaka michache kabla ya kujiuzulu au kuondolewa.