Trump: Democrats ina wingi kura za kuning’oa lakini...

Muktasari:

Madai ya kutaka mshindani wake kisiasa achunguzwe na Ukraine na China yazidi kupasua anga.

Washington. Rais Donald Trump amesema Chama cha upinzani cha Democrats kina wingi wa kura za kumwondoa madarakani, lakini Spika wa Bunge, Nancy Pelosi aliahirisha kura hizo ili kuanzisha uchunguzi wa geresha wa kumtimua urais.

“Wamepoka haki zetu,” Trump alisema Ijumaa alipozungumza na wanahabari wakati akimaliza juma ambalo taarifa nyingi kuhusu utawala wake na Ukraine zilikuwa zinaibuka kila siku.

“Wote wameshapangwa. Kwa sababu hata kama wengi wao hawataki kupiga kura ya kuniondoa, hawana la kufanya. Wanalazimika kufuata kile ambacho uongozi wao unataka. Na baada ya hapo tutakwenda kwenye Seneti na tutashinda,” alisema Trump.

Bunge la Marekani la Conress lina wajumbe wengi wa Democratic kuliko wa chama tawala cha repumlican lakini Bunge dogo la seneti lina wajumbe wengi wa chama tawala kuliko wapinzani wa Democratic.

Lakini wakati Trump akitambia ‘mshikamano ulipo katika chama chake cha Republican, kwamba kitamwokoa katika hatia hiyo, baadhi ya wanachama wa chama hicho nao wamemjia juu.

Wajumbe wawili wa seneti na ofisa mmoja wa zamani wa Republican wameeleza kutofurahishwa na juhudi za Trump kushawishi Serikali za mataifa ya kigeni kumchunguza Joe Biden, makamu wa zamani wa rais ambaye anawania uteuzi wa Democrats kugombea urais.

Katika tukio jingine, Mkuu wa makachero, Michael Atkinson Ijumaa alikutana na wabunge kujadili malalamiko ya ‘mfichua taarifa za siri’ kuhusu Trump kutumia vibaya madaraka.

Atkinson ambaye ni mteule wa Trump, awali alisema mtoa taarifa ‘anaonekana naaminika’ hivyo malalamiko yake yanafaa kufanyiwa kazi haraka na Bunge.

Licha ya madai ya Trump, kuwa Biden alihusika na rushwa na kuitaka Ukraine imchunguze, nyaraka ambazo The Washington Post imeziona zinaeleza kuwa Kurt Volker, mwanadiplomasia maalumu wa zamani wa Marekani nchini Ukraine ametoa maelezo ya kumtetea Biden.

Hatua hiyo inazima tuhuma za Trump kwa makamu huyo wa rais wa zamani kuhusu ufisadi.

“Namfahamu (Biden) kama mtu mwadilifu na anayeipenda nchi yetu Volker alisema katika kiapo chake Alhamisi iliyopita.

Ijumaa, Trump aliendelea kuweka msimamo wake na kujiweka kama mtu anayeonewa na Democrats. “Hatukutendewa haki kabisa, tofauti kabisa na mtu mwingine yeyote,” alisema.

Trump alisema ataeleza kila kitu katika barua kwa Spika Pelosi, ambaye wana Republican wanazidi kumshutumu kwa kuharibu utaratibu wa kawaida wa kumwondoa Rais madarakani, kwa kutoitisha kura ya wazi ndani ya Bunge badala yake akaamuru kufanya uchunguzi.

Madai hayo ya utaratibu wa kura ya kutokuwa na imani na Rais, pia yamekuwa sehemu ya mjadala, hasa kwa wana Republican wanapozungumzia mchakato wa kumwengua Trump madarakani, baadhi yao wakitetea wazi tabia yake, hasa kauli yake kuwa anayo haki kuitaka nchi ya kigeni kumchunguza mshindani wake.

Wakati huo, wajumbe wa Democrats wamezama zaidi katika uchunguzi, wakiwahoji maofisa mbalimbali wa serikali ya Trump na kutoa hati za kutaka maelezo sehemu ya uchunguzi huo.

Ijumaa kamati tatu za Bunge zilitoa hati ya kutaka nyaraka kadhaa kutoka Ikulu ya White House na mojawapo imemwandikia makamu wa Rais, Mike Pence, kuwasilisha zinazohusiana na mazungumzo yake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Barua hiyo ilimtaka Pence kuwasilisha nyaraka hizo Oktoba 15 akieleza jinsi alivyohusika katika juhudi za ikulu kumshinikiza Zelensky kufanya kumchunguza mpinzani wa Trump.

Pence alikutana na Zelensky mwezi uliopita nchini Poland wakati Marekani ilikuwa inashikilia msaada wa dola 400 milioni ulioidhinishwa kwa ajili ya Ukraine. Ofisi ya Pence imekataa madai hayo ikisema hayana uzito.

“Ofisi ya Makamu wa Rais imeipokea barua baada ya kuwa imetolewa kwenye vyombo vya habari na imetumwa kwa ofisi ya mwanasheria kutafuta majibu,” alisema Katie Waldman, msemaji wa ofisi ya makamu wa Rais. “Kiuhalisia, haionekani kama madai mazito, bali jaribio jingine la upande mmoja la Wademocratis ambao hawawezi kufanya lolote isipokuwa kuuvuta umma.

Democrats inachunguza iwapo Trump au watu wengine walihusisha kutolewa kwa msaada na mambo ya Rais wao la kutaka Ukraine imchunguze Biden.

Akiwasilia kwa simu na Zelensky mwezi Julai, Trump alishinikiza wapelelezi wa Ukraine kufanya kazi na Mwanasheria mkuu wa Marekani, William Barr na mwanasheria wake binafsi, Rudy Giuliani katika uchunguzi wa tuhuma za rushwa dhidi ya Biden na mwanaye Hunter.

Hunter alifanya kazi kwa miaka mitano katika bodi ya Burisma, kampuni kubwa binafsi ya gesi ya Ukraine, ambayo mmiliki wake alichunguzwa na wapelelezi wa Ukraine kwa matumizi mabaya ya madaraka na kujitajirisha isivyo halali.

Hata hivyo, Hunter Biden hakutuhumiwa kwa kosa lolote katika uchunguzi huo. Akiwa Makamu wa Rais katika serikali ya Clinton, Joe Biden aliishinikiza Ukraine mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin ambaye Biden na maofisa wengine wa magharibi walisema hakuwa anaendesha ipasavyo mashauri ya ufisadi.

Wakati huo, uchunguzi dhidi ya Burisma ulikuwa hauendelei kwa mujibu wa maofisa wa zamani wa Ukraine na Marekani.

Wajumbe wa Republican wanapambana kutafuta utetezi wa Trump kutokana na taarifa za “mtoa taarifa za siri” zilizovuja wiki iliyopita.

Mtoa taarifa huyo alisema Trump alishinikiza Serikali ya Ukraine kuchunguza mshindani wake kisiasa, madai ambayo yamethibitika baada ya Bunge kuanza uchunguzi wamepata ujumbe wa maandishi na nyaraka za ndani pamoja na kiapo kutoka katika utawala wa Trump.