Uchaguzi Serikali za Mitaa uliyotonesha kidonda cha siasa Tanzania mwaka 2019

Mwaka 2019 unakwisha ukiacha alama kubwa ya matukio ya kisiasa yanayoashiria sura mpya ya mwaka 2020.

Tukio kubwa lililoacha alama isiyofutika katika siasa za Tanzania ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019, ukisusiwa na baadhi ya vyama vya siasa huko CCM ikijitwalia ushindi mnono.

CCM ilishinda vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, mitaa 4,263 sawa na asilimia 100 na vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4.

Matokeo haya yalitarajiwa kwa sababu baadhi ya vyama vya upinzani vilijitoa kwenye uchaguzi huo vikieleza kuona utata mwingi na wagombea wake karibu wote kuenguliwa.

Vyama vilivyojitoa ambavyo pia ndivyo vilikuwa vimesimamisha wagombea, ni Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na ACT-Wazalendo. Vingine ni Chaumma, UPDP na CCK.

Tangu awali wakati wa kuandaa kanuni za uchaguzi huo vyama hivyo zililalamika kutoshirikishwa kikamilifu, lakini baadaye kanuni hizo zilipitishwa, huku Serikali ikisisitiza kushirikisha makundi yote.

Vyama hivyo licha ya malalamiko viliwahamasisha wanachama wao wajiandikishe kwenye daftari la wakaazi kwa ajili ya uchaguzi huo.

Ulipofika wakati wa uteuzi wa wagombea ndipo utata ulipoongezeka, kwani wagombea wengi wa vyama vya upinzani walienguliwa kwa sababu mbalimbali, lakini wagombea wa CCM hawakuguswa.

Hapo ndipo vyama hivyo zilianza kujitoa kimoja baada ya kingine. Kitendo cha vyama hivyo kujitoa kiliishtua Serikali pengine hata CCM yenyewe.

CCM ilitetea hali hiyo na katibu wake wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema chama hicho kilituma wanasheria nchi nzima kuwasaidia wagombea wake kujaza fomu zao na ndiyo maana hazikuwa na makosa kwa asilimia 100.

Waziri mwenye dhamana, Selemani Jafo alitoa kauli mbalimbali za kuhalalisha hali hiyo, lakini maelezo yake hayakuwashawishi wagombea wa vyama vilivyojitoa.

Matokeo yake CCM ilijikuta ikitawala kwenye uchaguzi huo hali iliyofanya wagombea wake wapite bila kupingwa.

Mbali na vyama vya upinzani, mabalozi wa Marekani na Uingereza nchini Tanzania walielezea kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi huo huku baadhi ya vyama vikielekeza wafuasi wake kutoshirikiana na waliopita bila kuchaguliwa.

Uchaguzi huo umeingia orodha ya mambo ambayo yamekuwa mwiba kwa upinzani tangu mwaka 2015, hali iliyosababisha baadhi yao kusalimu amri kutokana na mazingira magumu ya kufanya siasa huku mikutano ya hadhara ikiwa imezuiliwa na hali ngumu katika Bunge.

Yaliyomkuta Sumaye

Mwaka 2019 pia umekuwa mchungu kwa Frederick Sumaye, waziri Mkuu mstaafu aliyekuwa kada wa Chadema kabla ya kujitoa baada ya kuangushwa katika uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa Kanda ya Pwani.

Sumaye alijiunga na Chadema Agosti 22, 2015 wakati ambao tayari Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye naye alitoka CCM alishaandaliwa kugombea urais kupitia chama hicho.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 ambao CCM ilishinda, Chadema, kama vyama vingine vya upinzani, ilianza kupata misukosuko mingi, ikiwa pamoja na mikutano ya hadhara na maandamano kupigwa marufuku na hivyo kuweka mazingira magumu ya ufanyaji siasa kwa kambi hiyo, lakini Sumaye aliendelea kusimama imara.

Hata hivyo, mapenzi yake kwa Chadema yalitumbukia nyongo hivi karibuni wakati chama hicho kikiwa kwenye uchaguzi wa ndani na yeye akajitosa kugombea nafasi mbili; kwanza kutetea uenyekiti wake wa Kanda ya Pwani na pia alichukua fomu ya kugombea uenyekiti wa Taifa.

Mbali na Sumaye, pia mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe alitangaza kugombea nafasi hiyo ya juu.

Katika uchaguzi wa kanda ya Pwani uliofanyika Novemba 28, 2019 Sumaye aliyekuwa akigombea peke yake alipigiwa kura 48 za hapana na 28 za ndiyo, hivyo kuikosa nafasi hiyo.

Kutochaguliwa kwa Sumaye katika nafasi hiyo kulizua maswali mengi na katika kuonyesha hasira zake, Desemba 4, Sumaye alitangaza kujitoa Chadema, huku akikitupia lawama chama hicho kutomtendea haki katika uchaguzi huo.

Chadema yaja upya

Mwaka 2019 umefungwa kwa Chadema kupata safu mpya ya uongozi tangu wa ngazi za msingi hadi wa kitaifa.

Katika uchaguzi wa nafasi za kitaifa, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe hakuwa na upinzani mkali dhidi ya Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe, kwani alimbwaga kwa ushindi wa asilimia 93.5 dhidi ya asilimia 6.2 alizopata mpinzani wake.

Akitangaza safu yake mpya ya sekretarieti, Mbowe alimweka pembeni Dk Vincent Mashinji aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho na nafasi yake kuchukuliwa na Mbunge wa Kibamba, John Manyika.

Mbali na Mnyika, Mbowe pia alimteua Singo Benson Kigaila kuwa Naibu Katibu mkuu Bara akichukua nafasi iliyoachwa na Mnyika huku nafasi ya Salum Mwalimu akiendelea na nafasi yake ya Naibu katibu mkuu Zanzibar.

Mbali na uteuzi huo, Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amechaguliwa na mkutano huo kuwa Makamu Mwenyekiti Bara, huku upande wa Zanzibar nafasi hiyo imeendelea kushikiliwa na Issa Mohamed Issa.

Akizungumzia uteuzi alioufanya wa safu yake ya uongozi mbele ya mkutano wa Baraza kuu, Mbowe alisema umebaki muda mfupi kuelekea kwenye uchaguzi mkuu hivyo timu yake haitakuwa na muda wa kupoteza.

“Tuna kipindi kifupi sana kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, hakuna kulala, tutafanya kazi usiku na mchana. Viongozi tutasumbuana kwelikweli. Tunahitaji kushinda dola siyo kushiriki uchaguzi,” alisema Mbowe.

Licha ya mabadiliko ya siasa yanayojaribu kufanywa na vyama vya upinzani, bado vyama hivyo vina changamoto ya kushinda uchaguzi kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hali ambayo wanasema inahitaji Tume Huru ya Uchaguzi ili kuweka mfumo sawa wa ushindani.