Ujenzi nyumba za askari Magereza Ukonga wakamilika

Muktasari:

Ujenzi wa nyumba za askari  wa Jeshi la Magereza eneo la Ukonga nchini Tanzania umekamilika na muda wowote kuanzia sasa zitaanza kutumika.

 

Dar es Salaam. Ujenzi wa nyumba za askari  wa Jeshi la Magereza eneo la Ukonga nchini Tanzania umekamilika na muda wowote kuanzia sasa zitaanza kutumika.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Charles Mbuge ameeleza hayo leo Jumanne Novemba 12, 2019 alipotembelea mradi huo na kuridhishwa na namna kazi inavyofanyika.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,  Brigedia Jenerali Mbuge amesema kazi iliyofanywa na JKT imedhihirisha kuwa jeshi halishindwi.

“Machi 16, 2019 wakati nakabidhiwa mradi huu nilisema Jeshi halishindwi na hilo limedhihirika. Kazi imefanyika kwa ubora na niko tayari kumuita mkuu wa majeshi kuona ili amkabidhi Rais (John Magufuli).”

“Kazi imefanywa kwa umahiri mkubwa na vijana wa JKT  tumeona faida yake, wamekuwa vijana wazalendo tuna uhakika nchi imeongeza idadi ya mafundi,” amesema Brigedia Jenerali Mbuge

Kukamilika kwa ujenzi huo kutapunguza changamoto ya makazi kwa askari 172.