Ukawa giza nene uchaguzi 2020

Dar es Salaam. Matukio ya hivi karibuni yanayohusisha viongozi wakuu wa vyama vya upinzani nchini, yameibua wasiwasi iwapo vyama hivyo vitaweza kuwa na nguvu ya pamoja iliyoweka msisimko katika uchaguzi mkuu wa 2015; umoja uliopachikwa jina la Ukawa.

Takriban vyama vyote vinaonyesha kuwa tayari kushirikina na vingine kuendeleza mafanikio ya mwaka 2015 wakati mgombea urais wa upinzani alipopata kura milioni 6.07 na kuzidiwa kwa tofauti ndogo na mshindi kutoka chama tawala.

“Kwa msimamo wa ACT-Wazalendo, sisi tunaamini tunahitaji ushirikiano,” alisema mshauri mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad akijibu swali kama wanaweza kuwa na ‘Ukawa’ nyingine mwaka huu wakati alipohojiwa na Mwananchi mapema wiki hii.

“Hatuwezi kwenda katika uchaguzi huu (tukiwa) chama kimojakimoja. Na jambo dogo tu uangalie, uchaguzi mwaka 2015 kuna maeneo tumepoteza kwa kura chache sana kwa sababu kura za wapinzani ziligawanyika.

“Ingekuwa wapinzani waliungana katika maeneo yale, CCM ingepoteza. Kwa hiyo nasema, sisi tunaamini suala la vyama vile ambavyo viko serious kuungana au kushirikiana, ni jambo ambalo ni muhimu sana, sana. Huo ndio msimamo wetu sisi. Tunahitaji kufanya kazi pamoja.”

Wakati huo Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF viliamua kusimama pamoja katika uchaguzi kwa kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kukubaliana wagombea katika majimbo na kata.

Hamasa ya umoja huo iliibuka katika Bunge la Katiba ambako wajumbe, wengi wakiwa wa vyama vya upinzani, walisusia vikao kwa madai kuwa CCM imegeuza Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa katika chombo hicho na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.

Wajumbe hao, ambao wengi walikuwa wabunge, walisema Rasimu ya Katiba ndiyo iliyobeba maoni na utashi wa wananchi na hivyo kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), chombo ambacho waliingia nacho hadi katika Uchaguzi Mkuu.

Lakini mazingira hayo hayaonekana katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mwaka huu, huku kukiwa na matukio kadhaa yaliyotokea tangu mwaka 2017 yanayotishia uwezekano wa vyama hivyo kuunganisha nguvu.

Pia Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ina mtazamo tofauti na ile ya mtangulizi wake, Jakaya Kikwete katika masula ya demokrasia na uhuru wa vyama, hali ambayo imesababisha manung’uniko kutoka kwa wapinzani.

Akizungumzia vyama kuungana, Mhadhiri wa elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa alisema kuna uwezekano mkubwa muungano huo ukashindikana kutokana na sababu kadhaa.

“Huo muungano hatuwezi kusema asilimia 100 hautakuwepo, lakini kwa asilimia kubwa hauonekani kama utakuwapo,” alisema.

“Si kwa matukio ya sasa hivi, bali ni kwa matukio ya tangu wakati ule wa uchaguzi na baada yake, ushirikiano wao ulikosa mwelekeo.”

Hata hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Iringa), alisema kwa mtazamo wake ni vyema vyama hivyo vikaungana.

“Kwa mazingira ya siasa ya Tanzania ni vizuri hasa kwa uchaguzi wa mwaka huu vyama vya siasa viungane. Hata kama havitashinda, lakini walau vionyeshe upizani,” alisema Profesa Mpangala.

Mwaka 2015, Ukawa iliongezewa nguvu na ujio wa Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani ambaye aliihama CCM na kujiunga na upinzani baada ya chama hicho tawala kuengua jina lake miongoni mwa makada walioomba kupitishwa kugombea urais.

Ingawa hatua hiyo ilisababisha mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujivua uongozi, sawa na Dk Willbroad Slaa kujivua ukatibu mkuu Chadema, vyama hivyo vinne vilisimama na kupambana katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Lowassa alifuatiwa na waziri mkuu mwingine wa zamani, Frederick Sumaye, mawaziri wa zamani, wenyeviti wa mikoa, wabunge, madiwani na wanachama walioongeza nguvu kwa wapinzani.

Hata hivyo, baada ya uchaguzi huo CUF iliingia katika mgogoro baada ya Profesa Lipumba kulazimisha kurejea madarakani na hatimaye katibu wake mkuu, Maalim Seif na wenzake kujiondoa na kujiunga na ACT Wazalendo, ambayo ilikataa Ukawa mwaka 2015.

Pia, hamahama ya wabunge, madiwani na viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani kurejea CCM, pia ilionekana kuyumbisha upinzani.

Lakini hatua ya hivi karibuni ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kujiunga na NCCR-Mageuzi imeleta sura mpya katika siasa na inaweza kuwa moja ya sababu zinazoweza kufuta uwezekano wa vyama hivyo kuunganisha nguvu.

“Ukawa haukuwa umoja uliosajiliwa kisheria,” alisema makamu mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Profesa Bernadeta Killian.

“Tukumbuke pia vyama vyote vya siasa vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na kila chama kinapambana kushika dola. Kwa hiyo hapo ndipo kuna changamoto ya kuendeleza muungano ambao haupo kisheria wala kikanuni.”

Muungano mpya?

Lakini Profesa Mpangala anaona kuna dalili za kuungana.

“Kuna dalili za kuungana kwa kuwa vyama hivyo vilishikamana kususia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019,” alisema msomi huyo.

Alikuwa akirejea uamuzi wa vyama saba-- Chadema, ACT Wazalendo, CUF, NCCR Mageuzi, UPDP, Chaumma na Chama cha Kijamii-- kususia uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019.

Na Maalim Seif alizungumzia hilo katika mahojiano na Mwananchi.

“Sisi, we have tried to reach out kwa wenzetu (tumejaribu kuwasiliana na wengine),” alisema Maalim Seif alipoulizwa kama kuna mikakati yoyote imefanyika ya kuanzisha muungano.

“Na ni mapema mno kusema kuwa tumefikia hatua gani.. Lakini tumereach out na response (majibu) tuliyopata si mbaya. Kwa hiyo ni matumiani yangu, na bila kupoteza muda, tukae tuangalie ni jinsi gani tunaweza kupata ushirikiano ambao kila mmoja ataridhika.”

Wakati mwaka 2015 vyama hivyo viliunganishwa na Katiba mpya, katika siku za karibuni vinaonekana kuwa na ajenda zinazoshabihiana; tume huru ya uchaguzi na kupatikana kwa Katiba mpya. Hata hivyo licha ya ajenda hizo, kuna mambo yanayoweka shakani dhamira hiyo.

Wapo wanaohoji iwapo Profesa Lipumba anaweza kufanya kazi na aliyekuwa katibu mkuu wake Maalim Seif au iwapo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anaweza kufanya kazi na kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alikuwa mbunge wa Chadema hadi mwaka 2010.

Zitto aliondolewa Chadema baada ya hukumu ya kesi ya kupinga kufukuzwa chama hicho, kutokubali hoja zake.

Alikuwa akituhumiwa kwa usaliti.

Hata hivyo, tayari vyama hivyo vilishatoa Azimio la Zanzibar ambalo linataka waungane kupambana na CCM.

Pia Februari 25, baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani vilionyesha utayari wa kushirikina lakini vikaweka bayana kwamba Chadema ndicho chenye dhamana ya kuvikutanisha vyama vingine kwa kuwa ndicho chama kikuu cha upinzani.

Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema chama hicho kinathamini sana suala hilo na kwamba wameishaunda kamati ambayo yeye ni katibu wake kwa ajili ya ushirikiano na vyama vingine.

“Hatua ya sasa, tushirikiane kudai tume huru ili tukipata tume huru ya uchaguzi tutajua hata tunapoingia kwenye uchaguzi tuna uhakika tutashinda,” alisema Mrema.

Wapinzani kuitwa Ikulu

Wakati hayo yakiendelea, suala la baadhi ya viongozi kuitwa Ikulu kwa mazungumzo binafsi linaweza pia kuwa kikwazo kwa umoja huo.

Mbatia, Profesa Lipumba na Maalim Seif wameshaitwa mara mbili tangu mwaka 2015 kuzungumza na Rais Magufuli, lakini walichojadili hakikuwekwa bayana kwa mapana.

Hata hivyo, Maalim Seif aliiambia Mwananchi kuwa yeye ndiye aliyeandika barua mara tatu kuomba kukutana na Rais.

Safari hizo za Ikulu zimekuwa zikizua minong’ono katika vyama na wiki hii, baadhi ikitokana na kutowekwa bayana kwa mazungumzo na kitendo cha wiki hii cha Mbatia kueleza kuwa ataanza ziara ya nchi nzima siku moja baada ya mazungumzo na Rais, kuonekana kama kilitokana na ruhusa ya kipekee.

Hata hivyo, Mbatia anafanya mikutano ya ndani.

Mbowe aliliambia gazeti hili wiki hii kuwa iwapo ataitwa Ikulu, atataka aende na viongozi wenzake na kwamba Rais pia awe na wasaidizi wake.