Ukiingia Morogoro jihadhari, si salama

Morogoro. Maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika manispaa ya Morogoro yamefikia asilimia 4.5 kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kwenye vituo vya afya na huduma ya mkoba.

Hali inaifanya halmashauri ya manispaa hiyo kuongeza kasi ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU.

Taarifa hizo zilitolewa juzi na mratibu wa Ukimwi wa manispaa hiyo, Pendo Elias kwenye kikao cha maandalizi ya Siku ya Ukimwi Duniani inayoadhimishwa Desemba mosi kila mwaka.

Katika kikao hicho kilichokutanisha wadau mbalimbali ikiwamo asasi za kupambana na maambukizi ya Ukimwi, Pendo alisema maadhimisho ya mwaka huu mbali ya kutoa huduma ya kupima virusi vya Ukimwi, kutakuwa na huduma ya upimaji saratani ya shindo ya kizazi, kisukari na shinikizo la damu.

Pia, Pendo alisema elimu itatolewa kwa makundi tofauti ya watu wakiwamo vijana ambao ndiyo kundi kubwa linaloonekana kuathirika, watu wanaojihusisha na biashara ya ngono na wanafunzi hasa wa vyuo kuhusu madhara ya Ukimwi na unyanyapaa.

Awali, akifungua kikao hicho kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, Michael Waluse alisema takwimu za maambukizi ya Ukimwi za manispaa hazipendezi hivyo lazima kila mdau aweke nguvu ya kupambana na maambukizi mapya badala ya kuachia kazi hiyo halmashauri.

Waluse alisema lengo la Rais John Magufuli la kuwa na Tanzania ya viwanda haliwezi kufanikiwa kama wananchi hususan vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa haitakuwa na afya bora na matumaini ya kuishi.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni Jamii ni chachu ya mabadiliko tuungane kutokomeza maambukizi ya Ukimwi, hivyo kila mdau anapaswa kushiriki katika mapambano hayo.

Machi 6, 2018 Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TacAids) ilitoa ripoti mpya ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini ikieleza watu 225 huambukizwa kila siku.

Ripoti hiyo inaonyesha watu 6,750 huambukizwa kila mwezi huku 81,000 huambukizwa kwa wa mwaka.