Ukomo wa urais ulivyozivuruga nchi za Afrika

Wakati ukomo wa urais umechukua sehemu ya mijadala hapa nchini katika maeneo mengine hasa nchi za Afrika suala hilo limezua misukosuko, machafuko na kutoelewana.

Katika baadhi ya nchi limesababisha mauaji, limechochea mapinduzi, upendeleo na kutoaminiana.

Kwa hapa nchini aliyeibua mjadala huo ni Juma Nkamia, mbunge Chemba akijenga hoja ya gharama za uchaguzi na baadaye kuendelezwa na watu wengine wa kada mbalimbali akiwamo aliyekuwa Mbunge wa Korogwe, Marehemu Stephen Ngonyani wakitaka Rais aongezewe muda kwa sababu amefanya kazi nzuri.

Hivi karibuni limeibuka kwa sura mpya katika Mahakama Kuu ambako mkulima mmoja amefungua kesi akitaka ukomo wa urais uondolewe.

Hata hivyo, Rais John Magufuli ameshasema kuwa hana mpango wa kuongeza muda na ataondoka madarakani baada ya muda wake kuisha.

Uzoefu Afrika

Suala la marais wa Afrika kung’ang’ania madarakani si geni Afrika, kuna mifano kadhaa ya marais waliotekeleza suala hilo na kisha kuondolewa kwa aibu na wengine kusalia madarakani kwa mkono wa chuma.

Viongozi hao wakishaingia madarakani hushinikiza kubadilisha katiba za nchi zao ili waendelee kusalia madarakani, hali ambayo katika baadhi ya nchi imeibua migogoro na machafuko.

Miongoni mwa waliokuwa viongozi ving’ang’anizi ni aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe (marehemu) aliyekaa madarakani kwa miaka 37, hata alipofukuzwa ndani ya chama chake Zanu-PF, aligoma kung’atuka.

Mugabe aliondolewa madarakani kwa nguvu na jeshi, baada ya kuzuiliwa nyumbani kwake kwa siku kadhaa.

Kwa uamuzi huo, mazuri yote aliyoyafanya wakati wa uongozi wake yameingia dosari.

Ukiacha mfano, yupo Yoweri Museveni, Rais wa Uganda ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1986.

Museveni (74) ameshadumu madarakani kwa miongo mitatu na sasa Katiba ya nchi hiyo imebadilishwa ili kuondoa ukomo wa umri wa kuwania urais, lengo likiwa kumruhusu agombee tena 2021. Tayari chama chake kimeshampitisha kuwania tena.

Hivi karibuni Omar Al-Bashir wa Sudan aliyeingia madarakani mwaka 1989 naye aling’olewa na jeshi na anashtakiwa kwa kusababisha mauaji katika harakati za kulinda madaraka yake.

Rais mwingine aliyedumu muda mrefu madarakani ni José Eduardo dos Santos wa Angola, akiwa ni wa tatu kwa waliotawala kwa muda mrefu zaidi Afrika baada ya Paul Biya wa Cameroon na Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea aliyekuwa madarakani kwa miaka 40 sasa.

Dos Santos aliyekaa madarakani kwa karibu miongo minne, wakati anaondoka alisema hajutii alichokifanya katika utawala wake. Hakuwania tena urais kwenye uchaguzi wa Agosti 2017 na alimkabidhi madaraka waziri wake wa ulinzi, Joan Lourenco.

Aliyekuwa Rais wa Burkina Faso, Christian Kabore alitawala kwa miaka 27 hadi alipoondolewa kwa mapinduzi ya kijeshi.

Nchi hiyo tangu ijinyakulie uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960, asilimia kubwa ya viongozi wake wamekuwa wakichukua uongozi kwa mtutu wa bunduki.

Katika orodha hiyo ya ‘waliodumu’ madarakani huwezi kumwacha Teodoro Nguema wa Equatorial Guinea ambaye mpaka sasa ana miaka 40.

Rais huyo aliingia madarakani mwaka 1979 kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Amenusurika jaribio la mapinduzi lililofanywa na mamluki wa kigeni mwaka wa 2004, anatajwa kumuandaa mwanaye wa kiume, Teodorin kumrithi atakapoacha urais wa nchi hiyo.

Viongozi wengine ni Yahya Jammeh aliyekuwa Rais wa Gambia alitwaa madaraka kwa mapinduzi ya umwagaji damu mwaka 1994.

Bila kutarajia Jammeh, ambaye alikuwa kiongozi wa tisa katika orodha ya waliokaa muda mrefu madarakani Afrika baada ya kuongoza kwa miaka 22, alishindwa vibaya kwenye uchaguzi na akakiri kushindwa kwa mgombea ambaye hakuwa maarufu, Adama Barrow. Lakini baadaye akabadili msimamo hadi.

Jammeh alizamika kuachia madaraka baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) kutuma majeshi yake Gambia kumshurutisha akubali Barrow aapishwe. Jammeh alipewa hifadhi ya kisiasa katik nchi ya Equatorial Guinea.

Wengine walikaa madarakani hadi walipoonyeshwa mlango wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya Kiarabu yaliyoibuka mwaka 2011 yaliyowang’oa Rais wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali; Rais wa Misri, Hosni Mubarak; na Kiongozi wa Libya, Muammar Gadaffi.

Ben Ali aliingia madarakani mwaka 1987 baada ya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na alikimbilia Saudi Arabia lakini alihukumiwa jela miaka 35 hadi kifo chake hivi karibuni.

Mubarak aliyejiuzulu baada ya maandamano ya siku 30, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa uhalifu uliotendeka kipindi hicho cha maandamano. Mahakama ilimfutia mashtaka na kuachia huru.

Gadaffi aliyeingia madarakani mwaka 1969 aliogopwa, kuheshimika na kuabudiwa. Vuguvugu lilipoanza Februari 2011 aliapa kuwasaka waasi lakini alitimuliwa Agosti na akauawa.

Viongozi wengine walioondolewa madarakani baada ya kukaa muda mrefu Laurent Gbagbo wa Ivory Coast (2011); na Amadou Toumani Toure wa Mali (2012); Jenerali Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika Kati (2013); na Blaise Compaore wa Burkina Fasso (2014).

Vituko vyao

Baada ya kukaa madarakani muda mrefu huchukiwa sana lakini wao hulazimisha kuonekana wanapendwa na hivyo uhuru wa watu wa maoni na kisiasa hubanwa na huteua watu watakaowasaidia kudumu madarakani.

Baada ya kuchaguliwa katika muhula wa tano kwenye uchaguzi wa mwaka 2016, Rais Museveni alimteua mke wake, Janet kuwa waziri wa elimu na michezo.

Pia, alimteua mwanaye, Muhoozi Kainerugaba, kwenye cheo cha juu jeshini (jenerali) na kuwa mkuu wa kikosi maalumu kinachosimamia ulinzi wa rais na kulinda maeneo muhimu kwa serikali Uganda.

Hali hiyo ilitafsiriwa na wakosoaji wake kama upendeleo wa kifamilia.

Mwaka 2017, Rais Mugabe naye alimteua binti yake kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya benki mpya nchini humo, ikiwa ni mara ya pili kupata uteuzi ndani ya kipindi cha wiki moja.

Awali, binti wa Mugabe, Bona aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Sensa, jambo lililosababisha mashambulizi dhidi ya Rais kuwa amempendelea na anataka kuiweka familia yake katika nafasi nyeti.

Kutokana na hali hiyo wakosoaji wanasema tabia ya viongozi hao kung’ang’ania madarakani imekuwa ikichangia kuwapo uhasama kati ya viongozi na wananchi.

Wanasema viongozi wanapaswa kuheshimu matakwa ya kikatiba ya nchi zao na kuongoza kwa muda unaokubalika na kuachia wengine kwa amani.

Kauli za wanasiasa

Akizungumzia suala hilo, Ado Shaibu, katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT Wazalendo, anasema uongozi ni lazima uwe na mipaka ya madaraka pamoja na ukomo wa kuongoza.

Anasema kiongozi akikaa madarakani kwa muda mrefu, ataongoza kwa mazoea na matokeo yake kukosekana tija.

Anasema hali hiyo ndiyo imeifanya ACT Wazalendo kimeiomba Mahakama Kuu kuingia katika kesi ya mkulima, Dezydelius Mgoya anayeomba ukomo wa urais kuondolewa.

Shaibu anatoa mfano kuwa Rais wa Uganda alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza aliongoza vizuri, lakini ulipoondolewa ukomo wa uongozi, anafanya vibaya.

“Museveni wa miaka 80 alipoingia madarakani na wa sasa ni tofauti. Mugabe naye alipoingia madarakani alikuwa kipenzi cha watu, lakini alivyoendelea kukaa madarakani alipoteza ubora wake,” anasema.

“Uongozi sio mtu mmoja. Sisi ni binadamu tunaweza kuondoka kwa sababu za kifo au maradhi. Hii ya kung’ang’ania madaraka haina afya,” anasema.

Anasema nchi ikiwa na taasisi imara, kila uongozi unapoingia madarakani utaendeleza mambo yaliyokuwapo na kutolea mfano Rais Magufuli ameendeleza miradi iliyoachwa na utawala wa awamu ya nne.

Lakini, John Mrema, mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, anasema suala la viongozi kung’ang’ania madarakani lina athari kubwa.

“Tumeona hali ilivyokuwa Burundi kutokana na kiongozi kung’ang’ania madarakani na Rwanda hali ilikuwa hivyo mpaka walipopitisha kuwa na urais wa milele,” anasema Mrema.

Anasema hali hiyo inachangia kuwapo mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na kutolea mfano hali iliyokuwa nchini Congo, wakati Joseph Kabila alipojaribu kusalia madarakani.

“Hakuna faida yoyote ya kiongozi kung’ang’ania madaraka. Kule DRC uliona hali ilivyokuwa Kabila alipojaribu kung’ang’ania mpaka Kanisa Katoliki lilipohamasisha wananchi kuandamana kupinga hali hiyo,” anasema.

Anasema kwa kuwa viongozi wanapochaguliwa huapa kuilinda katiba, waendelee kuiheshimu hata kama wanaiona haifai.

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza anasema hali hiyo hutokana na viongozi kujiona bora kuliko wengine.

“Mnaweza kumuona ni kiongozi mzuri, lakini kumbe ana madudu yake, hivyo ili kuendelea kuyaficha atalazimika kung’ang’ania madarakani ili yasifahamike kwa wananchi,” anasema Ruhuza ambaye ni mdhamini wa chama hicho.

Mjadala huo umemwibua pia Fahim Dovutwa, mwenyekiti wa UPDP, anaungana na Ruhuza kuwa hali hiyo inatokana na kujiona wao ni bora kuliko wengine.

“Suala hili linachangiwa kwa kisasi kikubwa na wapambe ambao wanawaaminisha watu kuwa nchi haiwezi kuendelea bila wao au watu wanaowapenda.

“Wakati ule Nyerere alipotangaza kung’atuka watu walilia na wengine kuzimia, lakini alishikilia msimamo wake na kuondoka. Hali hiyo imejirudia katika tawala zote kwa upande wa Tanzania Bara na visiwani,” anasema.

Anasema wapambe hao hushinikiza viongozi hao kutoondoka kutokana na kunufaika kimaslahi na uongozi uliopo.

Maelezo ya Dovutwa yanaungwa mkono na Kanali Ngemela Lubinga, anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM anayesema mawazo ya watu huwezi kuyazuia kujadili ukomo, lakini kinachozingatiwa na chama hicho ni katiba yake kwamba muda wa miaka mitano ukifika rais anayekuwa madarakani akitaka anawania tena anapewa nafasi na ikifika miaka 10 wanateua mwingine anaendelea.

Lubinga aliyezungumza katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni anasema hata wakati wa awamu ya kwanza walikuwapo watu ambao hawakutaka mwalimu Nyerere ang’atuke na mwalimu alisema walikuwa wanahofia nafasi zao.