Unajua kilichomo kwenye uyoga?

Uyoga ni chanzo kizuri cha madini ya chuma, shaba na protini ambayo hufanya vizuri katika mwilini wa binadamu.

Kama ulikuwa hufahamu, uyoga una nyuzi nyuzi nyingi ambazo husaidia kuweka sawa kiwango cha mafuta na sukari mwilini, pia wenyewe hauna mafuta.

Ofisa Mtafiti Mwandamizi wa Sayansi na Chakula, Francis Modaha anasema uyoga upo katika kundi la vitamini B kwa wingi, yaani vitamini B2 (Riboflavin), Niacin na Pantothenic acid.

Anasema kundi hilo la vitamini B huusaidia mwili kupata nishati lishe kutokana na virutubishi vya protini, mafuta na wanga.

Modaha anasema mbali na kuwa na vitamini B, pia una vitamini D na madini ya selenium ambayo husaidia kuimarisha kinga mwili.

“ Madini ya shaba yaliyopo katika uyoga, husaidia kuzalisha nishati lishe, mifupa laini mwilini na seli nyekundu za damu ambayo hubeba hewa ya oksijeni katika sehemu zote za mwili,” anasema Modaha.

Pia, anasema uyoga husaidia kuimarisha mishipa ya fahamu.

Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Chakula kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Dk Elifatio Towo anasema uyoga ni mzuri kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari kwa sababu unaiweka sawa sukari kulingana na mahitaji.

“Uyoga una vitamini C pamoja na kiasi kidogo cha vitamini A, ambazo husaidia kupambana na matatizo mbalimbali ikiwamo msongo wa mawazo,” anasema Dk Towo.

Pia, anasema vitamini B iliyopo katika uyoga, ina uwezo wa kuzuia uchovu wa mwili na akili hasa wakati wa kazi nyingi, huku vitamini B3 husaidia kupunguza kiwango cha lehemu mwilini, wakati vitamini B6 hupunguza hatari ya mtu kupatwa na shambulio la moyo.