Ushirika wa Bobi Wine, Besigye kutikisa kiberiti cha Museveni

Umaarufu wa muda mfupi wa msanii, Robert Kyagulanyi “Bobi Wine” katika siasa za Uganda umeonekana dhahiri kuitia hofu Serikali ya Rais Yoweri Museveni (75) ambaye ametawala kwa miongo mitatu sasa.

Bobi Wine ambaye ni mbunge wa Kyadondo Mashariki amekuwa akikamatwa mara akwa mara na polisi na kufunguliwa mashtaka mbalimbali likiwamo la uhaini ambalo alifunguliwa Agosti 2018 kwa madai kwamba alishambulia msafara wa Rais Museveni katika mji wa Arua uliopo Kaskazini Magharibi mwa Uganda.

Rekodi yake hiyo haina tofauti sana na ya mwenzake, Dk Kiiza Besigye, mpinzani wa siku nyingi wa Rais Museveni. Sasa wawili hao wamekaa chini ya mwavuli mmoja, People’s Power, nia yao ikiwa ni kumwangusha Museveni. Swali ni je, watafua dafu au wataishia tu kutikisa kiberiti?

Ushirikiano na Besigye

Bobi Wine na Dk Besigye wameahidi kushirikiana katika kundi linaloitwa People’ Power ili kuiondoa madarakani NRM ya Rais Museveni.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa hivi karibuni na wanasiasa hao ilieleza kuwa wamekubaliana katika kushirikiana kisiasa dhidi ya Rais Museveni.

“Tunaungana na vyama na vikundi vingine kutaka mageuzi, tunajua kwamba kumaliza haya mapambano ni muhimu kukaa pamoja,” alisema Bobi Wine.

Tamko la People Power, muungano unaoshirikisha wawili hao, walisema pande hizo mbili zitatekeleza shughuli zao za kisiasa kwa pamoja katika kutafuta njia za kumtoa madarakani Museveni.

Dk Besigye amewahi kusema kwamba miaka mingi ya Museveni kusalia madarakani ndiyo chanzo cha ukosefu wa usalama na mauaji ya watu mashuhuri nchini humo, hasa katika mji mkuu Kampala.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Uganda wanasema ushirikiano kati ya Bobi Wine na Kizza Besigye si tishio kwa serikali ya Museveni.

Wanaona tofauti ya sera na maslahi kati ya viongozi hao wawili inafanya kuwa vigumu kwa muungano au ushirikiano wa aina hiyo kuwa thabiti.

“Kila mtu ana nia yake na malengo yake, wameamua kukubaliana au kufanya jambo pamoja lakini wakati ukifika wa kusema tuchague mgombea wa muungano, watu wataanza kupata mawazo tofuati,” anasema mmoja wa wachambuzi aliyenukuliwa na BBC.

Ushirikiano huo unakuja katikati ya masaibu ambao wanasiasa hao wanakabiliana nayo kutoka kwenye vyombo vya dola.

Katika tukio ambalo inadaiwa msafara wa Museveni ulipigwa mawe, dereva wa Bobi Wine alikutwa amekufa kwenye gari baada ya kupigwa risasi.

Polisi nchini Uganda walisema kwamba dereva huyo alipigwa risasi kwa bahati mbaya wakati wakiwarushia risasi watu waliokuwa wakiupiga mawe msafara wa Rais.

Katika tukio hilo, Bobi Wine alikamatwa hotelini baada ya milango kadhaa kuvunjwa na polisi wakimtafuta.

Licha ya mkanganyiko wa taarifa hizo, Bobi Wine pamoja na watu wengine 32 walishtakiwa kwa kosa la uhaini ambalo adhabu yake ni kifo au kifungo cha maisha. Hata hivyo, tangu mwaka 2005, Uganda haijanyonga mtu kwa kosa la uhaini.

Bobi Wine (37) amekuwa mkosoaji wa Serikali ya Rais Museveni, jambo ambalo limemjengea chuki kwa upande mmoja na kwa upande mwingine, amepata umaarufu na kukubalika hasa kwa vijana chini ya miaka 30 ambao ni robo tatu ya watu katika nchi hiyo yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 40.

Umaarufu huo unatafsiriwa kuwa mwiba mkali kwa Museveni kwa sababu Bob Wine anatishia utawala wake aliouasisi tangu mwaka 1986 alipoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi.

Julai 24, 2019, Bobi Wine alitangaza kugombea urais dhidi ya Museveni katika uchaguzi wa mwaka 2021. Uamuzi wake huo umezidi kumweka kwenye mkandamizo zaidi kutoka kwenye vyombo vya dola.

“Kwa niaba ya watu wa Uganda, nitashindana na Museveni katika uchaguzi huru na wa haki wa mwaka 2021,” alisema msanii huyo wa muziki kwenye tukio moja mjini Kampala.

Agosti 6, Bobi Wine aliongezewa shtaka la kumkasirisha na kumkejeli Museveni katika kesi ya uhaini.

Pamoja na kesi, bado anakabiliwa na mashtaka mengine katika mahakama nyingine kwa kuongoza maandamano kupinga sheria inayoweka kodi kwenye mitandao ya kijamii na biashara zinazofanywa kupitia malipo ya simu za mkononi.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo aliliambia gazeti la Financial Times kwamba zaidi ya wabunge 50 wakiwamo 13 kutoka kwa chama tawala cha Rais Museveni cha NRM, wanamuunga mkono kwa uamuzi wa kuwania urais.

Katika mfululizo ya matukio yanayomwandama Bobi Wine, Agosti 5, mshirika wake wa karibu, Michael Kalinda maarufu kama Ziggy Wine alifariki dunia katika hospitali kuu ya Mulago nchini humo.

Ziggy alitekwa wiki chache zilizopita na watu wasiojulikana ambao walimpiga hadi akawa hatambuliki huku jicho lake likiwa limenyofolewa.

Kifo hicho kilitangazwa na Bobi Wine kupitia ukurasa wake wa Facebook. Alieleza kwamba rafiki yake huyo pamoja na kutekwa, kuteswa na kung’olewa jicho la kushoto, vidole vyake viwili vilikatwa kabla ya kutupwa katika geri la hospitali ya Mulago.

Msemaji wa Polisi, Fred Enanga alikaririwa na BBC akisema wamefungua faili ili kuchunguza kilichosababisha kifo cha Ziggy Wine.

Enanga anasema maofisa wa polisi wametumwa katika hospitali ya Mulago kukusanya ushahidi wa kanda za CCTV ili kubaini ni gari gani lililomtupa msanii huyo katika hospitali ya Mulago.

Kuibuka kwa Bobi Wine

Nje ya muziki, Bobi Wine alianza kuwa maarufu kisiasa mwaka 2017 baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Kyadondo Mashariki, yeye akiwa kama mgombea binafsi.

Wachambuzi wa mambo wanasema alifanikiwa kushinda kwa sababu tayari alikuwa maarufu kutokana na muziki.

Tangu wakati huo, amekuwa akiwafanyia kampeni wagombea wengine wa upinzani na kushinda chaguzi ndogo.

Jambo hilo limemfanya kuonekana ana nguvu kubwa ya ushawishi na watu wengi wamekuwa wakimtaka agombee urais.

Lakini Bobi Wine anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.

Mwanasiasa huyo anakabiliwa na mashtaka mengi kama ilivyo kwa mpinzani wa muda mrefu wa Rais Museveni, Dk Kiiza Besigye ambaye pia anakabiliwa na kesi ya uhaini na nyinginezo kadhaa.

Sasa wanasiasa hao wameunganisha nguvu zao katika siasa za Uganda kuelekea uchaguzi wa 2021.

Bobi Wine ameapa kumng’oa madarakani Rais Museveni kwa madai kwamba nchi hiyo inahitaji kiongozi mwingine ambaye atatengeneza ajira kwa maelfu ya vijana ambao hawana kazi licha ya kwamba wamesoma mpaka vyuo vikuu.