Utata mzozo wa Diamond, Ali Kiba

Saturday November 2 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Unaweza kusahau tukio la Diamond na Ali Kiba kupena mikono kwenye msiba wa kupeana mikono kwenye msiba wa video queen, Agness Masogange katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni.

Wakati huo, Ali Kiba hakutoa mkono wote kumsalimu Diamond aliyemfuata kumsalimu, lakini angalau uso wake ulipambwa na tabasamu lililotafsiriwa kuwa wawili hao hawana ugomvi isipokuwa mashabiki wao.

Lakini tukio la siku chache zilizopita linaweza kutafsiriwa vingine na kurudisha nyuma kumbukumbu nyingi za masuala mengi baina ya wawili hao kuweza kujua kinachowafanya wasiive jiko moja.

Juzi, Diamond akitangaza kwa waandishi wa habari tamasha la Wasafi, aliulizwa kuhusu uwezekano wa kumwalika Ali Kiba na Harmonise, na jibu lake likawa rahisi tu; menejimenti yake inawasiliana na ya Ali Kiba kuhusu ushiriki huo.

Baadaye mchana moshi ulifuka. Ali Kiba aliandika Instagram maneno ambayo yanaonekana kumjibu Diamond; alisema kuna mtu analeta mambo ya darasa la pili ya kumuibia penseli na baadaye kumwambia amsaidie kuitafuta.

Hakuishia hapo, alisema huyo mtu ndio amekuwa akimkwamisha na kwamba akiamua kueleza mambo yake, hakuna mtu ambaye ataweza kuhudhuria hilo tamasha.

Advertisement

Hapo ndipo mashabiki na wadaui wa sanaa walipoona dhahiri kuwa kuna moto chini ya moshi uliofuka mchana huo.

Hakuna sababu ya wazi inayojulikana kuhusu ugomvi wao waliong’ara kwa nyakati tofauti; wakati Diamond anaibuka Ali Kiba alishapata mafanikio, si ndani ya nchi tu bali nje pia.

Lakini wasanii hao walikuwa marafiki ambao walidhaniwa wangeweza kufanya makubwa.

Diamond Platnumz aliwahi kukaririwa akisema alitaka kuingiza sauti kwenye wimbo wa Kiba unaoitwa “Single Boy”, lakini alikataliwa kwa madai kuwa alikuwa anataka mteremko.

Madai hayo yalikanushwa vikali na Kiba mwaka 2015 alipofanya mahojiano na gazeti hili. Alikiri kuwa na mgogoro na Diamond kwa miaka mitatu, lakini akasema hautokani na wimbo huo kama alivyodai Dai.

Kiba alidai kuwa katika wimbo huo alishirikiana na Lady Jaydee. Pia mara kadhaa Ali Kiba aliwahi kukaririwa akiwaambia watu wake wa karibu kuwa aliimba na Diamond wimbo “Lala Salama”, lakini ulipotoka haukuwa na sauti yake.

Wakati Ali kiba alipotoa kibao cha “Seduce Me”, saa chache baadaye Diamond akatoa kibao cha “Zilipendwa”, kitu kilichotafsiriwa kuwa alitaka kumzima mwenzake.

Kilichofuata ni wafuasi wa wawili hao kuanza kushindana na pengine kuhasiana huku wengine wakiwasihi kuingia studio pamoja ili kutuliza hali.

Mashabiki wa kila msanii hawamkubali mwingine na kila mmoja anapotoa wimbo, mashabiki huangalia upande wa pili kuna nini.

Advertisement