Vitambulisho vya machinga vyaibua mambo

Dar es Salaam. Vitambulisho vilivyotolewa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo vinazidi kuibua changamoto na uchunguzi wa Mwananchi umebaini matatizo matano.

Vitambulisho hivyo vilitolewa kwa wafanyabiashara ambao mtaji wao hauzidi Sh4 milioni na Rais John Magufuli ameweka bayana kuwa mwenye kitambulisho hicho asidaiwe kodi yoyote na halmashauri aliyopo.

Rais Magufuli aliamua kutengeneza vitambulisho 670,000 na kuwagawia wakuu wa mikoa Desemba 10, 2018 ili nao wawape wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri wavigawe kwa machinga.

Lakini mazingira ya utendaji kazi ya wafanyabiashara hao, ulinzi waliopewa na masuala mengine yamesababisha kuibuka vita kati yao na wafanyabiashara wenye leseni, baadhi ya halmashauri kulalamikia kushuka kwa mapato, usumbufu unaotokana na vitambulisho kutokuwa majina wala picha, kutoheshimiwa kwa katazo la kuwatoza kodi na urasimu katika upatikanaji.

Mvutano Arusha

Mkoani Arusha, uchunguzi umebaini vijana wenye vitambulisho hivyo, maarufu kama machinga, hupanga bidhaa zao mbele ya maduka na hivyo kuwa chanzo cha mgogoro baina ya pande hizo mbili.

Katika kata ya Levolosi eneo la Rangers Safari, mwenyekiti wa wafanyabiashara wenye maduka, Daniel Mollel alisema Machinga wanatumia vibaya kauli ya Rais kwamba wasibughudhiwe na ndio maana wanapanga bidhaa zao mbele ya maduka.

Naye mwenyekiti wa machinga wa Jiji la Arusha, Amina Njoka amesema chuki kati ya wafanyabiashara ni ya muda mrefu iliyosababisha kufikishana uongozi wa jiji hilo.

“Tuna mgogoro na wafanyabiashara wakubwa kuhusu maeneo ya biashara tunaomba sasa kupatiwa ufumbuzi,” alisema na kudai tatizo ni kutofahamiana kwa viongozi wa pande zote ili kuutatua.

Halmashauri zaathirika kimapato

Lakini vitambulisho hivyo havijaathiri wafanyabiashara wenye leseni pekee, bali pia mapato ya halmashauri.

Akizungumzia mchakato wa utoaji vitambulisho, meya wa jiji, Kalist Lazaro alisema ni jambo zuri lakini limeanza kuonyesha athari za kupunguza mapato ya jiji katika masoko mbalimbali.

Lazaro anasema katika masoko, walikuwa wakikusanya ushuru wa Sh500 kwa siku ambapo kwa mwezi ni wastani wa Sh18,000 lakini sasa kwa mwaka wanalipa 20,000 tu za kitambulisho cha Machinga.

“Hatujafanya tathmini ya kutosha lakini ukweli ni kuwa kuna athari katika masoko na Arusha tuna masoko makubwa ya Kilombero na Soko Kuu la Arusha,” alisema meya huyo.

Wajasiriamali bado watozwa ushuru

Pamoja na Rais kusisitiza kuwa Machinga wasitozwe kodi, mkoani Katavi, wamelalamikia kutozwa ushuru wakati wa usafirishaji kutoka kwenye maeneo wanayonunulia.

Chausiku Lyamba ambaye anajihusisha na biashara ya samaki Mpanda, alisema wamekuwa wakitozwa ushuru wa Sh15,000 hadi Sh20,000 hali ambayo inawarudisha nyuma kimaendeleo.

Akijibu malalamiko hayo, mkuu wa mkoa huo, Juma Homera alisema vitendo vinavyofanywa na trafiki ni rushwa, na akaahidi kwenda tena maeneo hayo kutoa maagizo ya kiserikali.

Kilio kama hicho kilitolewa na baadhi ya wajasiriamali mkoani Tanga. Thadeus Temu, mkazi wa Makorora Jijini Tanga, alidai yeye huuza mabusati kwenye magulio mbalimbali likiwamo la Tengamano, lakini maofisa wa TRA wamemfuata na kudai hakustahili.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema hakuna ruhusa kuwabughudhi wajasiriamali hao.