Vitambulisho vya wajasiriamali vyawavuruga viongozi, machinga

Muktasari:

Machinga wanavitumia kama kinga kufanya biashara katika maeneo hatarishi

Dodoma. Umiliki wa vitambulisho vya ujasiriamali kwa machinga kwenye Jiji la Dodoma umesababisha baadhi yao kupanga na kuuza bidhaa zao maeneo yasiyoruhusiwa na hatarishi.

Mwananchi lilishuhudia idadi kubwa ya wafanyabiashara wakiwa wamepanga bidhaa zao ndani ya stendi ya daladala hali inayohatarisha maisha yao kutokana na msongamano wa magari.

Mwaka jana mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi aliwahamisha wafanyabiashara hao soko la Sabasaba baada ya madereva wa daladala kugoma kutokana na stendi hiyo kuvamiwa na machinga.

Mgomo huo ulitokea baada ya mtu mmoja kufariki dunia katika stendi hiyo kwa kugongwa na daladala lililokuwa likiegeshwa.

Hata hivyo, ikiwa ni miezi kadhaa kupita kundi la wafanyabiashara hao kwa kutumia mgongo wa vitambulisho vya ujasiriamali limerudi kwa kasi.

Akizungumza jana mmoja wa madereva katika stendi hiyo, Mussa John alisema hali ya stendi ni mbaya kwa sababu machinga wameweka majiko ya mkaa na gesi hadi ndani ya kituo hicho jambo linahatarisha maisha ya watu.

“Hatuwakatazi kufanya biashara zao lakini waangalie na usalama. Tunapata shida kuegesha magari yetu hapa. Naomba wenye mamlaka wachukue hatua kabla hatari haijatokea,” alisema.

John alisema anafahamu wanatafuta riziki lakini kwa kufanyabiashara eneo hilo ni hatari kwasababu breki za magari zinaweza kufeli na kusababisha ajali.

Alipoulizwa ofisa masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna alisema jiji lilishafanya uhakiki wa machinga hao na kuwapangia kwenda masoko ya Sabasaba na Bonanza.

Hata hivyo, Yuna alisema zoezi la kuwahamisha limekuwa gumu kwa kuwa wanadai wana vitambulisho vya ujasiriamali vinavyowataka kufanya biashara eneo lolote bila kizuizi.

“Kuna wakati huwa tunawaondoa kwa kutumia mgambo lakini tukiondoka tu huku nyuma wanarudi bila kujali hatari iliyopo kuwa wanaweza kugongwa na gari na kusababisha vifo au vinginevyo,” alisema Yuna.

Agizo la JPM

Desemba 6, 2016 Rais John Magufuli alimuagiza Waziri na Katibu Mkuu (Tamisemi) kusitisha mara moja utekelezaji wa kuwaondoa machinga maeneo ya mijini mpaka mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha machinga.

“Kumeibuka tabia ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwafukuza wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, hili jambo sio sawa hata kidogo.” alisema.