Wabunge waliohamia CCM njiapanda

Dar es Salaam. Wabunge na madiwani waliohama vyama na kupewa fursa ya kuchaguliwa tena katika nafasi hizohizo kwenye vyama vingine, wako njiapanda kuhusu nafasi zao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2015, CCM imekuwa inavuna wanachama wapya kutoka katika vyama vya upinzani wakiwamo wabunge, madiwani na wanachama wa kawaida.

Chadema na CUF ni miongoni mwa vyama ambavyo makada wake wamehama kwa wingi na kupitishwa na CCM kuwania nafasi zilezile na kushinda.

Hali hiyo mbali na kuviathiri kisiasa vyama vya upinzani, imeinufaisha CCM kwa kuongeza wanachama na ruzuku kutoka Sh12.4 bilioni kwa mwaka 2015/16 hadi Sh13.5 bilioni ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh1.1 bilioni.

Licha ya waliogombea na kushinda kirahisi kupitia CCM, wachambuzi wanabainisha jinsi ambavyo wanasiasa hao wanavyotazamwa ndani ya chama, na kizingiti cha kura za maoni, tofauti ya namna ya walivyochujwa katika uchaguzi mdogo.

Wana kazi ya ziada

Wachambuzi hao wa masuala ya siasa wanasema wanasiasa watakuwa na kazi ya ziada katika uchaguzi ujao.

“Kwanza hawana mizizi ndani ya CCM, pili ule upendeleo wa kuteuliwa nje ya mchakato hautakuwepo kwa sababu lengo la kudhoofisha upinzani lilishafanikiwa,” alisema Profesa Gaudence Mpangala, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu).

“Watakaofanikiwa kupenya ni wale watakaobebwa na utendaji na historia yao binafsi,” aliongeza.

Mchambuzi mwingine na mtetezi wa haki za binadamu, Edwin Soko alisema kwamba wabunge na madiwani hao watakumbana na ule usemi wa “ng’ombe aliyekatwa mkia” uliowahi kutamkwa na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuwa anakuwa tofauti.

Vilevile, katika mazingira ya sasa ambayo vyama vinakwepa migawanyiko wakati wa uteuzi, haitarajiwi kuwa rahisi kupitisha wagombea kwa njia ileile ya uchaguzi mdogo ili kuepuka kupoteza kirahisi.

“Wengine wameshasema wanahama majimbo, hao wanajua hawana lao iwe CCM hata huko upinzani walikotoka,” alisema Athumani Miraji, mkazi wa Kitunda jijini Dar es Salaam.

Kauli ya wabunge

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wabunge waliohama Chadema kwenda CCM walisema wanakusudia kutetea nafasi zao katika uchaguzi mkuu ujao na wanaamini watashinda wakipewa nafasi.

“Nikiteuliwa nina uhakika wa kushinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa sababu wapiga kura wananikubali kutokana na utendaji wangu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta ya maji, elimu, kilimo na barabara,” alisema Pauline Gekul wa Babati Mjini.

Kwa upande wake Dk Godwin Mollel, mbunge wa Siha (CCM) alisema licha ya kujijengea uaminifu na kukubalika miongoni mwa wapiga kura, atalazimika kufanya kazi ya ziada kushinda mchakato ndani ya chama.

Alisema hali hiyo inatokana na kukabiliana na nguvu mbili, moja kutoka Chadema na nyingine ndani ya CCM.

“Nikiwa Chadema mwaka 2015, nilijenga mfumo imara na madhubuti ulioshinda mfumo wa CCM na kuniwezesha kuibuka mshindi, sasa nimerejea CCM ambako nalazimika kupambana na mfumo ule nilioushinda pamoja na mwingine nilioujenga Chadema.”

“Hapo ndipo kuna kazi, lakini tutakabiliana nayo,” alisema Dk Mollel.

Kikwazo kingine

Wakati wimbi la wabunge na madiwani kuhamia CCM linaanza madiwani kadhaa mkoani Arusha waliangushwa katika kura za maoni, kabla ya vikao vya juu kuagiza wateuliwa, hatua inayoashiria kuwa inaweza kuwatokea hata wengine.

Wabunge waliopita

Wabunge waliojiuzulu nafasi hiyo na kufanikiwa kutetea nafasi zao kupitia CCM, saba kutoka Chadema na watatu kutoka CUF ni Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Chacha Ryoba (Serengeti),Godwin Mollel (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Joseph Mkundi (Ukerewe).

Kwa upande wa CUF ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Zuberi Kachauka (Liwale) na Abdallah Mtolea wa Temeke.

Mameya nao wamo

Mbali na wabunge hao, kuna idadi kubwa ya madiwani wakiwamo ambao ni mameya na wenyeviti wa halmashauri ambao walichukuliwa katika mkondo huo.

Miongoni mwao ni aliyekuwa meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko alijiengua Chadema na kujiunga na CCM na nafasi hiyo kumwachia aliyekuwa naibu meya, Omary Kumbilamoto (CUF).

Hata hivyo, Kumbilamoto naye baadaye alijiengua CUF na kujinga na CCM, kisha akachaguliwa kuwa meya.

Pia lipo sakata la meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro ambaye alijiengua hivi karibuni kutoka Chadema na kujiunga na CCM, lakini hajapata fursa ya kuwania tena kwa kuwa muda ulikuwa umekwisha kisheria.

Katika baadhi ya maeneo ambapo upinzani ulishinda halmashauri, juhudi zimekuwa zikilenga kuhamisha wingi wa madiwani kutoka upinzani kwenda upande wa pili ili kuuwezesha kupata meya.

Baadaye Kamati Kuu ya CCM iliyokaa Oktoba 30, mwaka jana ilitangaza Novemba 15 ingekuwa tarehe ya mwisho kupokea maombi ya wenye nia ya kujiunga na chama hicho na kupewa dhamana ya uwakilishi kwa wabunge na madiwani kutoka vyama vingine.

Akitangaza uamuzi huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphey Polepole alisema kwamba baada ya tarehe hiyo hakuna kiongozi yeyote atakayepewa nafasi ya kugombea kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi wa marudio, badala yake watakuwa wanachama wa kawaida.

Hata hivyo, makada wengine wameendelea kupokewa wakiwamo wanasiasa maarufu wa upinzani walioamua kurudi CCM wakieleza sababu mbalimbali, zikiwamo za kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kuleta maendeleo au kutoridhishwa na demokrasia ndani ya upinzani.

Miongoni mwao ni aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa, waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa. Vilevile, waziri mkuu mwingine mstaafu, Frederick Sumaye naye alijiunga na CCM hivi karibuni akitokea Chadema siku chache baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti Kanda ya Pwani.

Vilevile, wiki hii aliyekuwa mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) amejiuzulu nafasi hiyo na kujiunga na CCM ikiwa ni baada ya kuwania uenyekiti Chadema na kuambulia kura chache. Kabla vumbi la Mwambe halijatua aliyekuwa Katibu mkuu wa Chadema na kuenguliwa wakati wa uchaguzi ndani ya chama hicho Desemba mwaka jana, Dk Vincent Mashinji naye amejiunga na CCM.

Kulingana na matamshi mbalimbali ya viongozi na makada wa CCM na hata upinzani, bado inatarajiwa makada zaidi wa upinzani kujiunga na chama hicho tawala.