Wabunge wapya wajinasibu kuchapa kazi kweli

Muktasari:

Baadhi ya wabunge wapya wamesema itawachukua muda mfupi kujifunza utendaji wa Bunge na kuzielewa kanuni kuifanya kazi ya uwakilishi vizuri.

Dodoma. Baadhi ya wabunge wapya wamesema itawachukua muda mfupi kujifunza utendaji wa Bunge na kuzielewa kanuni kuifanya kazi ya uwakilishi vizuri.

Kabla Spika wa Bunge, Job Ndugai hajaanza kuwaapisha wawakilishi hao wa Bunge la 12, aliwaomba wazisome kwa umakini kanuni za kudumu za Bunge n akuzielewa.

“Humu ndani huwezi kuofanya chochote bila kujua kanuni… tumeandaa semina tutakazoanza baada ya Bunge hili kuahirishwa ambazo zitasaidia kuwafungua macho,” alisema Ndugai.

Mbunge huyo wa Kongwa alisema zipo taratibu zinazoelekeza utaratibu wa mavazi ambazo wasipozipata watarudishwa na habari kuwafikia wapigakura wao kupitia vyombo vya habari.

Ndugai alitoa ushauri huo akizingatia ukweli kwamba kuna wabunge wengi wapya wakiwamo 170 kati ya 264 waliochaguliwa kwenye majimbo ya uchaguzi. Ndani ya Bunge hili, CCM ina wabunge 366 huku vyama vya upinzani vikiwa nao 27 tu kati ya 393 wanaotakiwa.

Wakizungumza katika viwanja vya Bunge jana, baadhi ya wabunge wapya walisema wanahitaji wiki moja kujifunza na kuzielewa kanuni hizo na kuzielewa ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi bila mgongano.

Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi alisema “kama kawaida yangu huwa najifunza nikiingia eneo jipya na ninajifunza kwa haraka. Itanichukua wiki moja kuzisoma na kuelewa Kanuni za Bunge.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga alisema kwa siku mbili alizokaa bungeni ameona mshikamano mkubwa walionao wabunge.

“Ukitazama wabunge wapya tunaweza kuwa wageni bungeni lakini si wageni wa mawazo. Mawazo tunayo, tunataka kuingia na kufanya pale walipoachia wenzetu na sisi tukaendeleze,” alisema.

Mwakilishi wa Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya alisema kwa muda mfupi aliokaa bungeni amebaini Bunge la 12 lina wabunge wengi vijana, wengi wakiwa wasomi.

“Nyie wenyewe ni mashahidi safari hii tumeingiza madaktari maprofesa, digrii, diploma. Tunahitaji huu mchanganyiko kwa sababu katika maisha yetu tunahitajiana kwa namna moja ama nyingine,” alisema.

Alisema Bunge hilo litakuwa na ufanisi mkubwa kwa sababu limeingiza vijana wanaojitambua, wasomi ambao anaamini wataisimamia Serikali, kuchambua sera, bajeti na kuangalia vipaumbele ambavyo CCM imepanga kuvitekeleza ndani ya miaka mitano ijayo.

Naye mbunge wa Kwela, Deus Sangu alisema Bunge la 12 lina mchanganyiko wa watu wengi wenye ari ya kufanya kazi.

“Asilimia kubwa ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwa sababu hiyo tulipokuwa tunanadi ilani yetu tulitamani majimbo yote ndani ya Tanzania na kwa asilimia kubwa tumelitimiza hilo naamini tutaenda kuongea lugha moja ya kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema.

Kuhakikisha kero zinamalizwa alisema wataendelea kupaza sauti kuwatetea wananchi waliwawatuma ambao waliwaamini kuwa wanaweza kuifanya kazi hiyo.

“Kwanza ni kujitambua kuwa tuna dhamira gani na kwa wajibu huo tutafanya yale ambayo Watanzania wanayatazamia na wala hakutakuwa na shida,” alisema.

Kutoka Mufindi Kusini, David Kihenzile alisema Bunge la 12 ni tofauti kidogo na mabunge mengine yaliyoundwa tangu mfumo wa vyama vingi uingie nchini.

“Kwanza ni Bunge la kwanza tangu nchi iingie kwenye uchumi wa kati kwa hiyo ni Bunge la kuivusha Tanzania kwenda mbele zaidi lakini kwa taswira ya watu wengine ni Bunge ambalo tangu uingie mfumo wa vyama vingi limejaa wanaCCM wengi zaidi,” alisema.

Licha ya wingi wa wabunge wa CCM, Kihenzile alisema matarajio yake kwa Bunge hilo ni kupata uwakilishi mzuri wa wananchi.

Alisema Rais Magufuli amefanya mambo makubwa katika miaka mitano iliyopita na katika mitano mingine ijayo atafanya makubwa zaidi.

“Kama katika miaka mitano iliyopita Taifa lilikuwa linakimbia kwa spidi ya kilomita 120, Bunge hili linakwenda kuikimbiza Serikali kwa zaidi ya spidi ya kilomita 200 ili mambo ambayo hayakukamilika katika miaka mitano ya kwanza yakamilike kwa miaka michache ijayo,” alisema Kihenzile.

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alisema kwa sababu ameingia bungeni wakati Rais Magufuli ambaye anajipambanua kuwa mpenda maendeleo, ni kipindi kizuri cha kuwasemea wapiga kura wake.

Alisema utakuwa wakati mzuri wa kuwasemea wakazi wa Arusha mjini bungeni na kuzuishughulikia changamoto zao ikiwamo upatikanaji maji, ubovu wa barabara, umeme, huduma za sekta ya utalii, madini na masuala ya maendeleo kwa ujumla.

“Mimi ninawaahidi wananchi nitakuwa sauti yao ndani ya Bunge, nitawasemea changamoto zao, nitawasemea kero zao ili Arusha yetu iweze kuwa Calfonia kama vile Rais Magufuli alivyoahidi kwenye kampeni zake Arusha,” alisema.